Tafuta

Katekesi Roho Mtakatifu na Bibi Arusi: Roho Mtakatifu na Maandiko Matakatifu

Roho Mtakatifu ndiye Mfafanuzi wa Maandiko Matakatifu. Maandiko yote Matakatifu ni kitabu kimoja cha Mungu, na kitabu hiki kimoja ni Kristo Yesu, kwa sababu kila Andiko la Mungu husema juu ya Kristo Yesu na kila Andiko la Mungu hukamilika katika Kristo Yesu. Maandiko Matakatifu yana Neno la Mungu, na kwa kuwa yamevuviwa ni kweli Neno la Mungu. Rej. DV 24. Mungu ndiye Mwandishi wa Maandiko Matakatifu, kwa sababu ndiye aliyewavuvia watu kuandika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo, Jumatano tarehe 29 Mei 2024 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu.” Tafakari hii imenogeshwa na Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Mwanzo 1: 1-2: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.” Mwa 1: 1-2. Baba Mtakatifu anasema, katika Katekesi hii atawazamisha waamini katika hatua kuu tatu muhimu katika historia ya wokovu: Agano la Kale, Agano Jipya na Nyakati za Kanisa. Daima waamini wakimkazia macho Kristo Yesu ambaye ni tumaini lao. Kile ambacho kiliahidiwa kwenye Agano la Kale, kinapata utimilifui wake kwenye Agano Jipya na la Milele katika Kristo Yesu. Katekesi hii ni kama kufuata mzunguko wa jua tangu machweo hadi kuzama kwake. Ni katekesi inayojikita kwa Roho Mtakatifu katika kazi ya uumbaji, Mbingu na nchi zinatangaza utukufu wa Mungu na kwamba, kwa Katekesi hii, waamini na watu wenye mapenzi mema, wamtambua Roho Mtakatifu Muumbaji. Baba Mtakatifu anasema, “Upepo huvuma unapotaka. Palipo na Roho wa Mungu, pana uhuru.” Anawaalika watu wa Mungu kumwomba Kristo Yesu awaweke huru kwa njia ya Roho wake Mtakatifu, ili wakiwa huru waweze kutumikia kwa upendo na furaha kuu. “Kila Andiko lina uvuvio wa Mungu.” Kujua upendo wa Mungu kutoka kwa maneno ya Mungu” ndiyo kauli mbiu iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 12 Juni 2024. Mwenyezi Mungu ndiye Mwandishi wa Maandiko Matakatifu. “Ukweli uliofunuliwa na Mungu, ambao umo katika Maandiko Matakatifu, umekabidhiwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu na kwamba, vitabu vilivyovuviwa vinafundisha ukweli na kwamba, Ukristo ni dini ya “Neno la Mungu.”

Roho Mtakatifu ndiye Mfafanuzi wa Maandiko Matakatifu
Roho Mtakatifu ndiye Mfafanuzi wa Maandiko Matakatifu

Roho Mtakatifu ndiye Mfafanuzi wa Maandiko Matakatifu. Maandiko yote Matakatifu ni kitabu kimoja cha Mungu, na kitabu hiki kimoja ni Kristo Yesu, kwa sababu kila Andiko la Mungu husema juu ya Kristo Yesu na kila Andiko la Mungu hukamilika katika Kristo Yesu. Maandiko Matakatifu yana Neno la Mungu, na kwa kuwa yamevuviwa ni kweli Neno la Mungu. Rej. DV 24. Mungu ndiye Mwandishi wa Maandiko Matakatifu, kwa sababu ndiye aliyewavuvia watu walioyaandika. Yeye alifanya kazi ndani yao na kwa njia yao. Kwa namna hiyo anatuhakikishia kwamba waliyoyaandika yanafundisha ukweli wake kwa wokovu bila kosa. Rej. KKK 101-141. Kuhusu uaminifu kwa Neno la Mitume na Manabii, Mtume Petro katika Waraka wake wa Pili kwa Watu wote anasema, “Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” 2 Pet 1:20-21. Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, Roho Mtakatifu ndiye aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Anakazia Maandiko Matakatifu pamoja na Mapokeo ya Kanisa, kuwa ndiyo kanuni kuu kuliko zote ya maisha na utume wake katika imani. Ni Maandiko yaliyovuviwa na Mungu na kutungwa mara moja kwa daima, yanashirikisha bila hitilafu yoyote ile Neno la Mungu mwenyewe; hii ni sauti ya Roho Mtakatifu katika maneno ya Manabii na Mitume.

Ukristo ni dini ya neno la Mungu
Ukristo ni dini ya neno la Mungu

Neno la Mungu ni hai, tena lina nguvu, laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Ni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, Kristo Mfufuka aliwafunulia akili zao wapate kuelewa Maandiko Matakatifu. Rej. Lk 24:45. Huu ni mwaliko kwa kuyasoma Maandiko Matakatifu kwa jicho la imani na sala, ili kuweza kupata mwanga wa Roho Mtakatifu na hatimaye, kuyatambua mapenzi ya Mungu katika maisha. Neno la Mungu ni egemeo na nguvu kwa Kanisa; ni uthabiti wa imani, chakula cha roho na chemchemi safi na ya daima ya maisha ya kiroho kwa watoto wa Kanisa. Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu. Rej. Ebr 4:12. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ndiye kiini cha Maandiko Matakatifu na kwamba, Mama Kanisa anayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, tafsiri za Biblia zinakuwa sahihi na aminifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Ni neema kwa mwamini kuweza kujitambua katika baadhi ya vifungu vya Maandiko Matakatifu au katika mazingira fulani ya Maandiko Matakatifu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Neno la Mungu limeandikwa kwa ajili ya watu wote. Neno la Mungu ni nguvu ya Roho Mtakatifu linapopokelewa kwa moyo mnyofu, ili kuleta mabadiliko katika maisha ya mwamini. Mapokeo ya Kikristo yamesheheni amana na utajiri mkubwa wa mang’amuzi na tafakari mintarafu Neno la Mungu. Kwa namna ya pekee, hili linajidhihirisha katika “Lectio Divina.” Maana yake halisi ni “Masomo ya kimungu” yaani njia ya kutafakari Neno la Mungu katika hatua nne: Mosi, Kusoma, “Lectio”, Neno la Mungu kwa umakini na utii mkubwa kwa Neno la Mungu, ili kuweza kufahamu mambo msingi yanayofumbatwa katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu. Hatua inayofuata ni kuzama katika tafakari kwa msaada wa Neno la Mungu, kiasi kwamba, vile vifungu vya Maandiko Matakatifu vinakuwa ni sehemu ya sala. Hii ndiyo hatua ya Pili yaani: Kuwaza, “Meditatio”. Sehemu ya tatu ni Kusali “Orati”, hatimaye ni Kutafakari “Contemplatio.”

Mungu ndiye Mwandishi wa Maandiko Matakatifu
Mungu ndiye Mwandishi wa Maandiko Matakatifu

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mahubiri yanayotolewa kwenye Ibada ya Misa Takatifu yawasaidie waamini kulitafsiri na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anaendelea kukazia umuhimu wa mahubiri kuwa ni mafupi, yanayosheheni ujumbe wa Neno la Mungu, unaopaswa kufanyiwa kazi, ili kuandika “Kitabu cha Maisha.” Waamini wajitahidi kulipokea na kulihifadhi Neno la Mungu katika sakafu ya maisha yao. Mwenyezi Mungu amejifunua mwenyewe kwa njia ya Maandiko Matakatifu, katika upendo wake usiokuwa na mipaka anaongea na wanadamu kama na marafiki, tena ukaa nao ili kuwaalika na kumpokea katika ushirika naye. Kwa njia hii ufunuo wa ukweli juu ya Mungu na juu ya wokovu wa mwanadamu unang’ara kwa njia ya Kristo Yesu, ambaye Yeye mwenyewe ndiye mshenga na utimilifu wa ufunuo wote. Rej. Dei verbum 2. Baba Mtakatifu anawashauri waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga utamaduni wa kutembea na kusoma Neno la Mungu, na kwa njia hii, wataweza kuwa karibu na Roho Mtakatifu, anayewasaidia waamini kupokea upendo wa Mungu na kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku!

Maandiko Matakatifu
12 June 2024, 15:07

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >