Hati ya Papa kuhusu Moyo Mtakatifu wa Yesu itachapishwa Septemba ijayo
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Katekesi yao, ametoa salamu kwa mahujaji kwa lugha mbali mbali. Akizungumza kwa waamini na mahujaji wa lugha ya kiitaliani Jumatano tarehe 5 Juni 2024 amesema: “Tuko tunasafiri kwa mwezi huu uliowekwa wakfu kwa Moyo Mtakatifu. Tarehe 27 Desemba mwaka jana iliadhimisha kumbukumbu ya miaka 350 ya udhihirisho wa kwanza wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa Mtakatifu Margherita Maria Alacoque.
Katika hafla hiyo, kipindi cha sherehe kilianza ambacho kitakamilika mnamo Juni 27 mwaka ujao. Kwa sababu hii nina furaha kuandaa hati inayokusanya tafakari za thamani za maandiko ya awali ya mafundisho na ya historia ndefu iliyoanzia kwenye Maandiko Matakatifu, ili kupendekeza tena leo hii, kwa Kanisa zima, ibada hii iliyojaa uzuri wa kiroho.” Baba Mtakatifu Francisko akiendelea amesema kuwa “Ninaamini kwamba itatufaa sana kutafakari mambo mbalimbali ya upendo wa Bwana yanayoweza kumulika njia ya kufanywa upya kikanisa; lakini pia yaseme jambo muhimu kwa ulimwengu ambao unaonekana kupoteza moyo wake. Ninawaomba mnisindikize kwa maombi, katika wakati huu wa maandalizi, kwa nia ya kuweka waraka huu kwa umma Septemba ijayo.” Ameeleza Baba Mtakatifu..
Tumwombe Mungu kwa maombezi ya Mama yake kwa ajili ya amani.
Baba Mtakatifu Francisko aidha amewakaribisha kwa moyo mkunjufu mahujaji wanaozungumza Kiitaliano. Hasa, amewasalimu vijana wa Seminari ya Kanda ya Puglia na kuwatia moyo kuitikia kwa furaha na ukarimu wito wa Bwana. Hatimaye, mawazo yake yamewaendea vijana, wagonjwa, wazee na wenyendoa wapya. “Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu na kumbukumbu ya Moyo Safi wa Maria, ambayo Kanisa linajiandaa kuiadhimisha siku zijazo, inatukumbusha umuhimu wa kuendana na upendo wa ukombozi wa Kristo na kutualika kumtumainia maombezi ya Mama wa Bwana.” Tumwombe Mungu kwa maombezi ya Mama yake kwa ajili ya amani.” Papa amesisitiza kuwa “Amani katika Ukraine inayoteswa, amani katika Palestina, katika Israel, amani katika Myanmar... Tuombe kwamba Mama huyo atupe zawadi ya amani na kwamba dunia isiteseke sana na vita. Bwana atubariki sisi sote! Amina.” Amehitimisha.