Tafuta

Wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa ulioandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi na Sayansi Jamii, Alhamisi tarehe 16 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa ulioandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi na Sayansi Jamii, Alhamisi tarehe 16 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.   (Vatican Media)

Waathirika Wakuu wa Mabadiliko ya Tabianchi ni Maskini Duniani

Wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa ulioandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi na Sayansi Jamii, Alhamisi tarehe 16 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu umuhimu wa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini, ili kuweza kutoa majibu muafaka yatakayokuwa ni chimbuko la matumaini kwa vizazi vijavyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika dimbwi la: Ujinga, umaskini na magonjwa ya mlipuko. Ikolojia ya maisha ya kiroho iwahamasishe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na shauku ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa kufungamanisha maisha ya kiroho na utunzaji bora wa mazingira; kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu katika kazi ya uumbaji, kwa kuonesha moyo wa ukarimu na kujali, kwa kutambua kwamba, ulimwengu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuwa, huu ni mwaliko wa kujitoa sadaka kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira haina budi kupewa kipaumbele cha pekee kama ilivyo pia kwa sekta ya afya na vita sehemu mbalimbali za dunia, wito kwa wote ni wongofu wa kiikolojia unaosimikwa katika wongofu wa kijumuiya ili kuleta mabadiliko endelevu na ya kudumu; mambo yanayopaswa pia kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwani waathirika wakuu ni “Akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuendelea kujikita katika mchakato wa kuragibisha elimu ya ikolojia na maendeleo fungamani ya binadamu. Amesema, changamoto na matatizo yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji toba na wongofu wa ndani pamoja na maamuzi thabiti yanayopaswa kufanywa na kutekelezwa kwa ujasiri mkuu. Ni katika muktadha huu, watafiti, viongozi wa kidini, magavana, pamoja na mameya kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanashiriki katika mkutano wa Kimataifa unaonogeshwa na kauli mbiu “Kutoka kwenye Mgogoro wa Hali ya Hewa hadi Kustahimili Hali ya Hewa.” Lengo kuu ni kushirikishana, uelewa na mang’amuzi, ili hatimaye, kuweza kujenga msingi utakaosaidia kutoa ufumbuzi wa changamoto hizi kwa kukazia umuhimu wa kuhakikisha viwango vya joto duniani visalia kuwa chini ya nyuzi joto 1.5 hadi kufikia mwaka 2030.

Waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi ni maskini.
Waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi ni maskini.

Mkutano huu wa Kimataifa umeandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi na Sayansi Jamii na wajumbe wake, Alhamisi tarehe 16 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu umuhimu wa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini, ili kuweza kutoa majibu muafaka yatakayokuwa ni chimbuko la matumaini kwa vizazi vijavyo! Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii kwa sababu hawa ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia! Kwa sasa Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na changamoto za kimfumo ambazo ni tofauti kabisa, lakini zimeunganishwa yaani: Mabadiliko ya hali ya hewa, upotezaji wa bioanuwai, uharibifu wa mazingira nyumba ya wote, tofauti za ulimwengu, ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula na vitisho kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Masuala haya yasiposhughulikiwa kwa haraka yanaweza kuathiri familia ya binadamu, viumbe hai na mfumo mzima wa kiikolojia. Jambo moja linapaswa kufahamika na wengi kwamba, watu maskini duniani wanateseka zaidi, ingawa wanachangia kiasi kidogo katika matatizo haya. Kumbe, athari za mabadiliko ya tabiachi zimejikita katika masuala jamii, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Nchi 46 changa zaidi duniani zinazalisha hewa ya ukaa kwa asilimia 1.1%, ikilinganishwa na nchi za Umoja wa Ulaya zinazozalisha asilimia 80% ya hewa ya ukaa.

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni jambo la dharura
Athari za mabadiliko ya tabianchi ni jambo la dharura

Tafiti zinazonesha kwamba, waathirika wakuu ni wanawake na watoto na matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Kumbe, athari za mabadiliko ya tabianchi ni jambo la dharura linalopaswa kuvaliwa njuga mapema iwezekanavyo. Watu zaidi ya milioni moja kila mwaka wanaathirika na mabadiliko ya tabianchi na zaidi ya watu bilioni tatu wako hatarini hali inayotishia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lakini ikumbukwe kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu, kumbe mazingira nyumba ya wote yanapaswa kulindwa na kuendelezwa. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe ili kupambana kwa haraka na athari za mabadilio ya tabianchi; kupunguza ongezeko la joto duniani kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa. Kiasi kikubwa cha hewa ya ukaa kinapaswa kuondolewa angani, kwa kulinda na kutunza maliasili, Bonde la Amazoni na lile la Congo DRC; kwa ufupi, Jumuiya ya Kimataifa ijikite katika kukuza mifumo ya ikolojia inayoendeleza maisha. Changamoto hii inahitaji ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa; katika mchakato wa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa; elimu makini juu mtindo wa maisha pamoja na kugharimia miradi inayodhibiti ukame. Uundwe mfuko maalum utakaosaidia nchi zilizo athirika vibaya pamoja na kusamehe deni la nje kama deni la kiikolojia. Huu ni mwaliko wa kugeuza athari za mabadiliko ya tabianchi kuwa ni fursa ya kukuza na kudumisha usawa na haki jamii. Ni vyema kutenda kwa haraka na kwa ushupavu, ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mazingira
16 May 2024, 15:04