Wakimbizi na wahamiaji hawa baada ya kutengana na familia, ndugu na jamaa wanakutana mbele ya kuta za ubaguzi na utengano. Wakimbizi na wahamiaji hawa baada ya kutengana na familia, ndugu na jamaa wanakutana mbele ya kuta za ubaguzi na utengano.   (AFP or licensors)

Nia za Papa Francisko Kwa Mwezi Juni 2024: Wakimbizi na Wahamiaji

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Juni 2024, zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya wahamiaji na wakimbizi wanaokimbia vita, au njaa, watu wanaolazimika kufanya safari zilizojaa hatari na vurugu; ili wapate kukaribishwa na hatimaye kupata fursa mpya za maisha! Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna sababu nyingi zinazowalazimisha watu kuzikimbia au kuzihama nchi zao: Vita, Majanga asilia, Umaskini nk. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali kuta za ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi!

Wakimbizi na wahamiaji wanahatarisha maisha na utu wao
Wakimbizi na wahamiaji wanahatarisha maisha na utu wao

Baba Mtakatifu anasema Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walitambulikana kama “wanafunzi wa njia” Rej. Mdo 9:2. Mwamini ni msafiri ambaye anatambua kwamba, kamwe hajafikia lengo na hatima ya safari yake hapa duniani. Kumbe, anapaswa kujifunza kila siku, akijitahidi kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni: njia, kweli, na uzima unawaowapeleka kwa Baba wa milele. Rej. Yn 14:6. Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kufungua malango yake kwa wakimbizi na wahamiaji, kama ilivyokuwa kwa Msamaria aliyethubutu kuokoa maisha ya mtu yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi. Hata leo hii kuna watu wanaohatarisha maisha yao huko jangwani, misituni na kwenye mito, maziwa na bahari. Ni watu wanaoteswa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi, kiasi hata cha kutumbukizwa katika utumwa mamboleo. Mara nyingi hawa ni watu wanaokimbia: majanga asilia, vita pamoja na vitendo vya kigaidi kama inavyojitokeza kwa sasa. Kuna watu ambao hawawajali hata kidogo, hiki ni kielelezo cha ubinafsi, uchoyo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha moyo wa huruma na mapendo kwa sababu huu ndio utambulisho wa Mwenyezi Mungu katika mioyo ya wanadamu. Itakumbukwa kwamba, mtindo wa Mungu unasimikwa katika maneno makuu matatu: Ukaribu, Huruma na Upole na kwamba, hiki ni kielelezo makini cha ushuhuda wa Ukristo uliopelekea yule Msamaria mwema kutangaza na kushuhudia wema na upendo wa Mungu na udugu wa kibinadamu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa kama Msamaria Mwema kwa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji katika mateso yao. Ni vyema jamii ikajenga utamaduni wa kudumisha usalama barabarani, ili kusitokee watu wakaangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Hii ni changamoto ya kujizatiti kikamilifu katika mapambano ya mitandao ya biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo, kwa kuhakikisha kwamba, watu wanatumia njia halali katika kupata hifadhi.

Jengeni utamaduni wa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji
Jengeni utamaduni wa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji

Juhudi hizi zinapaswa kwenda sanjari na majadiliano ya sera za kisiasa mintarafu idadi ya watu duniani, pamoja na ukuaji wa uchumi, ili wakimbizi na wahamiaji waweze kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja ya kuwa na sera makini zinazowajibisha ili kuratibu wimbi la wakimbizi na wahamiaji linalotarajia kuongezeka maradufu kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Juni 2024, zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya wahamiaji na wakimbizi wanaokimbia vita, au njaa, watu wanaolazimika kufanya safari zilizojaa hatari na vurugu; ili wapate kukaribishwa na hatimaye kupata fursa mpya za maisha. Hawa ni watu ambao wanakuwa na hisia ya kung’olewa katika maisha na tamaduni zao asilia na wala wasitambue nafasi yao katika jamii. Katika baadhi ya nchi wakimbizi na wahamiaji wanakaribishwa na changamoto za hali ya hatari, woga na wasiwasi. Wakimbizi na wahamiaji hawa baada ya kutengana na familia, ndugu na jamaa wanajikuta mbele ya kuta za ubaguzi na utengano. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tabia na mwelekeo huu ni kinyume kabisa cha Ukristo, kwani kwa Wakristo kuwapokea na kuwakaribisha wakimbizi na wahamiaji ni sawa na kumkaribisha Kristo Yesu. Kumbe, kuna haja ya kuragibisha utamaduni wa kijamii na kisiasa utakaosimama kidete kulinda, kutetea: utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji; mwelekeo utakaosaidia kuwajumuisha katika nchi wahisan na hivyo kupata fursa ya kukua na kukomaa. Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha.

Nia Mwezi Juni
03 June 2024, 13:51