Papa Francisko:tunahitaji amani wakati huu wa vita vya dunia
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Sio tena vipande, lakini vita vya ulimwengu halisi. Ni maneno ya uchungu yaliyotamkwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kuhitimisha katekesi yake, akiwa anatoa salamu mbali bali kwa maefu ya waamini na mahujaji waliounganika katika Uwanaja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 22 Mei 2024. Papa alisema “Tunaomba amani. Tunahitaji amani. Dunia iko vitani.”
Kufikiria juu ya Ukraine, Mashariki ya Kati, Myanmar
Papa aidha akijitenga na hotuba iliyoandikwa na kuorodhesha nchi zinazoteseka kutokana na migogoro alisema: Ukraine, ambapo mvua ya ndege zisizo na rubani za Urussi zinaendelea; Mashariki ya Kati, ambapo idadi ya vifo kutokana na milipuko ya mabomu inaendelea; Myanmar, pamoja na mgogoro wa ndani na huko janga la Rohingya. “Tusisahau Ukraine inayoteswa ambayo inateseka sana. Tusisahau Palestina, Israel: acha vita hivi vikome. Tusisahau Myanmar na tusisahau nchi nyingi kwenye vita. Kaka na dada, tunahitaji kuombea amani wakati huu wa vita vya ulimwengu.” Alitoa wito Baba Mtakatifu Francisko.
Mwaliko kwa watoto
Amani ambayo kila mtu, kwa mchango wake, anaweza kuijenga. Hata watoto. Katika salamu zake kwa mahujaji wa Poland Papa Francisko, akiwahutubia vijana wote wanaosherehekea Komunyo yao ya Kwanza, alisema mkutano muhimu na Yesu, aliwahimiza katika wakati huu wa furaha kuweza pia kuona mahitaji ya wenzao ambao wanateseka, waathirika wa vita, njaa na umaskini. Maria atufundishe huduma ya unyenyekevu ambayo ni chemchemi ya amani duniani na Kanisani. Alisema papa
Uhaba wa miito nchini Italia
Katikati ya majanga ya dunia, Papa Francisko pia alitoa tafakari fupi kuhusu matatizo katika Kanisa, kama vile mgogoro wa ukosefu wa miito. Katika kuwasalimia Waitaliano, aliwatazama watawa waliokuwepo katika uwanja wa Mtakatifu Petro , na kusema: "Ninawaona hawa wanovisi na ninajiuliza: Waitaliano ni wangapi? Huh? Wachache... Kuna uhaba wa miito katika maisha ya wakfu nchini Italia.