Sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, tarehe 20 Mei 2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ibada kwa Bikira Maria, inalenga kuwasaidia waamini kukumbuka kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika Fumbo la Msalaba linaloadhimishwa katika Ekaristi Takatifu, Kanisa linapomtolea pia sifa na heshima Bikira Maria, Mama wa Mkombozi, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko lao kuhusu Fumbo la Kanisa wanafafanua kwa kina na mapana nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu katika Fumbo la Kristo na la Kanisa: tangu Agano la Kale, Fumbo la Umwilisho, Bikira Maria katika maisha ya hadharani ya Kristo Yesu na Bikira Maria baada ya Kristo Yesu kupaa mbinguni. Wanaendelea kufafanua dhamana na nafasi ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa kama mshiriki mwaminifu wa kazi ya ukombozi, mwombezi kwa ajili ya wokovu. Bikira Maria ni mfano wa utimilifu wa Kanisa katika maisha na utakatifu wake na kwamba, Bikira Maria ni ishara na matumaini thabiti na faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri huku bondeni kwenye machozi! Kwa hakika, Mapokeo ya maadhimisho ya Fumbo la maisha ya Kristo ambayo kamwe hayawezi kumtenga Bikira Maria, Mama wa Kristo na Kanisa. Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Wakristo ambao wamezaliwa kwake kwa njia ya fadhila ya upendo na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kama wanavyofundisha Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa pamoja na Mtakatifu Leo Mkuu. Umama wa Kristo na Kanisa ulidhihirishwa pale chini ya Msalaba, Bikira Maria alipopokea upendo wa dhati kutoka kwa Mwanaye mpendwa na Yohane kwa niaba ya wengine wote, wakawa ni wafuasi na mitume wa upendo kwa ajili ya Mama yake. Rej. Yn 19:25.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Awe ni faraja na matumaini kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanahimizwa kufanya hija ya maisha ya kiroho pamoja na Bikira Maria, aliyethubutu kumfuasa Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba, ili kuambata na kukumbatia huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Maria ni Bikira na Mama kwa sababu yeye ni ishara na utimilifu kamili wa Kanisa. Kanisa kwa kupokea Neno la Mungu kiaminifu linakuwa pia ni Mama, kwani kwa mahubiri na ubatizo linazaa watoto waliotungwa na Roho Mtakatifu na kuzaliwa na Mungu kwa uzima mpya usiokufa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 11 Februari 2018 alitangaza rasmi maadhimisho ya Sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, ambayo inaadhimishwa, Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste na kwa mwaka huu ni tarehe 20 Mei 2024. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anapenda kuwaweka waamini na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, ili Roho Mtakatifu aendelee kulijaza Kanisa, Ulimwengu na nyoyo za waamini moto wake wa upendo. Bikira Maria Mama wa Yesu ni wito ulio hai wa Roho Mtakatifu. Yeye ni Mama wa Kanisa. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anapenda kumkabidhi kwake, Jumuiya ambazo kwa wakati huu zinahitaji zaidi nguvu ya Roho Mtakatifu: Mtetezi na Mfariji; Roho wa kweli, uhuru na amani.
Bikira Maria aliendelea kuandamana na Kanisa katika sala wakati Mitume wakisubiria ujio wa Roho Mtakatifu. Kwa nyakati mbalimbali, waamini wamekuwa wakimheshimu na kumfanyia Ibada Bikira Maria kama: Mama wa Mitume, Mama wa waamini wa wale wote wanaozaliwa upya katika Kristo Yesu na Mama wa Kanisa kama wanavyofundisha Papa Benedikto XV pamoja na Papa Leo wa XIII. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 21 Novemba 1964, Wakati Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipokuwa wanahitimisha Kikao cha tatu cha Mkutano huo, alitamka kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa; yaani: ni Mama wa Wakristo wote na wachungaji wanaomkimbilia kama Mama. Kumbe, Bikira Maria, Mama wa Kanisa anapaswa kuheshimiwa na Wakristo wote. Katika maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho1975, kuliadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Litania ya Bikira Maria wa Loreto ikaongeza heshima hii katika Litania. Majimbo mbalimbali wakaona kwamba, inafaa na kuomba Kiti Kitakatifu kuruhusu maadhimisho haya yaingizwe katika kalenda ya majimbo yao! Kutokana na kukua na hatimaye, kukomaa kwa Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia tamko lililotolewa na Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kwamba, kuanzia sasa Sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa itakuwa inaadhimishwa Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste ya kila mwaka!