Kumbukizi ya Miaka 40 ya Kwaya ya Jimbo Kuu la Roma: Utulivu, Ushirika na Furaha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Muziki Mtakatifu ni chombo cha ibada na uinjilishaji; ni amana na utajiri wa Kanisa; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ibada, uchaji, unyenyekevu na unyoofu wa moyo! Hii inatokana na ukweli kwamba, nyimbo na muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa zinawasaidia waamini kuzamisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa! Muziki mtakatifu unasaidia sana maboresho na ushiriki wa waamini katika Liturujia na maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa, changamoto kwa wanakwaya ni kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha waamini wengine furaha ya Injili kwa njia ya muziki mtakatifu. Ikumbukwe kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayowakirimia waamini matumaini ya kuimba huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, hadi pale atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Mtakatifu Augustino anasema, “Qui bene cantat bis orat” yaani “Anayeimba vizuri anasali mara mbili” ili Mungu atukuzwe na wanadamu wapate kutakatifuzwa.”
Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Kwaya ya Jimbo kuu la Roma, yaani Mwezi Juni 1984 na Monsinyo Marco Frisina, kuanzia tarehe 7 hadi 9 Juni 2024 kunafanyika maadhimisho haya ambayo yamedhaminiwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu, Taasisi ya Kipapa ya Muziki Mtakatifu pamoja na “Nova Opera.” Hili ni tukio ambalo limewakusanya “Vigogo” wa Muziki Mtakatifu kutoka sehemu mbalimbali za dunia ambao, Jumamosi tarehe 8 Juni 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake amekazia: Utulivu, Ushirika na Furaha. Kristo Yesu katika maisha na utume wake alitoa kipaumbele cha pekee kwa watoto, kwani unyenyekevu wa watoto ni kielelezo cha wale wanaoutafuta Ufalme wa Mungu na kwamba, kumbukizi hii ni muhimu kwani inawatia shime wanakwaya kuendelea kutoa huduma hii muhimu kwa Jimbo kuu la Roma na sehemu mbalimbali za dunia. Kongamano hili la Nne Kimataifa linawashirikisha wanakwaya kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanaotoa huduma yao katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na kwamba, wanaunganishwa na imani na upendo kwa Muziki Mtakatifu, kielelezo makini cha umoja.
Baba Mtakatifu anasema, Muziki unawaletea watu amani na utulivu wa ndani; faraja kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; ni lugha isiyohitaji kutafsiriwa, ni amana na utajiri unaowafundisha watu umuhimu wa ujenzi wa sanaa ya kusikiliza kwa makini na kujifunza na kutafakari matendo makuu ya Mungu yanayowazunguka na hatimaye, kujenga amani na utulivu. Muziki Mtakatifu unasaidia kujenga ushirika, kila mwanakwaya akichangia karama na mapaji yake na kwamba, ufanisi wao unategemea ushirika wa kila mwanakwaya. Hivi ndivyo maisha ya Kanisa yanavyopaswa kuwa, yaani kila mtu atekeleze dhamana na wajibu wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Jumuiya nzima ya waamini, ili Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa na mwanadamu kutakatifuzwa. Rej. Zab 47:1. Tangu mwanzo, Muziki Mtakatifu umekuwa ni chemchemi na amana ya sanaa, uzuri na tasaufi. Hii ni changamoto ya kuondokana na uchu wa madaraka, wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko; kinzani na mipasuko; hali ambayo inaweza kuifanya kwaya isiwe ni chemchemi ya furaha. Kumbe, wanakwaya wanapaswa kujizatiti katika kukuza na kudumisha tasaufi ya maisha na wito wao kwa njia ya sala, tafakari makini ya Neno la Mungu sanjari na maisha ya Kisakramenti, kwa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kwa moyo na akili zao, ili kweli Muziki uweze kuwa ni majitoleo na sadaka ya furaha kwa Mwenyezi Mungu kama ambayo Mtakatifu Paulo anavyokazia katika utenzi wake juu ya upendo. Rej. 1Kor 13:1-13. Huu ni mwaliko kwa wanakwaya kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha kama anavyosema Mtakatifu Augustino. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanakwaya kwa huduma makini kwa Kanisa katika sala na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.