Mwenyeheri Giuseppe Rossi, Paroko, Shuhuda wa Imani na Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, Fumbo la Utatu Mtakatifu sana ndilo Fumbo la Msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Kwa hivyo ni chemchemi ya mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayowaangaza. Hili ni fundisho la kweli ya imani. Imani Katoliki ndiyo hii: Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kuchanganya nafsi, wala kutenganisha uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, nyingine ya Mwana na nyingine ya Roho Mtakatifu, ni umungu mmoja, wa Baba, na wa Mwana na wa Roho Mtakatifu; utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja wa milele. Rej. KKK 222-266. Ni katika maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Dominika tarehe 26 Mei 2024, huko Jimboni Novara, Italia, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Wenyeheri na Watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Mtumishi wa Mungu Giuseppe Rossi, kuwa ni Mwenyeheri. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 29 Mei 2024 amesema Mwenyeheri Giuseppe Rossi alikuwa ni Paroko mwenye ari na moyo mkuu wa upendo; shuhuda wa imani yake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Aliyesimama kidete kuwalinda na kuwatetea Kondoo wake wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kiasi hata cha kusadaka maisha yake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, ushujaa wake, utakuwa ni mfano bora wa kuigwa, wakati waamini wanapokabiliana na majaribu katika maisha, wapambane kikamilifu kwa kutumia fadhila ya nguvu. Ni mfano bora wa kuigwa na waamini walei wanaotekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa, na kwamba, mfano huu unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo na kwa njia hii, wanashiriki pia mateso na kifo chake Msalabani, kama ilivyokuwa kwa Mwenyeheri Giuseppe Rossi, Padre na Shahidi wa imani aliyeuwawa huko Castglione Ossola kwa chuki dhidi ya imani “In odium fidei” na kikosi cha Mafashisti mnamo tarehe 26 Februari 1945.
Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Wenyeheri na Watakatifu anasema, Mwenyeheri Giuseppe Rossi, alizaliwa tarehe 3 Novemba 1912 huko Varallo Pombia, Jimbo Katoliki la Novara. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 29 Juni 1937 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre; Kuhani aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na hatimaye, akayamimina maisha yake kwa ajili ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mtakatifu Paulo Mtume anasema, “Bwana wetu Yesu Kristo, usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema; Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema; Kikombe hiki ni Agano Jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo kwa ukumbusho wangu” (1Kor.11:23-25). “Maana kila mlapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.” 1Kor 11:26. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema, Kristo Yesu, usiku ule alipotolewa aliweka Sadaka ya Ekaristi Takatifu ya Mwili na Damu yake Azizi, ili kuendeleza Sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi kusudi aliachie Kanisa, ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu; Sakramenti ya Utakatifu “Sacramentum pietatis”, ishara ya umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo Kristo Yesu huliwa, na roho hujazwa neema, na hutolewa amana ya uzima wa milele. Rej. Sacrosanctum concilium, 47.
Huu ni muhtasari wa haki na huruma; kifo na maisha; uchungu na furaha, ili kuweza kuufahamu Ukuhani wa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Kumbe, kuna uhusiano wa ndani kabisa kati ya Ukuhani na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Mwenyeheri Giuseppe Rossi, katika maisha na utume wake kama Paroko alijiaminisha kwa Kristo Yesu, kiasi hata cha kufuata nyayo zake katika Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari, kiasi cha kuendelea kuteseka kwa furaha kwani aliamini kwamba, kwa njia hii alikuwa anaungana na Kristo Yesu katika mateso yake juu ya Msalaba. Huu ni mwaliko kwa waamini kutafakari kwa kina Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa Kristo Yesu unaotakasa dhambi zote za binadamu; kwa kuganga na kuponya madonda yake. Hivi ndivyo ilivyotokea tarehe 26 Februari 1945 Mwenyeheri Giuseppe Rossi, akabahatika kuwa ni Paroko wa maskini na wa watu wote, na Paroko shuhuda wa imani.