Majadiliano ya Kidini Yanasaidia Kudumisha: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali duniani kufahamiana, kuheshimiana na kushirikiana kwa dhati katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani. Waamini wanaweza kujenga na kudumisha umoja, udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii kwa kusaidiana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ushuhuda wa umoja na udugu wa kibinadamu ni tunu ya thamani kubwa katika ulimwengu mamboleo.
Adui mkubwa wa mchakato wa majadiliano ya kidini ni woga na wasiwasi usiokuwa na msingi, mambo yanayochangia watu wa dini mbalimbali kushindwa kufahamiana na hatimaye, kuishi kwa amani, umoja na udugu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo tofauti zao za kidini si sababu msingi ya malumbano na kinzani zisizo na tija wala mashiko kwa watu. Watambue kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja, Mzee Ibrahimu, Baba wa imani; mwaliko wa kuwa wazi, wenye upendo na ukarimu, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa familia kubwa ya binadamu. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 26 Juni 2024 alipokutana na kuzungumza na baadhi ya waamini wa dini ya Kiislam kutoka Bologna, nchini Italia.
Baba Mtakatifu anasema, majadiliano ya kidini yanayosimikwa katika ukweli na uwazi kati ya Wakristo na waamini wa dini ya Kiislam ni utii kwa mapenzi ya Mungu, ili watu wote waweze kupendana, kusaidiana pamoja na kutatua changamoto za maisha, kwa kusikilizana na kusaidiana; kwa kuelewana katika hali ya unyenyekevu na uvumilivu mkuu. Majadiliano ya kidini yanasaidia kutambua, kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kati ya haki hizi ni: ile ya uhuru wa dhamiri na uhuru wa kuabudu, kila mtu akiwa huru kufanya maamuzi kuhusu imani yake, na wala kusiwepo wongofu wa shuruti ili mwamini kuweza kujipatia fedha au ajira, wala kutumia ujinga wa waamini kuwaongoa. Kusiwepo ndoa za shuruti kama njia ya kuwaongoa baadhi ya watu kufuata dini ambayo ni kinyume cha dhamiri nyofu ya mtu. Baba Mtakatifu Francisko amewatia shime waamini wa dini ya Kiislam kutoka Bologna kuendelea kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano mazuri na Kanisa Katoliki, Maaskofu, Mapadre pamoja na waamini katika ujumla wake; kwa kuheshimiana na hivyo kuendelea kujenga urafiki wa kijamii. Ulimwengu mamboleo unawahitaji wajenzi wa amani jamii duniani. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kuwa ni vyombo na wajenzi amani.