Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 Yanabeba Ujumbe Mzito wa Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Jiji la Roma tarehe 10 Juni 2024 ni muhimu sana, wakati huu, wa maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025 ya Ukristo. Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Katika Tamko hili, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Matumaini katika Neno la Mungu ili kuamini, kutumaini, kupenda na kuvumilia kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni mahujaji wa matumaini. Alama za matumaini zinazomwilishwa katika amani, kwa kujikita katika Injili ya uhai, maboresho ya magereza; huduma kwa wagonjwa, vijana, wahamiaji na wakimbizi, wazee na maskini. Wito wa matumaini kwa kujikita katika matumizi bora ya rasilimali za dunia; msamaha wa madeni ya nje kwa nchi zinazoendelea duniani.
Roberto Gualtieri, Meya wa Jiji la Roma anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanabeba ujumbe mzito wa matumaini kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo; hii ni fursa kwa watu wateule wa Mungu kujikita katika ujenzi wa tunu msingi za kibinadamu zinazosimikwa katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Lengo kuu ni kujizatiti kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ujenzi wa uchumi shirikishi sanjari na ujenzi wa urafiki wa kijamii.
Kwa upande wake Mheshimiwa Svetlana Celli, Mwenyekiti wa Mkutano mkuu wa Jiji la Roma katika hotuba yake ya utangulizi kwa Baba Mtakatifu Francisko amekazia kuhusu umuhimu wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020; Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo pamoja na ujenzi wa amani ya kudumu sehemu mbalimbali za dunia. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020, unagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu inakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.
Baba Mtakatifu anagusia kuhusu siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa.” Watu wa Mungu hawana budi kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana. Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Dini na udugu ni chanda na pete; hapa mkazo ni umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili.
Ni katika muktadha huu, Mheshimiwa Svetlana Celli, Mwenyekiti wa Mkutano mkuu wa Jiji la Roma anasema, Waraka huu unatajwa kuwa kati ya nyaraka bora zaidi katika masuala ya kisiasa. Ni waraka unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu; malengo ya binadamu na changamoto mamboleo ili kuhakikisha kwamba, haki za kila mtu zinalindwa na kuheshimiwa; kwa kuendelea kujikita katika utu na ukarimu. Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” baada ya dhoruba ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; vita inayoendelea kupiganwa vipande vipande sehemu mbalimbali za dunia. Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini.
Huu ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Jiji la Roma linaendelea kuwekeza katika miundo mbinu ili kuwakirimia mahujaji na wageni watakaofika Roma kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei. Maadhimisho haya ni muda muafaka wa kupyaisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, ili kuragibisha ari na mwamko wa jamii fungamanishi, inayosimikwa katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu pamoja na ukarimu. Roma ni mji unaosafiri kuyaendea ya mbeleni kwa matumaini huku ukiendelea kukita mizizi yake katika mapokeo na historia yake; kwa kuendelea kujizatiti zaidi katika majadiliano na ujenzi wa demokrasia. Jiji la Roma linapenda kuuunga mkono jitihada za Baba Mtakatifu Francisko za kutaka kusitisha vita sehemu mbalimbali za dunia, na hivyo Jumuiya ya Kimataifa kuanza kujikita katika ujenzi wa amani ya kudumu. Kuna waathirika wengi wa vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia. Umefika wakati kwa chuki, uhasama na vita kutoweka na hivyo kuachia nafasi haki na amani; matumaini, heshima; udugu wa kibinadamu pamoja na maridhiano kushika kasi kati ya watu na tamaduni mbalimbali.