Tafuta

Papa Francisko mbele ya Picha ya Bikira Maria Afya ta Waroma. Papa Francisko mbele ya Picha ya Bikira Maria Afya ta Waroma. 

Barua ya Papa katika fursa ya Miaka 80 ya ibada kwa Maria Afya ya Warumi

Kuna migogoro mingi ya wazi na kumwaga damu ya binadamu,msijitoe kwenye mantiki ya silaha.Haya yako katika Barua ya Papa Francisko katika fursa ya kumbukumbu ya miaka 80 ya ibada maalum ya Papa Pio XII na jiji la Roma kwa Maria Salus Populi Romani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.Papa anaomba maadhimisho hayo yawe fursa ya kutafakari kuhusu janga baya la vita.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 4 Juni 2024 ametuma Barua kwa Askofu Baldassarre Reina Askofu Msaidizi wa Jimbo la Roma katika fursa ya Maadhimisho ya Miaka 80 tangu ilipofanyika Ibada maalum kwa Maria Salus Populi Romani, yaani (Maria  Afya ya Waroma) wakati nchini Italia imegubikwa na vita na mji wa Roma unataka kuangamizwa. Katika barua hiyo Papa anabainisha "anavyoungana kiroho na Jumuiya nzima ya kijimbo ambayo inaadhimisha kumbukizi la mara ya kwanza ya kiliturujia kwa Mtakatifu Maria Afya ya Waroma, kwa kukumbuka ahadi ile ya Ibada maaalum ambayo Watu wa Roma, pamoja na Mchungaji wao, Papa Pio XII walifanya kwa Mama mnamo tarehe 4 Juni 1944, ili kumuomba aweze kuokoa mji, wakatiulikuwa unaelekea kuangamia kutokana na mapigano kati ya Jeshi la Ujerumani na Wale wa Muungano na Uingereza na Marekani."

Miaka 80 baadaye kumbukizi la tukio ni hai

Baba Mtakatifu anaeleza kuwa “Ibada ya kizamani ya picha inayotunzwa katika Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu, iko hai kwa karne,  katika moyo wa Waroma, ambayo walijielekeza kwayo ili kuwakilisha maombi na sala, hasa wakati wa tauni, majanga ya asili na vita. Matukio muhimu ya maisha ya kidini na ya kiraia ya Roma yalipata mwangwi mbele ya picha hii. Kwa hivyo haishangazi kwamba watu wa Roma walitaka kumtegemea tena Maria Salus Populi Romani wakati Jiji likikumbwa na jinamizi la uharibifu wa Kinazi. Miaka themanini baadaye, kumbukumbu ya tukio hilo iliyojaa maana sana inakusudiwa kuwa fursa ya sala kwa wale waliopoteza maisha katika Vita vya Pili vya Dunia na kwa ajili ya kutafakari upya juu ya janga hilo baya la vita. Migogoro mingi sana katika sehemu mbalimbali za dunia bado iko wazi leo hii."

Vita Ukraine, Palestina, Israel, Sudan,Myanmar na kwingineko

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia hiyo anafikiria hasa "Ukraine inayoteswa, Palestina na Israel, Sudan, Myanmar, ambako silaha bado zinaunguruma na damu nyingi zaidi za binadamu zinaendelea kumwagika. Haya ni majanga yanayowagusa wahanga wasio na hatia wasiohesabika, ambao vilio vyao vya ugaidi na mateso vinatilia shaka dhamiri za kila mtu kwamba: hatuwezi na hatupaswi kujitoa katika mantiki ya silaha!” Papa aidha anaeleza kuwa "Miaka 20 baada ya kumalizika kwa Vita vya II vya Kidunia mnamo 1965, Papa Mtakatifu Paulo wa VI, akizungumza kwenye Umoja wa Mataifa, alijiuliza: “Je, ulimwengu utawahi kubadilisha mawazo ya kipekee na ya kivita ambayo hadi sasa yamesuka sehemu kubwa ya historia yake?” (4 Oktoba 1965, AAS 57 [1965], 882). Swali hili, ambalo bado linangojea jibu, Baba Mtakatifu amesisitiza  kuwa “linachochea kila mtu kufanya kazi kwa dhati katika kuunga mkono amani Ulaya na ulimwenguni kote. Amani ni zawadi kutoka kwa Mungu, ambayo lazima pia leo hii inafaa mioyo inapatikane ili kuikaribisha na kufanya kazi ya kuwa wasanifu wa upatanisho na mashuhuda wa matumaini."

Matumaini ya Papa:Mipango ya tukio iweze kufufua nia ya ujenzi wa amani

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu  kwamba: “mipango iliyohamasishwa  ya kuadhimisha Ibada ya Watu  wengi kwa Mama wa Mungu, katika sehemu nne ambazo walikuwa wahusika wakuu wa tukio hilo, inaweza kufufua kati ya Waroma nia ya kuwa wajenzi wa amani wa kweli kila mahali, kuzindua upya udugu kama hali muhimu ya kuunda tena ili kusitisha migogoro na uhasama. Wale walio nayo ndani yao wenyewe na kwa ujasiri na upole, wajitolee kuunda vifungo, kuanzisha mahusiano kati ya watu, na kulainisha mivutano katika familia, kazini, shuleni, kati ya marafiki, na wanaweza kuwa wajenzi wa amani. Hivyo kutimiza hivyo  hali ya heri ya kiinjili: “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mt 5:9).

Bikira wa huruma na faraja aimarishe imani tumaini na mapendo

Kwa kuhitimisha barua hiyo, Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba: Bikira Maria, Mpatanishi wa neema, mwenye kukesha daima na kuwajali watoto wake wote, awapatie wanadamu wote zawadi ya maelewano na amani.” Na zaidi Papa amewakabidhi wakazi wote wa Roma, hasa wazee, wagonjwa, wapweke na wenye shida, kwa maombezi ya mama Maria Salus Populi Romani.  Yeye, Bikira wa huruma na faraja, aimarishe imani, tumaini na mapendo ili kuangazia upendo na huruma ya Mungu ulimwenguni. Kwa hisia hizo Papa anawahakikishia maombi yake  na kutoa Baraka yake  kwa moyo wote.

Papa na barua kuhusu Salus Popoli Romani
04 June 2024, 18:51