Papa,Sala ya Malkia wa Mbingu:Neno la Mungu linyamazishe gumzo na kutoa nafasi ya Roho
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko akianza tafakari lake akiwa katika Dirisha la Jumbala Kitume mjini Vatican kwa waamini na mahujaji waliounganika katika Uwanja wa Mtakatifu, mara baada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, katika fursa ya Siku Kuu ya Pentekoste, Dominika tarehe 19 Mei 2024 alisema kuwa "Leo, Sherehe ya Pentekoste, tunaadhimisha kushuka kwa Roho Mtakatifu juu ya Maria na Mitume. Katika Injili ya liturujia, Yesu anazungumza juu ya Roho Mtakatifu na anasema kwamba anatufundisha "kila kitu alichosikia" (reje Yh 16:13). Lakini usemi huu unamaanisha nini? Roho Mtakatifu alisikia nini? Anatuambia kuhusu nini?"
Baba Mtakatifu akiendelea amesema kuwa: “Anazungumza nasi kwa maneno yanayoonesha hisia za ajabu, kama vile upendo, shukrani, uaminifu, na huruma. Maneno ambayo yanatufanya tufahamu uhusiano mzuri, unaong'aa, thabiti na wa kudumu kama vile upendo wa milele wa Mungu, maneno ambayo Baba na Mwana huzungumza wao kwa wao. Kwa hakika ni maneno ya upendo yanayogeuza, ambayo Roho Mtakatifu anarudia ndani yetu, na ambayo ni vizuri kwetu kusikiliza, kwa sababu maneno haya huzaa na kufanya hisia sawa na nia kukua katika mioyo yetu: ni maneno yenye kuzaa matunda.
Hii ndiyo sababu ni muhimu kwamba tujimwilishe kila siku kwa Maneno ya Mungu, Maneno ya Yesu, yaliyoongozwa na Roho. Na mara nyingi ninasema: soma kipande cha Injili, uwe na Injili ndogo, ya mfukoni na uende nayo, ukitumia wakati mzuri.” Papa Francisko amerudia kutoa ushauri. Papa amesema tena kuwa Padre na mshairi Clemente Rebora, akizungumzia kuongoka kwake, aliandika katika shajara yake kuwa: “Na Neno lilinyamazisha mazungumzo yangu!” (Wasifu wake).
Neno la Mungu hunyamazisha mazungumzo yetu ya kijuu juu na kutufanya tuseme maneno mazito, maneno mazuri, maneno ya furaha. Na Neno linanyamzishaa gumzo langu! Kusikiliza Neno la Mungu hunyamazisha gumzo. Hii ni jinsi ya kutoa nafasi ndani yetu kwa sauti ya Roho Mtakatifu. Na kisha katika Kuabudu Papa amesisitiza kuwa “ tusisahau sala ya kuabudu katika ukimya - hasa ile rahisi, ya kimya, kama jinsi ilivyo kuabudu . Na hapo tunasemezana maneno mazuri, tuyaseme moyoni ili tuweze kuyasema kwa wengine, baadaye,sisi kwa sisi, na kwa hiyo tunaona kwamba yanatoka katika sauti ya Mfariji, na wa Roho.
Papa Francisko amesema kuwa, kusoma na kutafakari Injili, kusali kwa ukimya, kusema maneno mazuri na siyo mambo magumu, hapana na kwa hivyo tunaweza kufanya wote. Ni rahisi zaidi kuliko matusi, kukasirika ... Na kisha tujiulize: maneno haya yana nafasi gani katika maisha yangu? Ninawezaje kuyakuza, kumsikiliza vyema Roho Mtakatifu, na kuwa mwangwi kwa wengine? Maria, aliyekuwapo katika siku ya Pentekoste pamoja na Mitume, atufanye tuwe wanyenyekevu kwa sauti ya Roho Mtakatifu.” Papa amehitimisha.