Mapadre Vijana Shikamaneni na Mapadre Wazee Katika Maisha na Utume wa Kipadre
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kuna fursa, matatizo na changamoto nyingi zinazowakumba Mapadre na kwamba, Kanisa halina budi kusoma alama za nyakati, kwa kuibua mbinu na mikakati mipya itakayoliwezesha Kanisa kuendelea kuwa ulimwenguni pamoja na kutekeleza dhamana yake ya Uinjilishaji, katika misingi ya ukweli na uwazi. Kanisa linatambua kwamba, katika miaka ya hivi karibuni limetikiswa kwa kashfa mbalimbali, lakini bado limeendelea kusherehekea vipindi vya umoja na furaha, kwa kuonesha uzuri wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu huu wa utandawazi, kuna hatari kubwa ya baadhi ya watu kujikuta wakiwa wamejifungia katika dhana ya mawazo mepesi mepesi, kwa kuonesha ukavu katika maisha ya kiroho kama ambavyo aliwahi kudokeza Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2005. Mama Kanisa hana budi kuhakikisha kwamba, anatumia rasilimali na uwezo wake wote katika mchakato wa maboresho ya wito na utambulisho wa maisha na utume wa Kipadre, kwa kufuata nyazo za Kristo Yesu, Mchungaji mwema kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Familia ya Mungu inawahitaji viongozi waliopakwa mafuta na Roho Mtakatifu si kwa ajili yao binafsi, bali kwa ajili ya huduma ya upendo, tayari kutoka kimasomaso ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili hususan miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Huu ni utume unaofumbatwa katika huduma makini kwa kujishikamanisha na Kristo Yesu kwa njia ya sala, tafakari na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yanayomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu. Majiundo ya maisha na utume wa Kipadre ni mchakato endelevu unaowajengea Mapadre uwezo wa kuwa kweli ni wafuasi amini wa Kristo Yesu. Ni malezi na majiundo ya: kiakili, kiutu na kiroho. Ikumbukwe kwamba, malezi awali na endelevu yanapaswa kutofautishwa kwani yanagusa maisha ya Kipadre kwa nyakati tofauti, ingawa lengo ni kumuunda Padre mkamilifu. Mapadre wakumbuke kwamba, wameteuliwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya mambo matakatifu; kumbe, wanapaswa kutambua wito na utambulisho wao, tayari kuzaa matunda yanayokusudiwa. Wito ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayoimarishwa kwa njia ya malezi ya Jandokasisi tangu mwanzo hadi mwisho wa maisha yake kama Padre, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa ili: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, yote haya ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na Mapadre 70 wa Jimbo kuu la Roma wanaoadhimisha kumbukizi ya miaka 40 na kuendelea tangu walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mkutano huu umefanyika kwenye Parokia ya “San Giuseppe, eneo la Trionfale, Roma. Kati yao alikuwepo Don Antonio Ciamei mwenye umri wa miaka 94 na tayari ameadhimisha kumbukizi ya Miaka 70 tangu alipopewa Daraja takatifu ya Upadre. Haya ni mazungumzo yaliyofanyika kwa faragha, lakini Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mambo mengine, amekazia umuhimu wa Mapadre wazee kushikamana na Mapadre vijana, katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mapadre wamemshirikisha Baba Mtakatifu, fursa wanazokirimiwa na Mama Kanisa, matatizo, changamoto na matumaini yao kwa leo na kesho katika maisha na utume wao kama Mapadre. Mapadre wazee wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na kamwe wasitelekezwe kama “Daladala iliyokatika usukani.”
Baba Mtakatifu alipata nafasi pia ya kusalimiana na watoto wanaojifunza Katekesi parokiani hapo. Itakumbukwa kwamba, Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana, urithi na utajiri wa imani; matunda ya Mafundisho ya kina kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hiki ni chombo mahususi cha kusaidia mchakato wa ukuaji na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chachu ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko katika azma nzima ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Katekisimu ambayo ni muhtasari wa Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Ni muhtasari wa adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Sakramenti za Kanisa, Sakramenti za Kristo, Sakramenti za wokovu, imani na uzima wa milele. Lengo la maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Katekisimu ni muhtasari wa dira na mwongozo wa Maisha ya Kikristo na Adili unaofumbatwa katika Amri kumi za Mungu zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha: kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani, kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katekisimu ni muhtasari wa Maisha ya Sala kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale na Sala kuu ya Baba Yetu kama ilivyofundishwa na Kristo Yesu kwa kubeba mafundisho mazito katika maisha na utume wake. Hii ni kazi iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II kama chombo muhimu sana cha maisha na utume wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo.