Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Tamko la Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na mbaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Katika Tamko hili, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Matumaini katika Neno la Mungu ili kuamini, kutumaini, kupenda na kuvumilia kwa kutambua kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini. Alama za matumaini zinazomwilishwa katika amani, kwa kujikita katika Injili ya uhai, maboresho ya magereza; huduma kwa wagonjwa, vijana, wahamiaji na wakimbizi, wazee na maskini. Wito wa matumaini kwa kujikita katika matumizi bora ya rasilimali za dunia; msamaha wa madeni ya nje kwa nchi zinazoendelea duniani. Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325. Nanga ya matumaini katika maisha ya uzima wa milele yanayopata chimbuko lake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu; Ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; hukumu ya Mungu na mwaliko kwa waamini kujitakasa; Rehema na Sakramenti ya Upatanisho; Wamisionari wa huruma ya Mungu. Bikira Maria ni shuhuda wa hali ya juu kabisa wa matumaini, Nyota ya Bahari na kwamba, hija ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo iwasaidie waamini kujikita katika Maandiko Matakatifu.
Huu ni muhtasari wa Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 uliosomwa wakati wa maadhimisho ya Masifu ya Jioni, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Alhamisi tarehe 9 Mei 2024. Kupaa Bwana Mbinguni ni sehemu ya furaha ya watu wa Mungu, kielelezo cha Ibada ya shukrani, kwani Kupaa kwa Kristo Yesu mbinguni ni kuinuliwa kwa waja wake na kwamba, amewatangulia yeye aliye kichwa chao kwa utukufu na huko huko ndiko wanakutumaini kuwepo wao ambao ni sehemu ya Fumbo la mwili wake, yaani Kanisa, ili waweze kutawala pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu milele yote! Rej. Kolekta Sherehe ya Kupaa Bwana. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kuhusu matumaini yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, Mwaka wa Sala kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo; Umuhimu wa fadhila ya matumaini katika maisha ya waamini na katika Kanisa. Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kisha akapaa mbinguni, awakirimie waamini neema na baraka za kuweza kugundua fadhila ya matumaini, ili kutangaza na kushuhudia matumaini, tayari kujenga matumaini. Ushindi wa Kristo Yesu unadhihirika kwani yupo mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, Malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake. Rej. 1Pet 3:22. Huu ndio msingi wa imani ya Kanisa unaofumbatwa katika mateso, kifo, ufufuko na hatimaye kupaa zake mbinguni, changamoto na mwaliko wa: kuadhimisha, kupokea, kutangaza na kulishuhudia Fumbo hili wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hii ni amana na urithi mkubwa wa imani inayowasaidia waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani, ingawa wakati mwingine ni “ngumu kumeza” lakini hakuna sababu msingi ya kukata wala kujikatia tamaa na hivyo kugeuka kuwa ni mfungwa wa mambo yaliyopita. Matumaini ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake wakati wa kupokea Sakramenti ya Ubatizo.
Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwaka 2024 uwe ni mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu katika ujumla wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, yatazinduliwa rasmi kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024. Mwaka wa Sala Kuelelea Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 unapania pamoja na mambo mengine anasema Baba Mtakatifu Francisko: Kupyaisha matumaini baada ya watu wengi kukata na kujikatia tamaa ya maisha kutokana na hali ngumu ya maisha, vita na mipasuko ya kijamii bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Huu ni mkakati wa shughuli za kichungaji unaopania kuwarejeshea tena watu wa Mungu matumaini. Ni mwaliko kwa kila jimbo, baada ya kusoma alama za nyakati kwa watu wake, liandae katekesi kuanzia wakati huu, hadi wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025 hapo tarehe 24 Desemba 2024. Katekesi hii ilenge kuwasaidia waamini kujiandaa kikamilifu kuingia katika lango la Jubilei, ambalo ni Kristo Yesu, Mwanakondoo Mungu. Huu ni wakati wa kupyaisha matumaini ya watu wa Mungu katika furaha na ujasiri tayari kuambata na kukumbatia Injili ya uhai. Tumaini halitahayarishi anasema Baba Mtakatifu, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini, dhidi ya uchoyo na ubinafsi; woga na ukosefu wa haki; mipasuko ya kijamii na vita inayopandikiza mbegu ya kifo. Vijana wanahitaji sana fadhila ya matumaini, kama ilivyo kwa wazee, ili kuondokana na utamaduni usiojali wala kuguswa na mangaiko ya watu wengine; wagonjwa wanahitaji matumaini, bila kuwasahau wale wanaoteseka kiroho na kimwili, ili waweze kuonja ujirani mwema pamoja na tunza.
Kanisa linahitaji kuwa na matumaini kwani linatambua kwamba ni Mchumba wa Kristo Yesu anayependwa kwa upendo na uaminifu wa dhati, ili liweze kulinda na kutunza mwanga wa Injili, ili hatimaye, kuwasha moto wa upendo ulioletwa na Kristo Yesu. Watu wa Mungu wanahitaji fadhila ya matumaini, ili kuzima kiu ya ukweli, upendo na uzuri, ili mwanga wa maisha uendelee kuwaka. Watu wanataka kuonja matumaini yatakayowawezesha kuonja ukaribu wa Mungu katika maisha yao. Inasikitisha kuona kwamba, walimwengu wanaendelea kuwa mbali na Mwenyezi Mungu na hivyo kuujaza utupu huu kwa mambo ya kidunia, yanayofifisha uwepo wa Neno la Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko karibu na waja wake, jambo la msingi kwa waamini ni kuendelea kuwa karibu na Mungu. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kisha akapaa mbinguni, awakirimie waamini neema na baraka za kuweza kugundua fadhila ya matumaini, ili waweze kuitangaza na kushuhudia fadhila ya matumaini, tayari kujenga matumaini.