Abazia ya Montevergine inaadhimisha kumbukizi ya miaka mia tisa tangu kuanzishwa kwake Abazia ya Montevergine inaadhimisha kumbukizi ya miaka mia tisa tangu kuanzishwa kwake   (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 900 ya Abasia ya Montevergine: Huduma ya Neno la Mungu

Madhabahu ya Bikira Maria wa “Montevergine” ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu! Baba Mtakatifu anasema, Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kusali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kufanya toba na kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Abasia ya “Montevergine” iliyoanzishwa na Mtakatifu Guglielmo wa Vercelli mwaka 1124 inaadhimisha Jubilei ya Miaka Mia Tisa tangu Kuanzishwa kwake. Kanisa limejengwa kilimani, kwa ajili ya wahudumu wa Neno la Mungu; mahali pa Sala na Tafakari ya kina; sehemu makini ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; hapa ni mahali ambapo Injili ya upendo inamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu, kiasi kwamba, watawa wanageuka na kuwa ni zawadi ya Mungu “Esto donum Deo ut sis donum Dei” na kuwa kweli ni watu wa Mungu.”

Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya Montevergine.
Jubilei ya Miaka 900 tangu kuanzishwa kwa Abasia ya Montevergine.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 13 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Abazia ya Montevergine inayoadhimisha kumbukizi ya miaka mia tisa tangu kuanzishwa kwake na kwamba, wito wa umonasteri unapata chimbuko lake katika matendo ya Mungu “Opus Dei” yaani katika maisha ya sala kama anavyokazia Mtakatifu Benedikto, Abate. Madhabahu ya Bikira Maria wa “Montevergine” ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu! Baba Mtakatifu anasema, Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao!

Madhabahu ya Montevergine ni mlango wa uinjilishaji mpya
Madhabahu ya Montevergine ni mlango wa uinjilishaji mpya

Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa, kuthaminiwa na kupendwa. Mara nyingi watu wanafanya hija kutokana na kuvutwa na Mapokeo, utajiri wa sanaa, uzuri wa mazingira pamoja na kufuata ushauri kutoka kwa jirani zao! Mahujaji kama hawa wanapoonja ukarimu, mioyo yao inafunguka na hivyo kuanza kujenga urafiki na hatimaye, kujiaminisha kwa Kristo na Kanisa lake! Watu wanaweza kukata tamaa, ikiwa kama hawataonja ukarimu kutoka kwa wenyeji wao! Madhabahu ya Bikira Maria wa Montevergine ni mahali pa sala na ukarimu kwa watu wa Mungu wanaokimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, anayewaonesha Mtoto Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kwa watu wake, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni zawadi ya Mungu, kwa njia ya sala kama anavyomwonesha Mtoto Yesu akiwa ameketi miguuni pake, kwa wale wote wanaokutana nao katika viunga vya maisha yao, lakini zaidi nyoyoni mwao. Baba Mtakatifu anasema, katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Jumuiya hii ilibahatika kuwa ni hifadhi ya Sanda Takatifu “Sacra Sindone na kwa Kiingereza “Holy Shrould” na hivyo Sanda hii inahifadhi siri kubwa ya Madhabahu ya Bikira Maria wa “Montevergine,” waliyotunza na kuipatia heshima; ikahifadhiwa mahali salama, ili kuilinda dhidi ya mashambulizi ya kivita, kielelezo makini cha wito wao wa asili, unaowataka kuihifadhi kikamilifu ile Sura ya Kristo Yesu iliyoko ndani mwao, tayari kuwashirikisha ndugu zao katika Kristo.

Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya
Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya

 

Baba Mtakatifu anapenda kutoa mwaliko kwa watawa hawa kuhakikisha wanakuwa ni zawadi kwa ajili ya jirani zao, kwa kuonesha moyo wa ukarimu na mapendo kwa wale wote wanaopanda Madhabahuni hapo kwa ajili ya kusali, kushiriki katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti ya Upatanisho walindwe kwa tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu. Kuwa Wamonaki kunawafanya kuwa mbali na malimwengu, lakini karibu sana na walimwengu katika shida na mahangaiko yao na hivyo kuwahifadhi katika kimya na ushirika, alama hai ya uwepo angavu wa Mungu Baba. Baba Mtakatifu amewaonya Wamonaki hawa kutokukengeuka na hatimaye, kutopoa na kumezwa na malimwengu, bali wajiruhusu daima mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kupyaisha nyoyo zao na hivyo kuwapatia nafasi ya kuendelea kukua ndani mwake, ili wale wanaotafuta mwanga angavu kamwe wasikatishwe tamaa. Jumuiya ya Abazia ya Montevergine imebahatika sana kupata hifadhi nyumbani mwa Bikira Maria, anayewaangalia kwa jicho la huruma, linalohifadhiwa na “Mama Schiavona” kama anavyojulikana na wengi. Baba Mtakatifu anawaalika Wamonaki hawa kukuza ndani mwao amana na utajiri huu, ili hatimaye, waweze kuwashirikisha na wengine wote.

Monteverine

 

 

15 June 2024, 14:08