Umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa: Vijana, Mafunzo na Taaluma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; “Rerum Novarum.”
Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, katika Waraka wake kuhusu Masuala ya Kijamii Centesimus Annus, alifafanua kwa kina kuhusu asili ya haki msingi za binadamu; umuhimu wa kukuza na kudumisha upendo na mshikamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa “Sollicitudo Rei Socialis” cheche ya uanzishaji wa vyama vya kitume kijamii vilivyokuwa vinapania kulinda na kutetea uhuru, utu na haki msingi za binadamu. Itakumbukwa kwamba, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni muhtasari wa haki zote za binadamu. Dini zisaidie kujenga amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na vita. Kanuni maadili na utu wema ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu zinazopaswa kuheshimiwa ili amani na utulivu viweze kushika kasi, bila kusahau nafasi na dhamana ya uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kufahamu vyema kweli za imani yao ili wasiyumbishwe, bali wasimame kidete kuilinda na kuitetea kwa ajili ya ustawi, mafao ya maendeleo ya wengi.
Shirikisho la Kitaifa la Mafunzo ya Kitaalam “CONFAP - Confederazione Nazionale Formazione Aggiornamento Professionale” lilianishwa tarehe 19 Novemba 1974, kumbe, kwa mwaka 2024, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Hili ni Shirikisho linalotoa huduma yake mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Na Chama cha Kitaifa Mafunzo ya Kitaalamu: “Associazione Forma FP” kilianzishwa kunako mwaka 1999 na hivyo kwa mwaka 2024 kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya huduma ya kitaalam kwa vijana wa kizazi kipya nchini Italia na chanzo cha ajira. Hiki ni Chama ambacho kimezalisha wataalam wanaojisadaka kwa ajili ya kutoa elimu na mafunzo kwa vijana. Wajumbe wa Shirikisho la Kitaifa la Mafunzo ya Kitaalam “CONFAP - Confederazione Nazionale Formazione Aggiornamento Professionale” pamoja na Chama cha Kitaifa Mafunzo ya Kitaalamu: “Associazione Forma FP”, Ijumaa tarehe 3 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake amejikita katika mambo makuu matatu; vijana, mafunzo na taaluma. Kuna matukio ya kijamii yanayopelekea vijana wengi kuyakimbia makazi yao ili kutafuta maisha bora zaidi na hivyo kutekeleza ndoto yao ya maisha; kuna baadhi ya vijana wananyonywa na hivyo kutoridhika na hali ya maisha yao na hivyo kuona kwamba, kazi haina maana yoyote kwao. Haya ni matokeo ya kukosekana kwa elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya, itakayowasaidia kuingia katika soko la ajira, kumbe ni dhamana na wajibu wa watu wazima, kuwajengea vijana ari na moyo wa kazi, kwa kutoa kipaumbele kwa vijana wanaotoka katika familia maskini zaidi kwa kuwapatia misaada ya hali na mali. Jambo la pili ni kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kipya wanapata mafunzo kwa kuwaondolea hofu ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kwamba, inaweza kutatua matatizo yote yanayo mwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.
Kumbe, hapa kuna haja ya kuwekeza rasilimali na nguvu kama sehemu ya maboresho ya mafunzo yanayohitaji kusimikwa katika kipaji cha ubunifu; kwa kujikita pia katika utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi kwa kuthamini hasa kazi za mikono ya wanadamu, ambayo hadi sasa haziheshimiwi na wengi ndani ya jamii. Mafunzo ya elimu hayana budi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na familia, ili kuweza kuwarithisha vijana wa kizazi kipya tunu msingi za maisha ya kiutu, kifamilia na kijamii, ili kuwapatia vijana nyenzo msingi za kufanya mang’amuzi ya fursa za ajira na hatari ya mifumo ya unyonyaji. Mafunzo ya taaluma yanatoa utambulisho wa mfanyakazi na kwamba, kazi ni muhimu sana katika maisha na wito wa mwanadamu. Mafunzo ya taaluma yasaidie ukuaji wa mtu: kiroho, kitamaduni pamoja na kikazi. Ni muhimu ikiwa kama vijana watagundua miito ya kazi mbalimbali wanazoweza kutekeleza miongoni mwa watu wa Mungu, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza; kwa kuonesha ukarimu na sadaka, ili kutoa maana ya kazi. Baba Mtakatifu amewataka wajumbe waendelee kujitosa kwa ajili ya kuwapatia vijana, mafunzo na taaluma. Ni kwa njia ya sadaka na majitoleo yao, leo hii inawezekana kabisa kuunganisha kazi na wito wa mtu. Kimsingi majiundo makini kitaaluma ni mchakato unaomwezesha mfanyakazi kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake kwa kutambua na kugundua kwamba, yuko duniani na ndani ya jamii.