2024.05.25Papa amekutana na Wakurgeniz wa Kitaifa wa mashirika ya Kipapa ya Kimisionari. 2024.05.25Papa amekutana na Wakurgeniz wa Kitaifa wa mashirika ya Kipapa ya Kimisionari.  (Vatican Media)

Papa kwa PMS:wito wa umoja unamaanisha mtindo wa kisinodi:kutembea,kusikiliza na mazungumzo

Katika Mkutano na Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Kazi za Kimisionari za Kipapa,Papa alisisitiza kwamba kwa kubaki katika ushirika na Yesu mtu anapata uzoefu wa ubunifu usioisha ambao unazalisha njia mpya za kueneza Injili na kuwahudumia ndugu zetu, hasa maskini zaidi. Amewaomba wawe na mawazo na msimamo kwa ajili ya Injili.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi 25 Mei 2024 akikutana na washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari baada ya kuwasalimu Kardinali  Antonio Tagle, Askofu Mkuu Nwachukwu, Askofu Mkuu Nappa na makatibu wakuu wanne wa Mashirika hayo ya Kimisionari amekaribisha kwa moyo na hasa waliosafiri kutoka mbali  zaidi ya nchi mia moja na ishirini katika Mabara matano kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya  Kipapa Kimissionari. Katika mkesha wa Sherehe ya Utatu Mtakatifu zaidi, Papa amesema tunaalikwa kutafakari fumbo la Mungu: fumbo la upendo linalojitoa, kikamilifu kwa ajili ya wokovu wa wote. Tukitafakari juu ya kazi hii ya wokovu, tunagundua sifa tatu za kimsingi za utume wa kimungu ambazo zimekuwepo tangu mwanzo: ushirika, ubunifu na msimamo.  Papa ameomba kuzingatia maneno haya muhimu, ambayo ni muhimu kwa Kanisa katika hali yake ya kudumu ya utume, hasa kwa Jumuiya zetu za Kimisionari zilizoitwa kupyaishwa ili kuwa na ufanisi zaidi katika huduma. Kwanza, ushirika.  

Baba Mtakatifu Francisko amebainisha kuwa “ Tunapotafakari Utatu, tunaona kwamba Mungu ni ushirika wa watu, fumbo la upendo.   Upendo ambao Mungu huja nao kututafuta na kutuokoa, uliokita mizizi katika kuwa kwake Mmoja na Utatu, pia ni msingi wa asili ya kimisionari ya Kanisa la Hija duniani (taz. Redemptoris Missio, 1; Ad Gentes, 2).   Katika mtazamo huo tumeitwa kuishi hali ya kiroho ya ushirika na Mungu na pamoja na kaka na dada zetu.  Utume wa Kikristo hauhusu kusambaza ukweli fulani usio wazi au imani ya kidini, lakini, kwanza kabisa, ni kuwawezesha wale tunaokutana nao kuwa na uzoefu wa kimsingi wa upendo wa Mungu.   Kwa hakika, ikiwa sisi ni mashahidi wenye kuangaza wanaoakisi mwale wa fumbo la Utatu, wataweza kugundua upendo wa Mungu katika maisha yetu na katika maisha ya Kanisa. Kwa hiyo, Baba Mtakatifu amewasihi kila mtu akue katika hali hii ya kiroho ya ushirika wa kimisionari, ambayo ndiyo msingi wa safari ya sasa ya sinodi ya Kanisa.    Amekumbusha jinsi ambayo alisisitiza katika Waraka wa Kitume Praedicate Evangelium na alisisititza tena sasa hasa wanapofanyia kazi ya kupyaisha sheria zao.

 Kwa kuwa safari ya uongofu wa kimisionari ni muhimu kwa kila mtu, ni muhimu kwamba fursa za malezi ya kibinafsi na ya jumuiya itolewe ili kukua katika hali ya kiroho ya “kijumuiya” ya kimisionari.   Madhumuni utume wa  Kanisa ni “kufanya kila mtu kujua na kuishi ushirika ‘mpya’ ambao Mwana wa Mungu alipofanywa mwanadamu ameuingiza katika historia ya ulimwengu” ( Praedicate Evangelium, I, 4). Kwa njia hiyo amesema kuwa wasisahau kwamba wito wa umoja unamaanisha mtindo wa kisinodi: kutembea pamoja, kusikilizana, kushiriki katika mazungumzo.   Hii inapanua mioyo yetu, na kukuza mtazamo wa ulimwengu unaozidi kuongezeka ambao ulisisitizwa wakati wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Uenezaji wa Imani:  "Hatupaswi kufikiria tu hii au utume huo hasa, lakini juu ya utume  na mipango yote ya kimisionari  ulimwenguni kote" (taz. MONS. CHRISTIANI NA J. SERVEL, Marie-Pauline Jaricot, 39).

Neno la pili ambalo Papa Francisko alipendekeza ni ubunifu.   Tukiwa na mizizi katika ushirika wa Utatu, tunahusika katika kazi ya uumbaji ya Mungu, anayefanya mambo yote kuwa mapya (rej. Ufu 21:5).   Pia tunashiriki katika ubunifu huo.   Papa kwa hiyo alipenda kusema mambo mawili kuhusu hili. La kwanza ni kwamba ubunifu unahusishwa na uhuru wa Mungu mwenyewe, ambao anatupatia katika Kristo na katika Roho.   Hakika, “alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru” (2 Wakor 3:17).   Hatupaswi kujiruhusu kukandamiza uhuru wa ubunifu wa kimisionari!   Pili, kama Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe, mmisionari wa Kifransiskani  huko Japan na mfiadini wa upendo, alivyosema kuwa : “upendo pekee ndio hutengeneza.” Tukumbuke kwamba ubunifu wa kiinjili unatokana na upendo wa kimungu, na kwamba shughuli zote za kimisionari ni za ubunifu kwa kadiri kwamba upendo wa Kristo ni chimbuko lake, umbo na mwisho wake.   Kwa hivyo, kwa mawazo yasiyoisha, upendo kama huo huhamasisha njia mpya za kuinjilisha na kuwahudumia wengine, hasa walio maskini zaidi, na hujumuisha makusanyo yaliyochukuliwa kwa ajili ya fedha za ulimwengu za mshikamano na utume.  Kwa maana hii, ni lazima tukuze makusanyo haya na kuchunguza njia mpya za kuhimiza ushiriki wa watu binafsi, vikundi na taasisi zinazotaka kuunga mkono juhudi za umisionari za Kanisa kama onesho la shukrani zao kwa neema walizopokea kutoka kwa Bwana.

Neno la tatu na la mwisho ni msimamo, yaani uthabiti na ustahimilivu katika kusudi na vitendo.   Tutafakari pia sifa hii ya upendo wa Mungu wa Utatu ambaye, ili kutimiza mpango wake wa wokovu, kwa uaminifu daima ametuma watumishi wake katika historia yote na, katika utimilifu wa wakati, alijitoa mwenyewe katika Kristo Yesu.   Utume wa kimungu “ni kwenda bila kuchoka kwa wanaume na wanawake wote, ili kuwaalika kukutana na Mungu na kuingia katika ushirika naye.   Bila kuchoka!   Kanisa kwa upande wake, kwa uaminifu kwa utume waliopokea kutoka kwa Bwana, litaendelea kwenda hadi miisho ya dunia, na kuanza safari tena na tena, bila kuchoka wala kukata tamaa mbele ya magumu na vikwazo” (Ujumbe kwa Siku ya Kimisionari Duniani 2024). Basi, tumeitwa kustahimili na kuwa wastahimilivu katika kusudi na matendo.   Wale kati yenu katika Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa wanakumbana na hali na matukio mbalimbali ambayo ni sehemu ya mpito na mtiririko mkuu wa maisha ya Kanisa kote ulimwenguni.

Hivyo, ingawa wanaweza kukutana na changamoto nyingi, hali ngumu, mizigo na uchovu unaoambatana na maisha ya kikanisa, wasivunjike moyo! Wawe makini, mioyo na, Papa aliomba aruhusiwe kusema mdomsmo ili kwamba, hata katikati ya shida nyingi, waweze kutambua kazi ya Mungu, karama za faraja na uponyaji anazowapati, na wakati mwingine mbegu zisizoonekana lakini zenye matunda ya utakatifu.  Kwa kukazia fikira mambo mazuri na shangwe inayotokana na kutafakari kazi ya Mungu, watajua jinsi ya kukabiliana na hali zenye matatizo kwa subira, kuepuka kutotenda na roho ya kushindwa.   Kwa ustahimilivu na saburi, waendelee mbele  katika Bwana! Papa Francisko amewashukuru tena pamoja na wafanyakazi wenzao kwa moyo wa ukarimu na moyo wa kujitolea katika kukuza dhamana ya utume wa waamini hasa katika kuwalea watoto wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu.   Mama Yetu awaombee.   Amewapatia baraka zangu za dhati.   Tafadhali wasisahau kumuombea.

Hotuba ya Papa kwa PMS
25 May 2024, 15:40