Papa Francisko:wakristo wawe marafiki,maadui tunao wengi nje!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumatato tarehe 22 Mei 2024, Baba Mtakatifu Francisko amewasalimu ujumbe kutoka Baraza la Kikristo la Hong Kong,Shirika la Kiekumene la Kiprotestanti. Akianza Papa amewashukuru kwamba “Asante! Asanteni sana kwa ziara hii ambayo ni faraja ya kweli: kuona ndugu zetu wote wakiwa na umoja, kaka na dada Wakristo wakiwa na umoja. Askofu mkuu wa Kiorthodox, Zizioulas, ambaye alikufa zaidi au chini ya mwaka mmoja uliopita, alisema kwamba tutakuwa na umoja wa Makanisa ya Kikristo siku ya hukumu ya mwisho. Lakini wakati huo huo - alisema – “lazima tuombe pamoja na kufanya kazi pamoja.” Hili ni muhimu sana: kufanya kazi pamoja, kwa sababu sote tunamwamini Yesu Kristo; kusali pamoja, kuomba kwa ajili ya umoja. Patriaki mwingine mkuu wa kiorthodox wa Konstantinople, alipompokea Papa Paulo VI, alisema sentensi nzuri: “Hebu tufanye jambo moja: tuwaweke wataalimungu wote kwenye kisiwa kimoja, kwa sababu wanabishana na sisi twenda mbele kwa amani".
Nzuri sana! Jambo muhimu: tuna Ubatizo sawa na hii inatufanya kuwa Wakristo. Maadui, tuna wengi nje. Sisi ni marafiki! Maadui, nje; hapa, marafiki. Ni kweli ninaposema maadui, kwa sababu ni ukweli ambao Bwana alituambia: Kanisa litateswa daima. Siku zote mauaji ya imani yapo katika historia ya Makanisa yetu, sivyo? Endeleeni. Jambo zuri sana lilitokea wakati Paulo VI alipokwenda Uganda. Alizungumza juu ya wafiadini Wakatoliki na Waanglikani. Wao ni wafia dini. Na mimi mwenyewe, wakati wale watu wa Coptic walipouawa, nilisema mara moja kwamba wao ni wafia dini wet" pia, ni wafia dini wa kila mtu.
Kuna ubatizo mara mbili: mmoja, ambao sisi sote tunao - Ubatizo ambao tumepokea na mwingine, ambao Bwana anauita “Ubatizo wa damu:” kifodini. Na sote tunajua ni nini mauaji ya Wakristo wengi waliotoa maisha yao kwa ajili ya imani”. Kwa kuhitimisha aliwashukuru tena. Na kwamba alitaka wote wasali kwa pamoja sala ya Baba Yetu. Baada ya sala hiyo aliwashukuru sana tena kufika kwao kwa lugha ya kiingereza: “Thank you very much for your visit.”