Takwimu zinaonesha kwamba, kuna kiwango cha chini kabisa cha watoto wanaozaliwa nchini Italia na kwamba, huu ndio ukweli. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna kiwango cha chini kabisa cha watoto wanaozaliwa nchini Italia na kwamba, huu ndio ukweli.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Maisha Ni Zawadi Kubwa Kutoka Kwa Mungu Ilindwe!

Kuna haja ya kuwekeza katika familia, kwa kuhakikisha kwamba, vijana wanapata fursa za ajira, ili waweze kuanzisha na kuzitegemeza familia zao kwani bila watoto Italia itapoteza matumaini. Umefika wakati wa kuondokana na vitendo vinavyowatweza wanawake sanjari na kuepukana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji na vizuia mimba. Jamii ijizatiti katika kuwalea na kuwatunza wazee, kwani kuwatelekeza wazee kutaitumbukiza Italia kwenye janga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Kitaifa nchini Italia kuhusu kiwango cha kuzaliana, “Stati Generali della Natalità”  kuanzia tarehe 9 hadi tarehe 10 Mei 2024 umeingia katika awamu yake ya nne, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kuwako huko, vijana zaidi, zaidi kwa siku zijazo.” Hili ni tukio muhimu sana linalopembua masuala ya kiwango cha kuzaliwa na ustawi wa familia. Ni mkutano unaowashirikisha watu kutoka katika ulimwengu wa siasa, uchumi, biashara na jamii katika ujumla wake. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna kiwango cha chini kabisa cha watoto wanaozaliwa nchini Italia na kwamba, huu ndio ukweli. Hii ni tafakari inayolenga kuunganisha mfumo mzima Kitaifa, kupembua na hatimaye, kutoa mapendekezo madhubuti ili kubadili mwelekeo wa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Italia, ili hatimaye, kupanga sera na mikakati kwa siku za usoni. Italia katika miaka ya hivi karibuni imejikuta ikiwa na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa na matokeo yake, idadi ya wazee nchini Italia inazidi kuongezeka maradufu.

Kuwako huko, vijana zaidi, zaidi kwa siku zijazo
Kuwako huko, vijana zaidi, zaidi kwa siku zijazo

Idadi ya watoto waliozaliwa kwa Mwaka 2023 imekuwa ni chini sana ikilinganishwa na miaka mingine. Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 10 Mei 2024 amewaalika watu wa Mungu nchini Italia kuwekeza katika watoto, kwani watoto ni kumbukumbu inayoielekeza jamii kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Misigano inayotokea maeneo ya kazi, majumbani na shuleni kwa upande wa watoto, wanaookoa jahazi ni babu na bibi! Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika familia, kwa kuhakikisha kwamba, vijana wanapata fursa za ajira, ili waweze kuanzisha na kuzitegemeza familia zao kwani bila watoto Italia itapoteza matumaini kwa watu wake. Umefika wakati wa kuondokana na vitendo vinavyowatweza wanawake wenye mimba katika ulimwengu wa wafanyakazi sanjari na kuepukana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji na vizuia mimba. Jamii ijizatiti katika kuwalea na kuwatunza wazee, kwani kuwatelekeza wazee kutaitumbukiza Italia katika janga la kijamii. Kumbe, changamoto ya uzazi nchini Italia inapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia: Uhalisia, kuona mbele na ujasiri.

Watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu walindwe
Watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu walindwe

Baba Mtakatifu Francisko anasema katika historia ya maisha ya mwanadamu kumekuwepo na tafiti kuhusu uchumi, kiasi cha kuonekana kwamba, binadamu ni tatizo, lakini ikumbukwe kwamba maisha ya mwanadamu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, licha ya uchafuzi wa mazingira, magonjwa na njaa, bado kuna watoto wanaozaliwa sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, hapa tatizo ni uchoyo na ubinafsi unaozalisha mifumo tenge ya ukosefu wa haki, kiuchumi na kisiasa na matokeo yake, idadi ya watoto wanaozaliwa ni ndogo na hivyo kuwatumbukiza watu wengi kwenye huzuni, lakini, watu hawa hawa wanapenda kumiliki paka na mbwa. Tatizo na changamoto kubwa ni ubinafsi, uchoyo na ulaji wa kupindukia kunawatosheleza watu, lakini kwa kuwaacha bila ya kuwa na furaha. Bila watoto na vijana, Italia inakosa mwelekeo wa matumaini kwa siku za usoni. Kuna baadhi ya nchi ambazo idadi ya watoto wanaozaliwa ni kati ya miaka 24, lakini nchini Italia ni miaka 47, hali inayoonesha idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa, huku kiwango cha wazee kikiongezeka maradufu, kiasi cha Bara la Ulaya kugeuka kuwa ni Bara la wazee wanaoogelea katika upweke hasi wakiwa na majonzi nyoyoni mwao kiasi cha kushindwa kufurahia maisha kama zawadi ya Mungu sanjari na uzuri wa maisha.

Mkutano wa Kitaifa Italia kuhusu kiwango cha kuzaliana
Mkutano wa Kitaifa Italia kuhusu kiwango cha kuzaliana

Kwa sasa watu wengi wanawekeza katika vifaa vya utoaji mimba sanjari na biashara haramu ya silaha duniani. Kumbe, kwa Italia kuna haja ya kujikita katika uhalisia, kwa kuona mbele pamoja na kuwa na ujasiri ili kupokea zawadi ya uhai, kwa kuwajengea vijana uwezo ili hatimaye waweze kutekeleza ndoto zao za maisha. Hii ni pamoja na kuwekeza katika sera na mikakati bora kwa ajili ya familia na hivyo kuondokana na migogoro kwa wanawake wajawazito kuamua kuchagua kubeba ujauzito na kuwatunza watoto wake au kuendelea na kazi. Kuna idadi kubwa ya vijana ambao hawana tena na matumaini ya kuweza kuanzisha familia na kuwa na makazi bora kwa sababu ya ukata. Umefika wakati kwa Italia kujikita katika utamaduni wa ukarimu na mshikamano. Malezi ya watoto yanadai sadaka na majitoleo, mambo msingi yanayopaswa kuendelezwa kama sehemu ya utamaduni unaojali watoto. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa na ujasiri wa kukabiliana na changamoto ya idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa, vita, magonjwa ya milipuko pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini wawe na ujasiri na kamwe wasijikatie tamaa, wawe ni vyombo vya matumaini kwa fursa mbalimbali za ajira. Italia iendelee kujikita katika ulinzi na tunza ya wazee, ambao ni nguzo muhimu sana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amewahakikishia kwamba anaendelea kuwasindikiza katika maisha na utume wao kwa njia ya sala na sadaka yake.

Uzazi Nchini Italia

 

10 May 2024, 15:03