Kuanzia tarehe 16 Mei hadi tarehe 18 Mei 2024 kunafanyika mkutano wa kimataifa kuhusu michezo na maisha ya kiroho. Kuanzia tarehe 16 Mei hadi tarehe 18 Mei 2024 kunafanyika mkutano wa kimataifa kuhusu michezo na maisha ya kiroho. 

Umuhimu wa Michezo Katika Maisha na Utume wa Kanisa

Papa katika ujumbe wake kwa washiriki anakazia: Umuhimu wa michezo katika maisha ya kiroho, umuhimu wa Kanisa kuwekeza katika shughuli za kichungaji katika michezo kwa vijana na kwamba, michezo ni muhimu sana katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anasema, maisha ya mkristo ni sawa na yale ya wanariadha wanaoshindana kwa kupiga mbio, lakini apokeaye tuzo ni mmoja na tuzo hiyo ni Kristo Yesu mwenyewe. Rej. 1Kor 9: 24.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu; ni njia ya mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Baba Mtakatifu anaendelea kusema, kwamba, michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuandika ukurasa mpya wa michezo katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika: ushirikishwaji; ukweli, uwazi na uaminifu pamoja na kuwa na upendeleo kwa maskini. Ni katika muktadha wa umuhimu wa michezo katika maisha na utume wa Kanisa anasema Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu kwamba, michezo inapaswa kuwa ni mahali pa kujenga na kudumisha amani na matumaini kwa watu wa Mungu.

Michezo ni mahali pa kujenga utamaduni wa amani na maridhiano
Michezo ni mahali pa kujenga utamaduni wa amani na maridhiano

Ndiyo maana kuanzia tarehe 16 Mei hadi tarehe 18 Mei 2024 kunafanyika mkutano wa kimataifa kuhusu michezo na maisha ya kiroho kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kuwekeza maisha yako kwenye michezo.” Huu ni mkutano ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ufaransa mjini Vatican. Washiriki wa mkutano huu, pamoja na mambo mengine, wameendelea kupembua umuhimu wa michezo na madhara yake katika maisha ya mwanadamu. Changamoto na mwaliko wa kujenga jamii inayosimikwa katika: udugu wa kibinadamu, maridhiano na usawa. Tangu mwanzo, Kanisa limetoa kipaumbele cha pekee kwa michezo, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Michezo isaidie kuragibisha ujumuishwaji wa vijana katika jamii yanayokolezwa na maisha ya kiroho. Watu wajenge utamaduni wa kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kumbe, hata walemavu wanayo nafasi ya kushiriki katika michezo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu, anakazia umuhimu wa michezo katika maisha ya kiroho, umuhimu wa Kanisa kuwekeza katika shughuli za kichungaji katika michezo kwa vijana na kwamba, michezo ni muhimu sana katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anasema, maisha ya mkristo ni sawa na yale ya wanariadha wanaoshindana kwa kupiga mbio, lakini apokeaye tuzo ni mmoja na tuzo hiyo ni Kristo Yesu mwenyewe. Rej. 1Kor 9: 24.

Michezo ijikite katika ushirikishwaji, ukweli na uwazi
Michezo ijikite katika ushirikishwaji, ukweli na uwazi

Mtume Paulo anasema, “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji la haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.” 2Tim 4: 7-8. Hapa mkazo ni nidhamu pamoja na udumifu mambo muhimu sana katika maisha ya Kikristo, ili kujenga mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, ili kuweza kuwa ni marafiki wa Mungu. Michezo ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu, mwaliko kwa watu wa Mungu kutafuta muda wa kufanya mazoezi, kwani hii pia ni fursa kwa michezo kujenga utamaduni wa kuwakutanisha na kuwaunganisha watu; na hatimaye, kujenga jumuiya, ili kuendeleza na kutekeleza ndoto za watu na hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anasema, michezo inasaidia kumwilisha tunu msingi za maisha na hivyo kutakasa uchoyo na ubinafsi na tabia ya kupenda sana malimwengu. Mama Kanisa anathamini sana mchango wa michezo kama sehemu muhimu ya uinjilishaji na kwamba, wadau wa michezo ndani ya Kanisa watambue kwamba, Kristo Yesu ni mwanamichezo wa Mungu. Matamko ya hivi karibuni kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Kanisa yanaonesha changamoto kubwa iliyoko kwenye tasnia ya michezo ni kuhakikisha kwamba, michezo inaendelea kujikita katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; ni wakati wa kupambana na rushwa na ubadhilifu na hivyo kuifanya michezo kuwa ni mahali maalum pa watu kukutana na hivyo kujenga udugu wa kibinadamu. Michezo ni muhimu sana katika medani mbalimbali ya maisha kwani inasaidia kujenga na kudumisha nidhamu katika maisha ya kijamii, kitamaduni, kisiasa na kiroho. Michezo katika ngazi mbalimbali haina budi kukuzwa na kuendelezwa, ili kuboresha maisha ya kiroho kwa wadau wa michezo. Wadau wa michezo hawana budi kuhakikisha kwamba wanasaidia kurithisha tunu msingi za maisha ya kiutu na kiroho kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa majiundo makini ya watoto na vijana wa kizazi kipya.

Michezo
17 May 2024, 14:15