Papa atoa wito wa usitishaji mauaji,vurugu na ghasia huko Congo DRC
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, alikumbuka tukio la kutangazwa Mwenyeheri huko huko Krakow nchini Poland, kwa Michele Rapacz, Padre na Mfiadini na kwamba “alikuwa mchungaji kulingana na moyo wa Kristo, shahidi mwaminifu na mkarimu wa Injili ambaye alipata mateso ya Wanazi na ya Kisoviet na akajibu kwa zawadi ya maisha.” Kwa njia hiyo Papa ameomba umati umpigie makofi Mwenyeheri mpya!...
Baba Mtakatifu aidha amebainisha kuwa:“Habari chungu nzima zinaendelea kuwasili kuhusu mapigano na mauaji katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. “ Kwa njia hiyo Papa amesema “Ninatoa ombi langu kwa mamlaka za kitaifa na Jumuiya ya kimataifa kufanya kila linalowezekana kukomesha ghasia na kulinda maisha ya raia. Miongoni mwa waathriwa, wengi ni Wakristo waliouawa kwa chuki (odium fidei.) Wao ni wafiadini. Sadaka yao ni mbegu inayoota na kuzaa matunda, na inatufundisha kushuhudia Injili kwa ujasiri na uthabiti.”
Na wakati huo huo Papa amesema: “Tusiache kuombea amani Ukraine, Nchi Takatifu, Sudan, Myanmar na popote pale palipo na vita. Papa amewageukiwa mahujai kutoka Roma.Kwa namna ya pekee amewasalimu waamini kutoka Lebanoni, Misri na Hispania; wanafunzi wa “London Oratory School”; wale wa Jimbo laa Opole huko Poland na wale wa Budapest-Albertfalva; washiriki katika Jukwaa la Walei la Ulaya, lenye mada: “Imani, sanaa na sinodi”; na kundi la akina mama kutoka Jumuiya ya Kikatoliki ya Congo ya Roma. Kwa wao ameongeza kusema Papa: “akina mama hawa wanaimba vizuri: ningependa kuwasikia wakiimba tena...”
Baba Mtakatifu aidha amewasalimu waamini wa Carini, Catania, Siracusa na Messina; watoto Kumunio ya Kwanza na Kipaimara wa Mestrino, wanakipaimawa wa Castelsardo (Sassari), wa Bolgare (Bergamo) na wa Camin (Padua); na hatimaye wazo la shukrani kwa wafadhili wa damu, ambao wameadhimisha Siku yao ya Kitaifa. Na hatimaye amewasalimu wote na kuwatakia Dominika njema. Tafadhali wasisahau kumuombea. Mlo Mwema, mchana nzuri na kwaheri ya kukuona!