Papa akutana na Wasanii:wanaleta furaha na kuamsha fikra za kina kwa kusimulia historia za maisha halisi!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 14 Juni 2024 amekutana na ulimwengu wa wasanii mbali mbali wapatao 200 katika ukumbi wa Clementina mjini Vatican. "Ni furaha yangu kuwakaribisha nyote na kutoa shukurani zangu kwa Baraza la Utamaduni na Elimu ambao wameandaa mkutano huu" na kwamba wamemweleza kuwa kwa kiitaliano "ucheshi unaleta damu nzuri." Papa Francisko aidha amesema anavyo waheshimu sana kwani wanajieleza kupitia lugha ya vichekesho, na kejeli. Miongoni mwa wataalamu wote wanaofanya kazi katika televisheni, sinema, ukumbi wa michezo, vyombo vya habari vya kuchapisha, nyimbo na kwenye mitandao ya kijamii, wao ni miongoni mwa watu wanaopendwa zaidi, wanaotafutwa na maarufu. Hakika, Baba Mtakatifu amebainisha ni kwa sababu wao ni wazuri sana kwa kile wanachofanya, lakini pia kuna motisha nyingine ile waliyo nayo ya kukuza kipawa cha kuwafanya watu wacheke. Katikati ya habari nyingi za kutisha, tukiwa katika dharura nyingi za kijamii na hata za kibinafsi, wana uwezo wa kueneza amani na tabasamu. Wao ni miongoni mwa wachache walio na uwezo wa kuzungumza na watu wa aina zote, kutoka vizazi na asili tofauti za kiutamaduni.
Kwa njia yao wenyewe, Baba Mtakatifu amesema,wanaunganisha watu, kwa sababu kicheko kinaambukiza. Ni rahisi kucheka kwa pamoja kuliko kucheka peke yako: furaha hutufungua kwa kushiriki na ni dawa bora dhidi ya ubinafsi na kujifungia. Kicheko pia husaidia kuvunja vizuizi vya kijamii, kuunda miunganisho kati ya watu na huturuhusu kuelezea hisia na mawazo, huchangia kujenga utamaduni wa pamoja na kuunda nafasi za uhuru. Wao wanatukumbusha kuwa homo sapiens pia ni homo ludens! Kwa furaha ya kucheza na kicheko ni muhimu kwa maisha ya binadamu, kujieleza, kujifunza, na kutoa maana kwa hali halisi. Kipaji chao ni zawadi ya thamani. Pamoja na tabasamu, wanaeneza amani mioyoni mwetu na miongoni mwa wengine, wakitusaidia kushinda magumu na kukabiliana na mikali ya kila siku. hutusaidia kupata ahueni katika kejeli na kupitia maisha kwa ucheshi. Papa anapenda awaombee kila siku kwa maneno ya Mtakatifu Thomas More: “Nipe, Ee Bwana, ucheshi mzuri.” Papa ameongeza kusema: "Ninaomba neema hii kwa kila siku maana inanisaidia kuyaendea mambo kwa roho sahihi."
Baba Mtakatifu amewasifu akisema kuwa pia wanafanikiwa kuleta muujiza mwingine na huo ni kufanikiwa kuwafanya watu watabasamu hata wakati wa kushughulikia shida na matukio, makubwa na madogo. Wanakemea matumizi mabaya ya madaraka; wanatoa sauti kwa hali zilizosahaulika; wanaangazia unyanyasaji; wanaonesha tabia isiyofaa. Wanafanya hivi bila kueneza kengele au hofu, wasiwasi au woga, kama aina nyingine za mawasiliano zinavyoelekea kufanya; wanawaamsha watu kufikiri kwa kina kwa kuwafanya wacheke na kutabasamu. Wanafanya hivi kwa kusimulia historia za maisha halisi, kusimulia ukweli kutoka katika mtazamo wao wa kipekee; na kwa njia hii, wanazungumza na watu kuhusu matatizo, makubwa na madogo.
Baba Mtakatifu Francisko kulingana na Biblia, mwanzoni mwa ulimwengu, wakati kila kitu kilipokuwa kikiumbwa, hekima ya kimungu ilitumia namna yao ya usanii kwa manufaa ya Mungu mwenyewe, mtazamaji wa kwanza wa historia anayependezwa na wana wa binadamu”(Mit 8:30-31). Baba Mtakatifu amesisitiza hili kwamba: wanapofanikiwa kuteka tabasamu huku wakijua kutoka kwenye midomo ya hata mtazamaji mmoja, pia wanamfanya Mungu atabasamu. Papa amewaeleza wasanii kuwa wanajua jinsi ya kufikiria na kuzungumza kwa ucheshi kwa aina na mitindo tofauti; na katika kila hali lugha ya ucheshi inafaa kwa kuelewa na "kuhisi" asili ya mwanadamu. Ucheshi hauudhi, hauwafedheheshi, au kuwashusha watu kulingana na kasoro zao. Ingawa mawasiliano leo hii mara nyingi huzua migogoro, wanajua jinsi ya kuleta pamoja mambo tofauti na wakati mwingine kinyume. Ni kiasi gani tunahitaji kujifunza kutoka kwao! Kicheko cha ucheshi kamwe sio "dhidi" ya mtu yeyote, lakini daima ni pamoja, yenye kusudi, inaleta uwazi, huruma na upole.
Papa amekumbuka historia katika kitabu cha Mwanzo wakati Mungu aliahidi Ibrahimu kwamba ndani ya mwaka mmoja atakuwa na mtoto. Yeye na mkewe Sara walikuwa wazee na hawakuwa na mtoto. Sarah alisikiliza na kucheka kimoyomoyo. Ibrahimu lazima alifanya vivyo hivyo. Hata hivyo, Sara akapata mimba na kuzaa mtoto katika uzee wake, kwa wakati ambao Mungu alikuwa ameweka. Sara alisema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atanicheka” (Mw 21:6). Ndiyo maana wakamwita mwana wao Isaka, maana yake, “anacheka”. Je, tunaweza kumcheka Mungu? Bila shaka, tunaweza, kama vile tunavyocheza na kufanya mzaha na watu tunaowapenda. Hekima ya Kiyahudi na mapokeo ya fasihi ni bwana katika hili! Inawezekana kufanya hivyo bila kuudhi hisia za kidini za waamini, hasa maskini. Baba Mtakatifu amesema Mungu awabariki na sanaa yao. Waendelee kuwachangamsha watu, hasa wale ambao wana wakati mgumu zaidi wa kuyatazama maisha kwa matumaini. Watusaidie, kwa tabasamu, kuona ukweli pamoja na kinzani zake, na kuota ulimwengu ulio bora! Kwa hisia za dhati, amewabariki; na ameomba wamwombee tafadhali.