Tafuta

Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Jiji la Roma tarehe 10 Juni 2024 Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Jiji la Roma tarehe 10 Juni 2024   (Vatican Media)

Mji wa Roma Una Nafasi ya Pekee Kwa Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa

Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa Jiji la Roma. Amekazia dhamana ya Kanisa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, Mkataba wa Lateran, uliofanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984 na kwamba, kwa mwaka huu, marekebisho haya yanatimiza miaka 40; Umuhimu wa Mji wa Roma katika medani za Kimataifa sanjari na Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Mji wa Roma ni wa pekee sana duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Jiji la Roma tarehe 10 Juni 2024 ni muhimu sana, wakati huu, wa maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025 ya Ukristo. Hili ni tukio la shangwe na furaha Mji wa Roma unapoadhimisha kumbukizi ya miaka 2, 800 tangu kuanzishwa kwake, kwa waamini huu ni upendeleo wa pekee. Roma ya zamani ni maarufu sana kwa maendeleo ya sheria, utaratibu na ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa ujenzi imara na wakudumu, kielelezo cha uthabiti na uhakika wa usalama, mambo msingi yanayoufanya mji wa Roma kuwa ni kitovu cha ustaarabu na ukarimu kwa kuwapokea wageni na mahujaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia na hivyo kuwashirikisha katika maisha yake ya kiraia na kijamii kiasi hata cha kuwapandisha hadhi kuwa ni sehemu ya viongozi wakuu wa Serikali. Utamaduni wa mji wa Roma ya zamani, ulisheheni tunu msingi na ujumbe uliosimikwa kwenye udugu wa kibinadamu, upendo, matumaini na uhuru wa kweli; mambo yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo. Huu ni mji ambao umesheheni shuhuda za wafiadini na waungama imani; vyombo na wajumbe wa Injili ya upendo. Kwa Warumi iliwabidi kufunga safari ya Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Golgota na hatimaye kuteremka chini kushuhudia Kaburi wazi la Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, jibu makini la ukweli, haki na upendo. Hii ndiyo Habari Njema ya Wokovu iliyotangwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu, aliyeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu na kubadili hali na mazingira ya nyakati zake. Kristo Yesu akawa ni chemchemi ya matumaini yaliyokuja kufutilia mbali kashfa ya utumwa kutoka katika sura ya nchi; utumwa unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mji wa Roma unayo nafasi ya pekee kwa Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa
Mji wa Roma unayo nafasi ya pekee kwa Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa

Hali hii inajitokeza hata katika ulimwengu mamboleo, kwa kufahamu au kwa kutofahamu, kiasi cha kuhatarisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kiasi hata cha kuibuka kwa mifumo ya kibaguzi inayopelekea baadhi ya watu katika jamii kujikuta wakiwa hawana uhakika wa usalama wa maisha yao! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa Jiji la Roma. Amekazia dhamana ya Kanisa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, Mkataba wa Lateran, uliofanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984 na kwamba, kwa mwaka huu, marekebisho haya yanatimiza miaka 40; Umuhimu wa Mji wa Roma katika medani za Kimataifa sanjari na Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Roma ya utawala wa Kaisari ilifuatiwa na Roma ya Mapapa, warithi wa Mtume Petro, ambao "husimamia kwa upendo" juu ya Kanisa zima na ambao, katika karne kadhaa, pia walipaswa kuchukua jukumu la kubadilisha mfumo wa utawala na mamlaka ya kiraia katika mgawanyiko unaoendelea wa ulimwengu wa kale. Mambo mengi yalibadilika, lakini wito wa mji wa Roma kwa ulimwengu wote ulithibitishwa na kuinuliwa. Kwa kweli, ingawa upeo wa kijiografia wa Dola ya Kirumi ulikuwa na moyo wake katika ulimwengu wa Mediterania na, ingawa ulikuwa mkubwa sana, lakini haukuhusisha ulimwengu wote, kumbe, utume wa Kanisa hauna mipaka katika dunia hii. Kanisa halina budi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Kristo Yesu, matendo yake na maneno yake ya wokovu kwa watu wa Mataifa. Muungano wa Italia, ulifungua ukurasa na awamu mpya ilianza baada ya migogoro, kinzani na kutoelewana kati ya Vatican na Italia, hatimaye, ukafikiwa muafaka wa kile kinachoitwa “Suala la Kiroma” takribani miaka 95 iliyopita, upatanisho kati ya utawala wa kiraia pamoja na Vatican.

Kumbukizi ya Miaka 40 ya Marekebisho ya Mkataba wa Laterano
Kumbukizi ya Miaka 40 ya Marekebisho ya Mkataba wa Laterano

Kardinali Pietro Gasparri, Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati huo kwa niaba ya Kanisa pamoja na Bwana Benito Mussolini, Waziri Mkuu wa Italia kwa niaba ya Serikali ya Italia, walitiliana saini Mkataba wa Lateran maarufu kama “Patti Lateranensi.” Mkataba huu ulikuwa na sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuhitimisha kinzani na mpasuko uliokuwa umejitokeza baada ya Serikali ya Italia kuvamia mji wa Roma kunako mwaka 1870. Mkataba huu ulitoa uhuru kwa Kanisa Katoliki nchini Italia kuweza kujiamria mambo yake bila kuingiliwa na Serikali. Huu ni msingi wa uhuru wa kuabudu. Vatican ikapewa mamlaka kamili ya kujisimamia yenyewe katika shughuli zake na Serikali ya Italia, tangu wakati huo, ikatambua uhuru na mamlaka ya mji wa Vatican hata katika udogo wake. Mkataba huu, uliiwezesha Vatican “Kiti Kitakatifu-Holy See” kuwa na uhuru kamili kuhusiana na masuala ya dini na imani. Mkataba wa Lateran, ulifanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984 wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kuendana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizokuwa zimeibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican. Ushirikiano kati ya Serikali ya Italia na Vatican unalenga kulinda, kudumisha na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mkataba unaojipambanua kwa kukazia uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Nchi ya Vatican inapaswa kuendelea kuwepo, ikiwa huru katika kujiamria mambo yake yenyewe, ili kutekeleza utume wake katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili ulimwenguni kote. Marekebisho ya Mkataba wa Lateran kwa mwaka 2024 yanaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 40, kwa Serikali ya Italia na Kanisa Katoliki kwa upande mwingine kutekeleza dhamana na majukumu yake kikamilifu bila kuingiliana, yote ikiwa ni kwa ajili ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mji wa Roma ni muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa
Mji wa Roma ni muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa

Roma ni mji wa pekee unaobeba historia ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, sanjari na Maadhimisho ya Miaka Mitakatifu. Mktaba wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya ICC ambayo kimsingi ni mahakama ya kwanza ya kudumu ya kimataifa ilioundwa ili kuwafikisha mahakamani watu wanaohusika na uhalifu mkubwa ikiwa ni pamoja na: uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari, Mkataba huu ulikuwa umejadiliwa kwa takribani miaka mitatu, na ulipitishwa baada ya kikao kilichofanyika mjini Roma 17 Julai1998. Baba Mtakatifu amegusia pia Michezo ya Olimpiki tangu mwaka 1960 na Roma kama makao makuu ya Mashirika ya Kimataifa kama, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO.) Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Yesu aliye hai na mbaye pia ni Mlango wa uzima. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hili ni tukio la maisha ya kiroho linalofumbata hija, toba na wongofu wa ndani, ili kuwakirimia waamini huruma na upatanisho. Ni katika muktadha huu mji wa Roma unahusika kikamilifu kuandaa miundo mbinu itakayo wapokea na kuwahudumia wageni, watalii na mahujaji watakaotembelea mjini Roma na hivyo maadhimisho haya yatakuwa na mchango mkubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao kwa mji wa Roma. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufanya maboresho makubwa kwa huduma za usafiri kwa mji wa Roma na hususan kwa wale walioko pembezoni mwa mji; Ulinzi na Usalama. Ni katika mwelekeo huu, uongozi wa Manispaa ya Jiji la Roma na Serikali ya Italia katika ujumla wake, ni wahusika wakuu, wanaopaswa kushirikiana na Kanisa ili maadhimisho ya Jubilei hii kama ambavyo pia Serikali ya Italia inavyopaswa kushirikiana na Vatican. Haya ni mahusiano yanayosimikwa katika utu na masuala ya fedha baadaye. Baba Mtakatifu ameweka nia ya kufungua Jubilei ya Miaka 2025 kwenye Gereza!

Papa Francisko Kuzindua Jubilei ya Miaka 2025 Gerezani
Papa Francisko Kuzindua Jubilei ya Miaka 2025 Gerezani

Huduma hizi muhimu anasema Baba Mtakatifu Francisko zinapaswa kuwa ni ushuhuda wa Injili ya upendo: huduma ya ukarimu kwa wageni, watalii, wahamiaji na wakimbizi, maskini na watu pweke; wagonjwa na wafungwa, wawe kweli ni mashuhuda wa ari na mwamko huo wa Injili ya upendo. Mji wa Roma uendelee kuonesha uso wake wa kweli: Uso wa ukarimu uliotukuka. Umati mkubwa wa wahamiaji na wakimbizi; watalii na wageni unaweza kuonekana kama mzigo unaokwamisha mchakato wa ustawi na maendeleo ya mji wa Roma, lakini ikumbukwe kwamba, mji wa Roma ni wa kipekee sana ulimwenguni, kwani una mvuto wake mkuu na wajibu wake kwa Italia, Kanisa la kwa familia ya binadamu. Kila shida ya mji wa Roma inaonesha ukuu wake na kwamba, shida hizi zinaweza kuwa ni fursa ya kuchochea maendeleo: kiraia, kijamii, kiuchumi na kitamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hazina kubwa ya utamaduni na historia iliyowekwa kwenye vilima vya Roma ni heshima na mzigo wa raia wake na watawala wake, na inangojea kuthaminiwa na kuheshimiwa vya kutosha. Kuzaliwa upya kwa asili na thamani ya Roma upyaishe kuzaliwa kwa kila mtu, ishara itakayo wasilisha mabara yote kwa kujikita katika ushirikiano wenye tija na ufanisi. Baba Mtakatifu anasema, tangu mwanzo akiwa bado Padre kijana, alikuza na kuendeleza ndani mwake Ibada kwa Bikira Maria Afya ya Warumi: “Salus Populi Romani” aendelee kuulinda Mji wa Roma na wananchi wake; awakirimie na kupyaisha matumaini, Bikira Maria afya ya Warumi aendelee kuhamasisha upendo, ili hatimaye, kuthibitisha mapokeo yake bora zaidi, na hatimaye, uendelee kuwa mwanga wa ustaarabu sanjari na kukuza amani.

Papa Jiji la Roma
10 June 2024, 15:04