Wazazi na Walezi ni Wahusika Wakuu na Wasanifu wa Kwanza Wa Elimu Kwa Watoto Wao
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kongamano la “Apel” Yaani “Jumuiya ya Wazazi wa Elimu Bila Malipo” kuanzia tarehe 31 Mei hadi tarehe 2 Juni 2024 huko Valencia linawakusanya pamoja: Wasimamizi wa Apel, wawakilishi wa jumuiya za elimu, wakuu wa shule, walimu, wakurugenzi watendaji wa majimbo pamoja na washirika wa Apel kwa kuongozwa na kau mbiu “Wazazi ni waelimishaji.” Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusu Elimu ya Kikristo “Gravissimum educationis” wanazungumzia kuhusu wajibu na haki msingi za wazazi zisizofutika za kuwalea watoto wao, lazima wapewe uhuru wa kweli katika kuchagua shule, wapewe misaada ili waweze kuwa na nyenzo msingi za kuwachagulia watoto wao nafasi za elimu kulingana na dhamiri zao. Serikali kwa upande wake, inapaswa kuhifadhi haki za watoto kupewa elimu ya kufaa shuleni na itekeleze wajibu huu kwa kuzingatia kanuni auni. Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unawasihi waamini wafanye bidii kusaidiana katika kutafuta mbinu za kuelimisha na taratibu za masomo zifaazo, na katika kuwaandaa walimu watakaojua kuwafundisha vyema vijana. Vyama mbalimbali vya wazazi vitoe mchango wao ili kutimiza wajibu wa shule, hasa kwa upande wa kujenga na kudumisha maadili na utu wema ambako ni juu yake kutekeleza. Rej. Gravissimum educationis, 6. Ni katika muktadha huu wa wajibu na haki msingi za wazazi katika malezi ya watoto wao, Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la “Apel” anakazia kuhusu dhamana na wajibu wa wazazi katika malezi na kwamba, wao ni wasanifu wa kwanza wa elimu ya watoto wao; Jumuiya ya shule ni ulimwengu mdogo ulio wazi kwa siku za usoni, Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” na kwamba, elimu ni bahari na kwamba, haina mwisho.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anawakumbusha wazazi na walezi kwamba, wao ni wahusika wakuu na wasanifu wa kwanza wa elimu kwa watoto wao, dhamana na wajibu unaohitaji msaada wa jamii nzima kwa kuanzia katika familia ili kurithisha ujuzi na maarifa; kanuni bora za maadili na utu wema pamoja na tunu msingi za maisha ya kiroho. Muungano huu wa kielimu kwa hivyo, ni fursa ya kukuza elimu shirikishi ya mwanadamu ili kuhakikisha ujenzi wa udugu wa kibinadamu zaidi na katika mwelekeo wake wa maisha ya kiroho, ili hatimaye, kugundua mpango wa Mungu kwa kila mmoja wao. Kwa upande mwingine, anasema Baba Mtakatifu Jumuiya ya shule ni kama Ulimwengu mdogo, ulio halisi na wazi kwa siku zijazo ; kwa kuwashirikisha wadau muhimu katika mchakato wa elimu unaosimikwa katika fadhila ya upendo. Kumbe, wazazi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuhudumia Jumuiya zao za elimu. Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ni mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kujenga mfumo wa elimu unaojikita katika msingi wa elimu fungamanishi. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti zaidi katika elimu fungamanishi inayowataka vijana wa kizazi kipya kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa!
Baba Mtakatifu anakazia mfumo wa elimu itakayosaidia pia kuleta Mfumo Mpya wa Uchumi Duniani unaojikita katika wongofu wa kiikolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika mfumo wa elimu duniani unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu”, mahali ambapo watu wote, kadiri ya dhamana zao, wanashiriki wajibu wa kuunda mtandao ambao ni wazi katika ujenzi wa mafungamano ya kibinadamu, kwani kila mtu anakuwa na wajibu wa kuchangia katika mchakato wa maboresho ya elimu! Elimu pia inapaswa kujikita katika uaminifu wa maisha ya kiroho, maana ya utakatifu wa maisha ya mwanadamu; kanuni maadili na utu wema; kwa kushirikiana, kujadiliana, kusamehena na kukua katika umoja na mshikamano, huku wakiruhusu tofauti zao msingi kuimba wimbo mzuri na wenye upatanifu. Baba Mtakatifu anawakumbusha wazazi na walezi kwamba, elimu ni kama bahari haina mwisho; ina wakati wake wa shangwe na majaribu kama ilivyokuwa katika mbegu ya haradali. Rej. Mk 4:26-29. Kazi ya wazazi na waalimu ni ngumu na ni tete sana, lakini kwa subira na uvumilivu mkubwa itazaa matunda yasiyotazamiwa kwa wakati ujao. Huu ni mwaliko wa kukabiliana na changamoto mamboleo kwa ujasiri mkubwa.