Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Mei 2024 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa ni kwa ajili ya kuombea malezi, makuzi na majiundo ya majandokasisi na walelewa wa maisha ya wakfu. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Mei 2024 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa ni kwa ajili ya kuombea malezi, makuzi na majiundo ya majandokasisi na walelewa wa maisha ya wakfu. 

Nia za Papa Francisko Kwa Mwezi Mei 2024: Malezi na Majiundo ya Majandokasisi na Walelewa

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Mei 2024 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa ni kwa ajili ya kuombea malezi, makuzi na majiundo ya majandokasisi na watawa, ili wakue katika neema, maisha ya sala, mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kwa njia ya malezi ya kibinadamu, kichungaji, kiroho na kijumuiya. Haya ni malezi yanayonga katika kukuza na kudumisha utu na tasaufi ya maisha na wito wa kipadre na kitawa

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekuwa ni changamoto kubwa ya kuangalia tena mchakato wa malezi na majiundo ya maisha, wito na utume wa kipadre na maisha ya kuwekwa wakfu ndani ya Kanisa, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hii inatokana na ukweli kwamba, mapadre na watawa si watu wa mshahara, bali ni wachungaji wa familia ya Mungu, wanaopaswa kwa namna ya pekee, kuwa ni watu wasikivu, wenye huruma na upendo kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Yesu aliwaonea watu huruma, akawasikiliza kwa makini, akawaganga na kuwaponya, akawasamehe dhambi zao na kuwapatia tena furaha ya kuendelea kuishi kwa imani na matumaini, kwani walikuwa wameonja na kukutana na Uso wa upendo na huruma ya Mungu katika safari ya maisha yao! Mambo makuu mawili yamepewa kipaumbele cha kwanza: “Utu” yaani, Majandokasisi na walelewa wanapaswa kusindikizwa ili waweze kuwa na ukomavu katika utu wa binadamu, ili kweli waweze kupenda na kupendwa katika hali ya ukomavu; watu huru kutoka katika sakafu ya maisha yao; watu wanaoweza kujenga na kudumisha mahusiano ya kijamii; watu wenye amani na utulivu wa ndani; wanaoweza kutoa na kupokea na kumwilisha Mashauri ya Kiinjili katika maisha yao bila shuruti, unafiki wala kutafuta njia ya mkato. “Tasaufi” ni neno la pili, linalopewa kipaumbele cha pekee katika malezi na majiundo ya kipadre na maisha ya wakfu kwa kufunda dhamiri nyofu mintarafu maisha na wito wa Kipadre na Kitawa. Ikumbukwe kwamba, Padre au Mtawa si mfanyakazi wa mshahara wala mfanyabiashara anayelitumia Kanisa kwa ajili ya mafao yake binafsi.

Malezi na Majiundo makini kwa walelewa maisha ya kitawa ni muhimu
Malezi na Majiundo makini kwa walelewa maisha ya kitawa ni muhimu

Padre na Mtawa ni mfuasi wa Kristo Yesu anayejisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwa kujenga na kudumisha uhusiano wa pekee na Kristo kwa njia ya Neno, Sakramenti, Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na sadaka binafsi, kielelezo cha Kristo mchungaji mwema. Mapadre wanapaswa kuboresha maisha yao ya kiroho yanayofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili kwa kujisikia kuwa na Kanisa kwa ajili ya Kanisa kama alivyokuwa Kristo Yesu. Mapadre na Watawa wanapaswa kuwa ni watu wa “Huduma” yaani “Wasamaria wema”, watu wenye huruma, upendo na msamaha. Hawa ni watu wanaopaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kwani katika maisha na utume wao, watakutana na watu wenye kiu ya kusikilizwa; watu wanaweza kuanzisha na kudumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi pasi ya kuwa na jazba au kutaka kulipiza kisasi. Ikumbukwe kwamba, ndani ya familia ya Mungu kuna watu ambao wamejeruhiwa vibaya wanapaswa kugangwa na kuponywa na huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, ushauri makini na ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Majandokasisi na Walelewa wanapaswa kuondokana na tabia ya kujifungia katika ubinafsi wao, tayari kujielekeza katika mwono mpana utakaowapatia mang’amuzi ya kina katika maisha na utume wao kwa siku za baadaye, kama Mapadre na Watawa.

Maaskofu na wakuu wa Mashirika ni walezi wakuu wa miito
Maaskofu na wakuu wa Mashirika ni walezi wakuu wa miito

Baadhi ya Mapadre na Watawa wanaishi na kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, kumbe wanahitaji kusindikizwa kwa njia ya sala na sadaka ili kamwe wasikate tamaa, hata pale wanapoteleza na kuanguka katika udhaifu wa kibinadamu wawe na ujasiri wa kusimama tena na kusonga mbele kwa imani na matumaini. Kanisa pia limebahatika kuwa na umati mkubwa wa Mapadre wema, watakatifu na wachapakazi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake bila hata ya kujibakiza, wote hawa wanapaswa kuungwa mkono ili waendelee kusonga mbele kwani mapambano bado kabisa yanaendelea hapa duniani, hadi kitakapoeleweka. Mapadre wajenge na kudumisha utamaduni wa maisha matakatifu katika utume wao wa Kipadre, kwa kuendelea kuboresha maisha yao ya kiroho kwa njia ya nyenzo ambazo zimewekwa na Mama Kanisa; waendelee kuwajibika barabara katika shughuli za kichungaji kwa kushirikiana na watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao. Mapadre na Watawa wawe makini na kuendelea kukesha daima katika sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti na matendo ya huruma, na kamwe wasidhani kwamba wamekwisha kufika, bali wako safarini na bado kuna vishawishi na changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kipadre na Kitawa!

Malezi ya Majiundo ya Majandokasisi yapewe uzito wa juu
Malezi ya Majiundo ya Majandokasisi yapewe uzito wa juu

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Mei 2024 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa ni kwa ajili ya kuombea malezi, makuzi na majiundo ya majandokasisi na watawa, ili wakue katika neema, maisha ya sala, mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kwa njia ya malezi ya kibinadamu, kichungaji, kiroho na maisha ya kijumuiya. Baba Mtakatifu anawataka majandokasisi na walelewa wa maisha ya kitawa wasiogope kuishi utakatifu kwani hii ni nguvu na furaha katika maisha na utume wao, hali itakayowawezesha kuwa ni waamini kutoka katika undani wa maisha yao. Kumtegemea na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, humweka mwamini huru na kumwongoza kutambua adhama yake kuu. Malezi, makuzi na majiundo ya kipadre na kitawa yawawezeshe majandokasisi na walelewa kuwa karibu na maisha ya watu watakaowahudumia, hili ni jambo muhimu sana. Ikumbukwe kwamba, malezi, majiundo na makuzi ni mchakato unaoendelea katika maisha na hatima yake ni kifo. Ndiyo maana kuna umuhimu wa kuendelea kujinoa; kiakili, kiutu, kihisia na katika maisha ya kiroho. Malezi haya yanaendelezwa pia katika Jumuiya, ingawa maisha ya kijumuiya yanachangamoto zake. Baba Mtakatifu anasema, maisha ya kijumuiya ni toba ya hali ya juu kabisa kama anavyokaza kusema Mtakatifu John Berchmans kwa lugha ya Kilatini kwamba, “Mea maxima poenitentia, vita communis.” Si rahisi sana kwani huu ni uhalisia wa maisha ya watu unaogusa matatizo, fursa na changamoto mbalimbali za maisha. Kuna wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko; kuna tabia ya watu wa kutaka kujimwambafai, kuna mashindano ambayo watu wanataka kujikuza na kujiona bora zaidi kuliko wanajumuiya wengine; hali ya kutoelewana, kinzani na misigano ya kibinadamu. Yote haya yanaendelea kujengeka taratibu katika nyoyo za watu, kiasi hata cha mapadre na watawa kushindwa hata kusalimiana kama ndugu katika Kristo Yesu.

Malezi ya kipadre na maisha ya wakfu yazingatie: utu na tasaufi ya wakfu
Malezi ya kipadre na maisha ya wakfu yazingatie: utu na tasaufi ya wakfu

Maisha ya kidugu katika jumuiya yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika sala, kwa kuombeana, kusaidiana na kutegemezana kwa hali na mali kwani, hakuna maisha pasi na mikwaruzano, kama haya yanaweza kutokea katika familia na maisha ya watu wa ndoa, sembuse watawa wanaokutanishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Daraja takatifu, ili kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani? Baba Mtakatifu anakaza kusema, kukosa na kukoseana ni jambo la kawaida katika maisha ya pamoja, kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu wa maisha, pasi na kubaki na kinyongo moyoni. Mapadre na Watawa wajifunze kusema na kushuhudia ukweli wa mambo bila woga, kielelezo makini cha ukomavu na uhuru kamili! Masengenyo na unafiki ni sumu mbaya inayopekenyua hata kuua maisha ya kijumuiya. Watawa wawe na ujasiri wa kushirikishana shida, mang’amuzi, uzuri na changamoto wanazokumbana nazo katika nadhiri zao, yaani: ufukara, useja na utii, kama kielelezo cha ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu! Watawa wawe ni nidhamu ya kuheshimu utu na heshima ya ndugu zao katika utawa na kamwe wasimpatie Shetani nafasi ya kuchafua utu na heshima ya ndugu zao katika Kristo Yesu!

Mwezi Mei 2024
28 May 2024, 15:33