Papa Francisko Ametoa Zawadi ya Gari la Wagonjwa Kwa Ukraine
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo anasema, Baba Mtakatifu Francisko ametoa gari la tatu kwa ajili ya wagonjwa nchini Ukraine, kielelezo cha mshikamano wa upendo na watu wa Mungu nchini Ukraine ambao kwa kiasi kikubwa wanaendelea kuathirika kwa vita. Kardinali Konrad Krajewski pamoja na gari hii, atawapelekea pia kiasi kikubwa cha dawa kilichotolewa na Duka la Dawa la Vatican kwa kushirikiana na Duka la Dawa la Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma. Hii ni mara ya nane kwa Kardinali Konrad Krajewski, kuendesha gari hadi nchini Ukraine. Hospitali ya Mkoa wa Ternol, nchini Ukraine, kila siku inapokea majeruhi wa vita.
Ni katika muktadha huu, gari hili la wagonjwa litakuwa ni msaada mkubwa kwa ajili ya huduma kwa majeruhi wa vita. Hii ni fursa pia ya kufungua Kituo cha Mazoezi cha Mtakatifu Yohane Paulo II, kilichofanyiwa ukarabati mkubwa huko Vinystia, kwenye Jimbo Katoliki la Kamyanets- Podilskyy. Hiki ni kituo ambacho kinatokana na juhudi za Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya huduma kwa waathirika wote wa Vita. Hawa ni askari pamoja na familia zao. Huu ni msaada kutoka kwa Shirika la Kipapa la Kanisa Hitaji. Hatima ya yote haya ni sehemu ya mchakato wa huruma, ili hatimaye ifunhue njia ya neema ya upatanisho.