Waraka Kwa Maparoko: Maparoko Kwa Ajili ya Sinodi: Ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu pamoja na Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makleri, kwa pamoja wameandaa mkutano wa kimataifa ambao umewashirikisha Maparoko 300 walioteuliwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki toka sehemu mbalimbali za dunia, kushiriki mkutano maalum kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 2 Mei 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maparoko Kwa Ajili ya Sinodi. Mkutano wa Kimataifa.” Lengo ni kuendelea kujenga utamaduni wa kusikiliza, kusali na kufanya mang’amuzi ya pamoja kutoka katika Makanisa mahalia. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, mchakato huu, unawahusisha: mashemasi, mapadre na maaskofu, ili kusikiliza sauti na mchango wao. Mkutano huu umejikita katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, majadiliano na wataalam pamoja na maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Uteuzi wa Maparoko walioshiriki katika Maadhimisho haya ni kama ule uliotumika kwa ajili ya kuwachagua wajumbe wa Sinodi ya Maaskofu iliyofanyika mwezi Oktoba 2023. Maparoko walioteuliwa ni wale wenye mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha Kanisa la Kisinodi katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa. Matunda ya kazi hii ya Maparoko kutoka sehemu mbalimbali za dunia, yatachangia kutengeneza Hati ya Kutendea Kazi, “Instrumentum laboris” katika Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2024, itakayofikia kilele chake mwezi Oktoba 2024.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Waraka Maparoko Wote wanaotekeleza dhamana na utume wao sehemu mbalimbali za dunia, akiwashukuru kwa sadaka na majitoleo yao katika kuwahudumia watu wa Mungu na kuendelea kupandikiza mbegu ya Injili kwa mfano wa mpanzi anayesimuliwa katika Injili Mk 4:1-25. Baba Mtakatifu katika Waraka wake kwa Maparoko anakazia: Utume wa Maparoko katika ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi; Umuhimu wa kumwilisha karama na mapaji yaokwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu; Maparoko wajifunze Sanaa ya kufanya mang’amuzi ya pamoja kwa kujikita katika wongofu katika Roho Mtakatifu, washirikiane na Maaskofu wao katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kwamba, mchango wao ni muhimu sana katika maandalizi ya Hati ya Kutendea Kazi, Instrumentum laboris. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza Maparoko wote katika maisha na utume wao kwa watu wa Mungu wakati wa furaha na magumu katika maisha; kwa rasilimali na mahitaji yao msingi. Ni katika muktadha huu, Kanisa linawahitaji Maparoko kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili kutembea kwa pamoja katika Njia inayolielekeza Kanisa katika Millenia ya tatu ya Ukristo. Kanisa linaweza kuwa ni la kimisionari na kisinodi, ikiwa tu kutakuwepo na ushiriki mkamilifu wa Wabatizwa wote kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wanaparokia wanaitwa kuwa wahudumu wa Injili katika jamii, familia, mahali pao pa kazi na katika medani mbalimbali za maisha. Jumuiya za Kiparokia ziwe ni mahali ambapo Wabatizwa wanatekeleza dhamana na wajibu wao kama Mitume wamisionari, ili kushiriki furaha na maajabu ya Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Rej. Lk 10:17.
Huu ni mwaliko kwa Maparoko wote kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya sala, mang’amuzi, ari na mwamko wa kitume, ili kuhakikisha kwamba, huduma yao inakwenda sanjari na mahitaji ya Kisinodi, changamoto inayowekwa mbele ya viongozi wa Kanisa katika ngazi mbalimbali, kwani wameitwa na kuwekwa wakfu ili kuwasikiliza watu wa Mungu, wakiwa na uhakika kwamba, neema za Mungu mwenyezi zinawaambata, kwa kujikita katika mambo msingi, yaani kutangaza na kushuhudia Habari Njema na pale ambapo Jumuiya ya waamini inapokusanyika katika kuumega mkate. Maparoko watambue kwamba, wao ni wajenzi wa Kanisa la kimisionari na la kisinodi. Baba Mtakatifu anaorodhesha mambo makuu matatu yanayoweza kusaidia kubadilisha mtindo wa maisha sanjari na shughuli zao za kichungaji. ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano na waamini walei. Maparoko wanapaswa kutambua kwa hisia za imani karama ambazo, ziwe ni ndogo ama kubwa, zinajaliwa kwa walei kwa mitindo mingi mbalimbali Rej. “Presbyterorum ordinis”, yaani Huduma na Maisha ya Mapadre n. 9., mambo msingi katika mchakato wa uinjilishaji pamoja na kuibua karama na amana mbalimbali katika uinjilishaji. Na kwa njia hii, watakuwa na furaha ya kweli kama Mababa katika uinjilishaji bila kuwamiliki wengine, bali kwa kuwapatia fursa ya kuweza kuchangia katika mchakato wa uinjilishaji.
Baba Mtakatifu anawataka Maparoko kujenga utamaduni wa kufanya mang’amuzi ya pamoja, kwa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika wongofu wa Roho Mtakatifu, mchakato ambao umeonekana kuwa na manufaa zaidi katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu na kwamba, wataweza kuvuna matunda mengi kutoka kwenye medani mbalimbali za maisha. Ikumbukwe kwamba, mang’amuzi ya pamoja ni sehemu muhimu sana ya shughuli za kichungaji kwa Kanisa la Kisinodi. Mchakato huu unapaswa kumwilisha pia sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, ili hatimaye, uweze kumwilisha katika maisha ya Kikanisa; kwa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na mgawanyo wa dhamana na nyajibu mbalimbali miongoni mwa wahudumu na hivyo kupanga yote mintarafu mwanga wa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawataka Maparoko kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha udugu wa kibinadamu na Maaskofu wao mahalia, ili kuhisi ule ubaba na undugu, umoja na ushiriki katika Jumuiya zao! Haya ni mambo ambayo Maparoko wanapaswa kuyamwilisha kwanza katika maisha yao na kwa njia hii, wataweza kuaminika katika maisha na utume wao. Hili ni hitaji lililojitokeza wakati wa maadhimisho ya Mkutano wa Kimataifa wa Majiundo Endelevu miongoni mwa Mapadre, uliofanyika mwezi Februari 2024 mjini Roma na kuhudhuriwa na wajumbe 800, wakiwemo: maaskofu, mapadre na waamini walei, kutoka katika nchi 18.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa la kimisionari na kisinodi linawahitaji Maparoko kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” na kilele chake ni mwezi Oktoba 2024. Kumbe, mchango wao ni muhimu sana kama sehemu ya maandalizi ya Hati ya Kutendea Kazi, Instrumentum laboris. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee anawaalika Maparoko walioshiriki katika Mkutano wa Kimataifa ulionogeshwa na kauli mbiu: “Maparoko Kwa Ajili ya Sinodi. Mkutano wa Kimataifa” kuwa ni wamisionari wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kati yao na wanaporejea majimboni mwao, waendeleze ari na mwamko huo kati ya Mapadre wenzao. Waendeleze tafakari hii wakiwa na wazo la ujenzi wa Kanisa la kimisionari na kisinodi, sera na mikakati ya upyaisho wa utume wa Maparoko, ili kuiwezesha Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kupata mchango wao, tayari kuandaa Hati ya Kutendea Kazi, Instrumentum laboris. Kanisa linapenda kuendelea kuwasikiliza Maparoko kama sehemu ya mchango wao katika ujenzi wa Kanisa la kimisionari na kisinodi, mchakato ambao Baba Mtakatifu Francisko anaushiriki kikamilifu.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2024, Jumamosi tarehe 9 Oktoba 2021, alitoa hotuba elekezi, ambayo ni msingi wa maadhimisho ya Sinodi katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Watu wa Mungu wakajitambua kuwa wao ni sehemu ya Kanisa la Kisinodi, tayari kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Kristo Yesu, kwa kushirikiana na binadamu wote, kusikiliza kwa makini kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kuyaambia Makanisa. Huu ni wakati wa kuanza tena kufanya hija hii ya kitume, kama mwendelezo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa kunako mwaka 2021 na itafikia kilele chake Mwezi Oktoba 2024. Hii ni sehemu ya barua kutoka katika Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari hatua muhimu kuelekea Sinodi ya Mwaka 2024. Sekretarieti kuu ya Sinodi imekwisha kuchapisha mwongozo utakaotumika katika Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu.
Kardinali Lazzaro You Heung-sik, “Yu Hung Shik” Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makleri, katika salam zake kwa Maparoko wanaohudhuria mkutano huu, amekazia umuhimu wa kusali kila siku, kusikiliza na kuhudumia, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kielelezo cha ushuhuda wa furaha ya Injili, tayari kuimwilisha katika maisha na utume wa Kipadre. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa Kanisa linalofumbatwa katika: Fumbo, Ushirika na Utume, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kulitafakari Fumbo la Kanisa, kwa kuendelea kujielekeza katika umisionari unaowashirikisha watu wote wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ndiyo dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Ushirika na utume ni dhamana inayomwilishwa katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa watu wote wa Mungu kuweza kutembea bega kwa kwa bega katika umoja na ushirika. Huu ndio mtindo wa maisha na utume wa Kisinodi, unaowashirikisha wabatizwa wote katika Kanisa, kila mtu akitekeleza dhamana na wajibu wake. Huu ni wajibu mkubwa ambao Roho Mtakatifu amewakabidhi wachungaji wa Kanisa, ili Parokia ziweze kuwa ni mahali pa kushiriki maisha, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka anayetembea bega kwa bega na waja wake.
Kwa upande wake, Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu ameelezea umuhimu wa Kanisa mahalia kuwa ni sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anatembea bega kwa bega na waja wake katika furaha, majonzi, matumaini na hali ya kukata na kujikatia tamaa; kifo na maisha. Lakini ikumbukwe kwamba, haya ni matokeo ya historia ya maisha ya mwanadamu ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kuiandika bado katika maisha ya waja wake, parokiani, majimboni na katika jamii ya binadamu katika ujumla wake. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni kutembea pamoja na Mwenyezi Mungu, anayetembea na waja wake. Ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ambalo linatembea pamoja na Kristo Yesu, kama sehemu ya utekelezaji wa historia ya Mungu katika maisha ya mwanadamu na kama sehemu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, Paroko kimsingi ni mtu wa watu kwa ajili ya watu wa Mungu, ambaye yuko tayari kusoma barua kutoka kwa Kristo Yesu iliyoandikwa na Roho Mtakatifu. Parokia ni mahali muafaka pa uinjilishaji wa kina na kwamba, mkutano huu ni fursa kwa Maparoko kushirikisha mang’amuzi na uzoefu wao.