Papa kwa Siku ya I ya Watoto Duniani:Amani itarudisha tabasamu kwa watoto!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika tukio kuu kwa utashi wa Baba Mtakatifu kuadhimisha Siku ya I ya watoto Duniani, Baba Mtakatifu Francisko amewakarisha na kuwasalimia watoto kutoka mataifa yote ulimwenguni waliokusanyika katika Uwanja wa Olimpiki Mjini Roma, Jumamosi tarehe 25 Mei 2024. Akianza hotuba yake amesema “watoto wapendwa na vijana: Tuko hapa! Matukio ya Siku ya Watoto Duniani yameanza.
Tumekusanyika hapa kwenye Uwanja wa Olimpiki, ili kuanzisha harakati za wavulana na wasichana wanaotaka kujenga ulimwengu wa amani, ambapo sisi sote ni kaka na dada, ulimwengu ambao una wakati ujao kwa sababu tunataka kuutunza kwa mazingira yanayotuzunguka. Wimbo wenu, “Ulimwengu Mzuri,” unasema yote. Asante kwa hilo!”
Baba Mtakatifu Francisko akiendelea na salamu hizo amesema ndani yao, watoto, kila kitu kinazungumza juu ya maisha na siku zijazo. Kanisa, kama mama, linawakaribisha na kuwasindikiza kwa huruma na matumaini. Mnamo Novemba 7 iliyopita, Papa Francisko amesema alivyopata shangwe ya kuwakaribisha maelfu ya watoto kutoka sehemu nyingi za ulimwengu hadi Vatican. Papa amesema kuwa walileta wimbi la furaha pamoja kwa siku hiyo; na walishirikisha naye maswali yao kuhusu siku zijazo. Mkutano huo uliacha hisia ya kudumu moyoni mwa Papa amesema. Kwa njia hiyo ameongeza kusema: “Nilisali na kutambua kwamba mazungumzo yetu yalipaswa kuendelea na kupanuka ili kufikia watoto na vijana wengi zaidi.”
Ndiyo maana wamekuwapo hapo siku hiyo ili kuendeleza mazungumzo, kuuliza maswali na kutafuta majibu pamoja. Papa Francisko aidha amebainisha anavyojua wanavyohuzunishwa na vita vinavyosababisha vifo na mateso mengi. Wana wasiwasi juu ya mabadiliko ya tabianchi na matokeo yake. Wanawahurumia watoto na vijana ambao hawawezi kwenda shule kwa sababu ya vita, mafuriko, ukame, au ukosefu wa chakula au matibabu.
Hizi ni hali halisi ambazo pia Papa anazibeba moyoni mwake, na kuziwasilisha kwa Mungu katika maombi. Kwa njia hiyo Papa Francisko ameomba kusali pamoja! Akiendelea na hotuba hiyo Papa Francisko amebainisha jinsi ambavyo wanajua, kuna jambo moja ambalo linamgusa sana. Baadhi ya watoto wa Ukraine, ambao nchi yao na familia zao zinateseka sana kutokana na vita, walikwenda kumwona. Aliona kwamba walikuwa wamepoteza tabasamu zao. Vita vimeondoa tabasamu kwenye nyuso zao.
Hili halikubaliki! Leo, pamoja na ninyi, ninataka kusema "hapana" kwa "jinamizi linaloondoa tabasamu za watoto. Ninawauliza: jina la mnyama huyu anayewanyima watoto tabasamu zao ni nani? vita! Papa ameongeza kusema: “Semeni kwa sauti kubwa, jina lake ni nani? vita! Itachukua nini kurudisha tabasamu hilo? Amani! Sote tuseme: amani!” Papa amesema. Papa aliongeza kwamba “watoto na vijana, wengine wanaweza kufikiria kuwa ndoto zao zimeibiwa pamoja na tabasamu lao. Lakini niambie, mtaacha ndoto zenu ziibiwe? Je, mtaendelea kuota? Amewapongeza na kuwashukuru kwa hilo “kwa sababu kwa pamoja tunaweza kujenga, siku baada ya siku, ulimwengu mzuri zaidi, wenye amani na wa kuishi kwa kila mtu. Asante! “
Papa kisha amesema: Mnajua kauli mbiu ya Siku hii ya watoto Duniani ni nini? Ilichukuliwa kutoka katika Maandiko, kutoka katika kitabu cha mwisho cha Biblia, cha Ufunuo. Mwishoni kabisa, Bwana, ambaye ameketi juu ya kiti chake cha enzi, anasema maneno haya: “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya” (Ufu 21:5). Hiyo ndiyo kauli mbiu. Sio nzuri? Ameuliza na kwamba: Hebu fikiria: Mungu, anayetawala juu ya ulimwengu wote, alisema kwa dhati, “Tazama, ninafanya vitu vyote kuwa vipya.” Kila kitu kizee, kibaya, hasi, kinachosababisha kifo na mateso, yote yatatoweka. Kutakuwa na “mbingu mpya na dunia mpya” (Ufu 21:1), ambamo upendo, furaha na amani vitatawala.
Hii ni ndoto ya Mungu! Mnaipenda? Ni vizuri. Papa ameongeza swali lenye changamoto: je, mnataka kushirikiana na Mungu katika kutimiza ndoto hii? Ni sawa kwamba mnataka kufikiria vizuri, kwa sababu ni chaguo muhimu. Kwa hiyo, mmeshawishika? Ni vizuri! Papa amefafanua jinsi wanavyoweza kushirikiana na Mungu kufanya upya ulimwengu. Sote tunaweza kufanya hivyo, kwa sababu inahusu kila mmoja wetu na ni sawa kwa kila mtu: lazima tumfuate na kumwiga Yesu, na kupendana kama alivyotupenda sisi. Ni lazima tufanye hivyo: kuishi Injili, tujaribu kuiweka katika vitendo katika maisha yetu ya kila siku.
Papa Francisko aidha alipenda kuwapatia mfano wa kuiga: kijana kama wao anaitwa Carlo Acutis; Kwa hiyo “Nadhani wengi wenu mmesikia habari zake. Carlo ametangazwa mwenyeheri na hivi karibuni nitakuwa na furaha ya kumtangaza kuwa mtakatifu. Alikuwa mtoto katika upendo na Yesu, hasa katika Ekaristi, na kwa upendo wa Mungu moyoni mwake alifanya mema mengi kwa wazazi wake, marafiki zake na maskini ambao alikutana nao.
Ninamkabidhi kwenu kama rafiki mzuri!” Papa akiendelea amesema “Mnajua, wavulana na wasichana wapendwa, kwamba Yesu mwenyewe alisema katika Injili kwamba anawapenda, kwamba anataka muwe karibu naye. Mnakumbuka? Wakati fulani alisema, “‘Waacheni watoto waje kwangu, msiwazuie; kwa maana ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambia, Yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mchanga hataingia humo.”
Na akawakumbatia, akawabariki, akawawekea mikono yake juu yao” (Mk 10:14-16). Jinsi gani ilivyo nzuri! Hata sasa, anataka kufanya vivyo hivyo: Yesu anataka kukutana na ninyi na kuwabariki, na anawaambia kwamba ninyi ndio watu wa karibu zaidi na ufalme wake, kwa ulimwengu mpya ambao ameumba. Papa ametoa ushauri mwingine muhimu: someni kidogo Injili, kifungu kifupi kila siku. Wazazi wenu, makatekista, na walimu watawasaidia kuelewa maana.
Hata hivyo, ninyi ndio mnapaswa kuisoma na kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie kuelewa na kuiweka katika vitendo. Mmekubali? Je, mko tayari kujitolea kusoma Injili kila siku? Ni vizuri ninyi ni jasiri! Mnahitaji ujasiri kufuata Injili lakini ndiyo njia ya furaha! Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru kwa kukubali mwaliko wake kwa kuja hapo na kuwa pamoja! “Bwana anaweza kufanya mambo makuu ikiwa tutaunganishwa sisi kwa sisi na pamoja na Yesu. Kaka na dada wote, familia moja kubwa, kama ulimwengu!