Tamko la Watoto Wadogo Kuhusu Udugu wa Kibinadamu: Amani na Furaha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mkutano wa Ulimwengu wa Udugu wa Kibinadamu, kuhusu Udugu wa kibinadamu umenogeshwa na kauli mbiu “Be Human” kuanzia tarehe 10 hadi 11 Mei 2024 umeandaliwa na Mfuko wa Udugu wa Kibinadamu unaosimamiwa na Kardinali Mauro Gambetti, Makamu Askofu, mji wa Vatican. Mfuko huu unapania pamoja na mambo mengine: Kumwilisha mawazo msingi yaliyobainishwa kwenye Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko wa: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ili kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; sanaa; majiundo pamoja na kukoleza majadiliano na walimwengu. Mkutano huu wa Kimataifa unawashirikisha watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wakiwa ni: Washindi wa Tuzo ya Nobel, wanasayansi, wasanii, maprofesa, mameya, madaktari, mameneja, wafanyakazi pamoja na mabingwa wa michezo, wamekusanyika kwa pamoja ili kujadiliana jinsi ya kukuza na kudumisha thamani ya udugu wa kibinadamu miongoni mwa watu wa Mataifa, wakati ambapo vita, hofu na misigano ya kijamii inaendelea kuwaka moto sehemu mbalimbali za dunia. Wajumbe wa Mkutano wa Ulimwengu wa Udugu wa Kibinadamu, kuhusu Udugu wa kibinadamu, Jumamosi tarehe 11 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu: huruma, utu, heshima, na haki msingi za binadamu kama Katiba ya Binadamu; huu ni mwaliko kwa wajumbe kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu na amani duniani. Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe kwa kuendelea kujizatiti kusimamia haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu, kwa kuishi pamoja kama ndugu wamoja. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa huruma kama inavyofafanuliwa kwa Mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema.
Jumamosi jioni, tarehe 11 Mei 2024 Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na watoto, mkutano ulionogeshwa na kauli mbiu “Yajayo.” Watoto wametoa tamko lao kuhusu udugu wa kibinadamu miongoni mwa watoto wadogo na kwamba, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa binadamu ni dhamana ambayo iko mikononi mwa watoto na wazee, kwani wazee wanawashirikisha watoto hekima na busara inayowawezesha watoto kukua na kuendelea kama mtoto aliyebebwa mikononi mwa mama yake. Kwa mtoto hapa anajisikia kwamba, yuko: huru, salama na analindwa. Padre Enzo Fortunato, Mratibu wa Siku ya Watoto Duniani itakotimua vumbi kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 26 Mei 2024 ameelezea maandalizi yaliyokwisha kufanyika hadi wakati huu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watoto wadogo, ili hatimaye, kujenga udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu; urafiki, amani na utulivu. Zaidi ya watoto 72, 000, wanatarajiwa kushiriki, huku wakisindikizwa na wazazi pamoja na walezi wao. Hii ni sehemu ya ujenzi wa mtandao utakaosaidia kutoa tiba kwa watoto sehemu mbalimbali za dunia kwa mfumo wa “Telemedicine.” Jambo la msingi ni kwa watu wa Mungu kutojenga mazoea ya vita, daima watafute haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu katika mahojiano na watoto amekazia umuhimu wa kulinda na kutunza furaha katika maisha; furaha inayowaunganisha pamoja kama familia kubwa ya Mungu ili kudumisha haki, amani na maridhiano. Amani ya kweli inajengwa kwa maneno na matendo; kwa kuishi kwa umoja, ushirikiano na mshikamano: na kwa watoto kucheza na kusoma pamoja kwa kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao. Uwepo huu unasimikwa katika maisha ya sala na kwamba, furaha ya kweli inafumbwa katika amani. Kuna watoto ambao wako katika maeneo ya vita na maisha yao yako hatarini sana. Hawa ni watoto wanaopaswa kuonjeshwa huruma, upendo na mshikamano wa dhati. Watoto wamesali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea bibi na babu zao. Watoto wajenge utamaduni wa kupendana.
Tamko la Udugu wa Kibinadamu Miongoni Mwa Watoto Wadogo: Baba Mtakatifu katika utangulizi wa tamko hili anakazia umuhimu wa watoto kukaa kwa pamoja kama marafiki wakiwa nyumbani, shuleni, parokiani, kwenye viwanja vya michezo, ili kucheza, kuimba pamoja na kugundua mambo mapya kwa pamoja. Wakati wakifurahia maisha, bila ya kumwacha mtoto yeyote nyuma. Hivi ndivyo urafiki wa kijamii unavyojengwa, kukua na hatimaye, kukomaa; katika kushirikishana mali za dunia; kwa kusameheana na kuishi katika hali ya utulivu na uvumilivu; ujasiri na ubunifu, bila wasiwasi, woga wala maamuzi mbele! Watoto wanasema, udugu wa kibinadamu unawawezesha kuishi kwa mshikamano ili kukabiliana na dhoruba mbalimbali za maisha, kwa kujikita katika mshikamano unaopaswa kupaliliwa ili kukuza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; upendo na furaha ya kweli tayari kupandikiza mbegu ya matumaini itakayozaa: upendo na ukweli; mambo msingi yanayoweza kuvunjilia mbali kuta za utengano. Ndoto yao kama watoto ni kuwa na ulimwengu ambamo watoto wote wanaweza kujisikia kuwa wako nyumbani; mahali ambapo haki, amani na maridhiano vinatawala; mahali ambapo watoto wanapata fursa ya kukua, kusoma, kucheza na kuwa na furaha. Hapa ni mahali ambapo watoto watajisikia kweli, mahali wanapoweza kuonwa, kupokelewa sanjari na kuendelezwa.
Watoto wanataka kuona ulimwengu ambamo hakuna vita wala misigano ya kijamii, bali mshikamano wa upendo kwa maskini na wanyonge zaidi. Watoto wanataka kuwaona watu wazima wakijenga mahusiano na mafungamano yao katika mwelekeo chanya na wenye utulivu; mahusiano yanayosimikwa katika ukarimu, majadiliano, heshima, ushirikishi, msamaha na mshikamano. Wanataka kuona watu wazima wakijenga na kudumisha urafiki wa kweli pasi na woga wala wasiwasi, huzuni na upweke hasi. Watoto wanawataka watu wazima kuonesha kwamba wao ni ndugu wa wote kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, rafiki wa kweli anayewafunza watoto kujenga urafiki. Watoto wanatoa mwaliko kwa watu wazima kuwasaidia kutekeleza hii ndoto yao ya maisha, kwa kuonesha maboresho ulimwenguni, kwa kuonesha matumaini kwa siku zijazo, kwa kuwasindikiza watoto katika njia ya amani, maelewano, udugu wa kibinadamu; ukuaji, ukarimu na matumaini, ili hatimaye, kuonja furaha ya kweli inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.