2024.05.21 Papa Francisko ametuma ujumbe kwa Mkutano kuhusu Baraza la Kwanza la China. 2024.05.21 Papa Francisko ametuma ujumbe kwa Mkutano kuhusu Baraza la Kwanza la China. 

Papa kwa Mkutano wa"miaka 100 ya Concilium Sinense kati ya historia na sasa"

Papa Francisko ametuma ujumbe kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano wa kuadhimisha miaka 100 ya Concilium Sinense huko Shanghai.Katika ujumbe huo Papa amehimiza Wakatoliki wa China kushuhudia imani yao kwa njia ya matendo ya huruma na mapendo,huku akihimiza utangamano wa kuishi pamoja kijamii.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Ilikuwa tarehe 15 Mei 1924 ambapo  lilifanyika Baraza la Kwanza la Kanisa Katoliki nchini China katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Ignatius wa Loyola. Hao waliounganika walikuwa ni Maaskofu, wakuu wa watawa ,mapadre, wengi wao wakiwa wamezaliwa katika nchi za mbali na walifika China kama wamisionari. Kwa njia hiyo miaka 100 baadaye, uzoefu wa sinodi ya Concilium Sinense imezidi kudhihirika kama kifungu muhimu katika safari isiyo na kifani ya Kanisa Katoliki katika China ya leo hii. Na leo inaendelea kutoa mawazo yenye matunda kwa yeyote anayependa mambo ya sasa na yajayo ya kazi ya utume duniani.

Ni katika muktadha huo ambapo Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wake kwa njia ya video. Akianza ujumbe huo Papa amesema: “Nina furaha kuweza kukuhutubia katika hafla ya mkutano wa maadhimisho ya miaka 100 ya Concilium Sinense, Baraza la kwanza na hadi sasa la kipekee la Kanisa Katoliki la China, lililofanyika  huko Shanghai kati ya Mei na Juni 1924, miaka mia moja iliyopita. Mada ya Mkutano huo ni “Miaka mia moja tangu Concilium Sinense, kati ya historia na sasa,”na maadhimisho haya hakika yanawakilisha fursa ya thamani kwa sababu nyingi. Mtaguso huo ulikuwa kweli hatua muhimu katika njia ya Kanisa Katoliki katika nchi kubwa ambayo ni China. Huko Shanghai, Mababa waliokusanyika katika Concilium Sinense waliishi uzoefu halisi wa sinodi na kuchukua maamuzi muhimu pamoja. Roho Mtakatifu aliwaleta pamoja, akafanya maelewano kukua kati yao, akawaongoza kwenye njia ambazo wengi wao hawakuwazia, hata kushinda mashaka na upinzani wao. Hivi ndivyo Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa hufanya.

Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kueleza kuwa:“Karibu wote walikuwa kutoka nchi za mbali, na mbele ya Baraza wengi wao walikuwa bado hawajawa tayari kufikiria fursa ya kukabidhi uongozi wa majimbo kwa mapadre na maaskofu wazaliwa wa China. Kisha, wakiwa wamekusanyika katika Baraza, walifuata safari ya kweli ya sinodi na wote walitia sahihi masharti ambayo yalifungua njia mpya ili Kanisa, hata Uchina wa Kikatoliki, uzidi kuwa na sura ya Kichina. Walitambua kwamba hiyo ndiyo ilikuwa hatua ya kuchukua, kwa sababu ujumbe wa Kristo wa wokovu unaweza kufikia kila jamii ya wanadamu na kila mtu ikiwa tu anazungumza katika lugha yake ya asili.

Papa Francisko aidha ameendelea kukazia kuwa “Mababa wa Mtaguso walifuata nyayo za wamisionari wakuu, kama vile Padre Matteo Ricci – Lì Mǎdòu; walifuata njia iliyofunguliwa na mtume Paulo, alipohubiri kwamba ni lazima kufanya kila kitu kwa kila mtu ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo mfufuka. Pili Mchango muhimu, katika kukuza na kuongozwa na Concilium Sinense, ulitoka kwa Askofu mkuu Celso Costantini, Msimamizi wa Kitume wa kwanza nchini China, ambaye kwa uamuzi wa Papa Pius XI alikuwa pia mratibu mkuu na Rais wa Baraza. Costantini alitazama hali halisi ya kimisionari. Na alithamini sana mafundisho ya Maximum illud, Barua ya Kitume juu ya Utume  iliyochapishwa mnamo 1919 na Papa Benedikto XV.

Kwa kufuatia msukumo wa kinabii wa waraka huo, Costantini alirudia tu kwamba dhamira ya Kanisa ilikuwa “kuinjilisha, si ukoloni.” Katika Mtaguso wa Shanghai, pia kutokana na kazi ya Celso Costantini, ushirika kati ya Vatican na Kanisa la China ulidhihirika katika matunda yake yenye matunda, mema kwa watu wote wa China. Tatu “Lakini Baraza la Shanghai halikusaidia tu kusahau mbinu potofu zilizokuwapo nyakati zilizopita. Halikuwa suala la “kubadilisha mkakati,” lakini la kufuata njia zinazoendana zaidi na asili ya Kanisa na utume wake. Kwa kujiamini katika neema ya Kristo mwenyewe na katika kuvutia kwake.

Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amesema kuwa “Washiriki wa Concilium Sinense ya kwanza walitazamia siku zijazo. Na mustakabali wao ni wetu sasa. Safari ya Kanisa katika historia yote imepita na kupita katika njia zisizotarajiwa, hata nyakati za subira na majaribio. Bwana, katika Uchina, alilinda imani ya watu wa Mungu njiani. Na imani ya watu wa Mungu imekuwa dira ambayo imeonyesha njia wakati wote huu, kabla na baada ya Baraza la Shanghai, hadi leo. Wakatoliki wa China, kwa ushirika na Askofu wa Roma, wanatembea wakati wa sasa. Katika mazingira wanamoishi, wao pia wanaishuhudia imani yao kwa matendo ya huruma na mapendo, na katika ushuhuda wao wanatoa mchango wa kweli kwa maelewano ya kuishi pamoja kijamii, katika ujenzi wa nyumba ya pamoja. Wale wanaomfuata Yesu wanapenda amani, na wanajikuta wakiwa pamoja na wale wote wanaofanya kazi kwa ajili ya amani, katika wakati ambao tunaona nguvu zisizo za kibinadamu zikifanya kazi ambazo zinaonekana kutaka kuharakisha mwisho wa dunia.

Nne: “Washiriki katika Baraza la Shanghai walitazamia siku zijazo. Na, siku chache baada ya kumalizika kwa Baraza, walikwenda kuhiji kwenye Madhabahu ya Mama Yetu wa Sheshan, karibu na Shanghai. Kwa njia hiyo “Sisi pia, kama Mababa wa Baraza la Shanghai, tunaweza kutazama siku zijazo. Na kwa kuukumbuka Mtaguso wa Shanghai pia leo hii tunaweza kupendekeza kwa Kanisa zima njia mpya na njia zilizo wazi zinazopaswa kufanywa kwa ujasiri wa kutangaza na kutoa ushuhuda wa Injili kwa sasa.” Kwa hakika katika siku hizi, katika mwezi wa Mei, uliowekwa wakfu na watu wa Mungu kwa Bikira Maria, Papa amebainisha kuwa kaka na dada zetu wengi wa China wanakwenda kuhiji kwenye Madhabahu ya Sheshan, ili kukabidhi sala na matumaini yao kwa maombezi ya Mama wa Yesu.

Papa katika hilo amesema kuwa: “Siku chache, tarehe 24 Mei, sikukuu ya Maria Msaada wa Wakristo, Kanisa lote ulimwenguni litasali pamoja na ndugu wa Kanisa nchini China kama alivyoomba Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake kwa Wakatoliki wa China. “Hata Mimi pia ninapanda  kwenye kilima cha Sheshan kwa mawazo. Na sote kwa pamoja tumkabidhi Mama Yetu, Msaada wa Wakristo, kaka na dada zetu katika imani walioko China, Wachina wote na ulimwengu wetu wote maskini, tukimwomba maombezi, ili amani ipate kushinda kila mahali. Bikira Maria, Msaada wa Wakristo, Mama Yetu wa Sheshani, utuombee!” Amehitimisha.

Ujumbe wa Papa kwa Mkutano wa Concilium Sinense
21 May 2024, 15:53