Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni: Watoto Ni Jeuri ya Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 26 Mei 2024 ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wote waliojibidiisha kuandaa na hatimaye, kufanikisha maadhimisho haya katika ubora wake. Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Watoto Ulimwenguni “World Children’s Day yataadhimishwa mwezi Septemba 2026. Amewakumbusha watoto kwamba, katika maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu wamemtafakari Mungu Baba kama Muumbaji, Mungu Mwana kama Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayelitakatifuza na kuliongoza Kanisa. Amewataka watoto kuwasalimia wazazi na walezi wao. Naye Padre Enzo Fortunato Mratibu wa Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni “World Children’s Day Rome 2024, Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, 26 Mei 2024 amewakumbusha watu wa Mungu kwamba, tema na kauli mbiu iliyochaguliwa kwa Maadhimisho haya yaani “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5 ni maneno ya Kristo Yesu mwenyewe; maneno angavu yanayotangaza majira mapya. Kumbe, Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni “World Children’s Day Rome 2024, ni mwaliko wa matumaini na wito wa kutembea kwa pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Siku ya Kwanza ya Watoto Ulimwenguni “World Children’s Day Rome 2024, ni kielelezo makini cha utashi wa Baba Mtakatifu Francisko, kielelezo cha unabii kwa watu wa Mungu nyakati hizi.
Huu ni ujumbe unaokita mizizi yake katika sakafu ya nyoyo ya watu wazima, kwa njia ya watoto wasiokuwa na mawaa mbele ya Mungu. Katika maadhimisho haya, watoto wenye tabasamu la kukata na shoka, limejionesha kwenye nyuso za walimwengu waliochoka na kujeruhiwa vibaya sana. Kwa upande wake Roberto Benigni, Msanii maarufu sana nchini Italia amesema vita ni kati ya dhambi kuu zinazoendelea kumchafua mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Amewataka watoto kuwa ni wadau katika maisha yao, tayari kujikita katika ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi. Amewataka watoto kuendelea kuota ndoto, kwa kutambua kwamba, wao kimsingi ni mashujaa, wathubutu kutenda hasa yale mambo magumu katika maisha yao, daima wakiwa na macho wazi; watambue kwamba, wao ni moto wa kuotea mbali.
Umefika wakati wa kusitisha vita, kinzani na misigano kwani wanapocheza watoto, mmoja wao akiumia, mara mchezo mzima unasitishwa kwa muda. Kumbe, kuna haja ya kusitisha vita vinavyoendelea kudharirisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hotuba ya Mlimani au Heri za Mlimani ni: dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo. Ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Anawataka kwa namna ya pekee: Wawe na huzuni na umaskini wa roho; wawe na njaa na kiu ya haki; wawe na rehema, wenye moyo safi na wapatanishi. Heri nane ni faraja ya Roho Mtakatifu kwa wale ambao wamekombolewa na kuweka nyoyo zao wazi kwa ajili ya kupokea neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, wako huru. Heri za Mlimani ni chemchemi ya furaha ya upendo aminifu wa Mungu unayobubujikia maisha ya waamini! Hii ni furaha endelevu ambayo hakuna mtu wala mazingira yanayoweza kuwapokonya watoto wapendwa wa Mungu. Hili ni wazo jema kwa binadamu katika ulimwengu mamboleo.
Roberto Benigni, amewataka watoto kuthubutu kutenda hata kama wakikosea, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kila mtoto anachangia katika kuboresha maisha, kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Amewataka watoto kupenda kile wanachotenda, ili kushiriki katika ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi, ili watoto waweze kuwa na furaha. Hii ndiyo ndoto ya watoto wengi kuweza kucheka na kufurahia maisha na kama ikitokea basi hii itakuwa ni siku njema zaidi katika historia ya Ulimwengu.