Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa viongozi wanaohudhuria mkutano wa G7 amekazia mapinduzi ya teknolojia ya akili mnemba Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa viongozi wanaohudhuria mkutano wa G7 amekazia mapinduzi ya teknolojia ya akili mnemba  (Vatican Media)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Wakuu wa G7 : Utu, Maadili na Siasa Safi

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa viongozi wanaohudhuria mkutano wa G7 amekazia mapinduzi ya teknolojia ya akili mnemba; teknolojia inayotumia hali ya binadamu, lakini bado ni tete sana; Utaratibu wa msingi wa teknolojia ya akili mnemba; umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na kanuni maadili; Siasa inayohitajika katika kujenga udugu na urafiki wa kijamii, ili kukuza na kudumisha amani ulimwenguni sanjari na utunzaji bora wa mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwenyezi Mungu aliwakirimia wanadamu Roho wake ili wapate ustadi, ufahamu na ujuzi katika kila kazi. Kwa hiyo sayansi na teknolojia ni bidhaa nzuri za uwezo wa ubunifu wa wanadamu na kwamba, teknolojia ya akili mnemba hutokana hasa na matumizi ya uwezo huu wa kazi ya uumbaji uliotolewa na Mwenyezi Mungu. Teknolojia ya akili mnemba ni chombo chenye nguvu sana kinachotumika katika medani mbalimbali za shughuli za mwanadamu. Kutoka katika dawa hadi katika ulimwengu wa kazi; utamaduni, mawasiliano, elimu na siasa na kwamba, matumizi ya teknolojia ya akili mnemba yanaathari zake katika maisha ya mwanadamu, mahusiano na mafungamano yake kijamii na hata jinsi ya kufikiria utambulisho wao kama wanadamu. Suala la teknolojia ya akili mnemba huchukuliwa kama utata, kwani kwa upande mmoja hutoa msisimko unaowezekana na wakati mwingine husababisha hofu kwa matokeo ambayo hutangulia. Kumbe hapa kuna hisia ya maendeleo makubwa yanayotokana na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba na wakati huo huo, woga unashamiri kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba.

Mkutano wa viongozi wakuu wa G7 Puglia, nchini Italia.
Mkutano wa viongozi wakuu wa G7 Puglia, nchini Italia.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 14 Juni 2024 wakati akishiriki mkutano wa Viongozi Wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7. Huu ni wito wa kutafuta, kujenga na kudumisha amani sanjari na ubinadamu katika enzi ya akili mnemba. Baba Mtakatifu anashiriki mkutano huu kwa mwaliko kutoka kwa Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mapinduzi ya teknolojia ya akili mnemba; teknolojia inayotumia hali ya binadamu, lakini bado ni tete sana; Utaratibu wa msingi wa teknolojia ya akili mnemba; umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na kanuni maadili; Siasa inayohitajika katika kujenga udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii, ili kukuza na kudumisha amani ulimwenguni sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, mapinduzi ya teknolojia ya akili mnemba yamesaidia kuunda mfumo mpya wa kijamii, kiasi kwamba, teknolojia hii inaweza kusaidia mchakato wa demokrasia, tafiti za kisayansi pamoja na kupunguza kazi zinazofanywa na mashine. Lakini maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba yanaweza kusababisha kukosekana kwa uwiano wa maendeleo kati ya nchi changa duniani na nchi zilizoendelea; ni teknolojia inayoweza kuibua matabaka kiasi cha kujenga utamaduni wa kutupa badala ya utamaduni wa kuwakutanisha watu. Maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba ni tishio linalohitaji tafakuri ya kina, ili kuweza kubaini changamoto zinazoletwa na teknolojia ya akili mnemba.

Papa Francisko: Akili mnemba, utu, maadili na siasa safi
Papa Francisko: Akili mnemba, utu, maadili na siasa safi

Hii ni teknolojia inayotumia hali ya binadamu, changamoto kwa binadamu wenyewe ni kuwa wazi kwa Mwenyezi Mungu pamoja na binadamu wenzao na kwamba, teknolojia hii inawaelekeza binadamu kwa maendeleo ya siku zijazo. Dhamiri ndicho kiini cha siri zaidi cha binadamu na hekalu la Mungu, ambamo sauti yake inasikika na utimilifu wa sheria hii ni upendo kwa Mungu na jirani. Kumbe, teknolojia ya akili mnemba inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zake msingi; kwa kukazia uhuru na uwajibikaji wake na kwa namna ya pekee ni kujihusisha na kanuni maadili na utu wema. Teknolojia ya akili mnemba isaidie kuzalisha nishati rafiki kwa matumizi ya binadamu. Lakini, teknolojia ya akili mnemba bado ni tete sana kwa sababu inajiendesha yenyewe, kinyume kabisa na matakwa na busara ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na udhibiti wa binadamu kwa kujikita katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Matumizi ya teknolojia ya akili mnemba katika shughuli za kijeshi ni hatari sana kwa sababu maisha ya binadamu yako hatarini na hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuchochea vita.

Wakuu wa G7 wakati wa mkutano wao Puglia, nchini Italia
Wakuu wa G7 wakati wa mkutano wao Puglia, nchini Italia

Utaratibu wa msingi wa teknolojia ya akili mnemba unajikita katika mchakato wa kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto zinazojitokeza, ili hatimaye kuboresha maisha. Lakini kumekuwepo na matumizi makubwa ya teknolojia ya akili mnemba kiasi hata cha kuanza kutumika Mahakamani; kujenga mahusiano na mafungamano ya kibinadamu pamoja na kukidhi mahitaji ya binadamu kimwili na kisaikolojia. Lakini ikumbukwe kwamba, teknolojia hii ni chombo tu na wala hakiwezi kuchukua nafasi ya binadamu. Ubora wa takwimu unaotolewa na teknolojia ya akili mnemba unategemea na maelezo yanayotolewa na binadamu. Teknolojia ya akili mnemba imewezesha watu wengi kuweza kujitafutia: ujuzi na maarifa kwa juhudi binafsi na kwamba, teknolojia hii ina mvuto mkubwa kwa wanafunzi wengi, lakini haiwasaidii sana katika kujibu maswali ya mitihani yao. Wanafunzi wanaonekana kuwa na udadisi mkubwa zaidi wa matumizi ya akili mnemba kuliko hata ilivyo kwa waalimu na wakufunzi wao na kwamba, wakati mwingine, makosa hayajitokezi mapema. Kuna hatari kubwa ya kuweza kutengeneza habari za kughushi na hivyo kuunda utamaduni wa “mwenye nguvu mpishe.” Kimsingi maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba, yanadumaza mchakato wa elimu, badala ya kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufanya upembuzi yakinifu, teknolojia hii, inawajengea tabia ya kurudia rudia.

Papa: Akili mnemba, utu, amani, kanuni maadili na siasa safi
Papa: Akili mnemba, utu, amani, kanuni maadili na siasa safi

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na kanuni maadili ili kujibu changamoto za kijamii zinazoendelea kuibuliwa na maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba kiasi cha kuathiri utu wa binadamu. Teknolojia huzaliwa kwa kusudi na, katika athari zake kwa jamii ya wanadamu, daima huwakilisha aina ya utaratibu katika mahusiano ya kijamii na mpangilio wa mamlaka, hivyo kuwawezesha watu fulani kufanya vitendo maalum huku wakiwazuia wengine kufanya tofauti.  Kwa njia iliyo wazi zaidi au kidogo, mwelekeo huu wa nguvu wa teknolojia daima unajumuisha mtazamo wa ulimwengu wa wale walioivumbua tekenolojia hii na kuiendeleza. Teknolojia ya akili mnemba isaidie kujenga leo na kesho iliyo njema na bora zaidi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, msukumo wa kimaadili ni muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, tarehe 28 Februari 2020 ni kumbukumbu ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Ushirikiano unaojulikana kama “Rome Call For Artificial Intelligence” umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili uliowekwa saini kati ya Taasisi ya Kipapa ya Maisha, Kampuni ya Microsoft, Kampuni ya IBM pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Food and Agriculture Organzation of the United Nations"; kifupi: FAO). Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba watu wote wenye mapenzi mema wataendelea kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge na kwamba, maendeleo ni kwa ajili ya wote!

Nyumba za asili za watu wa Puglia, Kusini mwa Italia
Nyumba za asili za watu wa Puglia, Kusini mwa Italia

Siasa inayohitajika katika kujenga udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii, inapania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha amani ulimwenguni sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali, yamesaidia maboresho makubwa katika matumizi ya “akili mnemba” katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu, iwe kwa mtu binafsi au jamii katika ujumla wake. Mapinduzi haya makubwa ya teknolijia yanawawezesha watu kujifahamu sanjari na kuufahamu ulimwengu unaowazunguka, kiasi hata cha kuathiri maamuzi, uwezo wa kufiki na kutenda katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Leo hii utashi wa mwanadamu unaathiriwa kwa namna ya pekee na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba kutokana na mchango wake mkubwa! Siasa inayojihusisha na matokeo ya haraka ikisaidiwa na sekta ya manunuzi husukumwa na uzalishaji wa muda mfupi na kwa masilahi ya watu wachache ndani ya jamii. Kumbe, ujuzi halisi wa uongozi unajionesha pale ambapo mkazo zaidi ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa taifa na ujenzi wa familia ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kuweka uhusiano mwema baina ya siasa na uchumi kwa ajili ya mustakabali wa binadamu. Na hii ndiyo hali halisi ya teknolojia ya akili mnemba. Ni wajibu wa binadamu kuweza kuitumia vyema na kwamba, lazima ziwepo sera bora zaidi za matumizi bora ya teknolojia ya akili mnemba.

Papa g7 Italia
14 June 2024, 15:43