Papa Apokea Hati za Utambulisho Kutoka kwa Mabalozi: Tanzania, Zambia, Burundi..
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Dhana ya diplomasia ya Vatican inafumbatwa katika amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo fungamani! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu, ili kuweza kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo. Mataifa yatambue kwamba, yanategemeana na kukamilishana na kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Kwa njia, hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbalimbali. Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kidiplomasia na uhusiano wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa anakazia kwa namna ya pekee: Mosi, umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu wa kibinadamu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.
Vatican inakazia: ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita, mipasuko ya kijamii, kinzani na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia! Lengo la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi. Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani! Kanisa linapenda kudumisha mchakato wa haki, amani, utulivu na maridhiano kwa kuzimisha moto wa machafuko, kinzani na vita kwa maji ya baraka, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 8 Juni 2024 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wa: Ethiopia, Zambia, Tanzania, Burundi, Qatar na Mauritania. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amejikita katika mambo makuu matatu: familia, matumaini na amani. Mababa wa Kanisa wanasema, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, udugu wa kibinadamu, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anasema, kimsingi, diplomasia haina budi kujikita katika kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; ustawi na maendeleo ya watu wengi. Baba Mtakatifu anawahasa wanadiplomasia pamoja na nchi zao, kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda; Ustawi na maendeleo ya wote; kulinda haki msingi za binadamu; utu na heshima ya wote; kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu na ushirikiano.
Inasikitisha kuona kwamba, leo hii familia nyingi zimesambaratika kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kama jinsi hali inavyojionesha huko Sudan, Ukraine pamoja na Ukanda wa Gaza. Na matokeo yake ni uhaba mkubwa wa makazi, maji, chakula na huduma ya tiba. Kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao; kuna ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na makazi hata ndani ya nchi zao wenyewe; biashara haramu binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo; athari za mabadiliko ya tabianchi; mambo yote haya yana athari kubwa kwa vijana wa kizazi kipya. Ikiwa kweli Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata suluhu ya matatizo na changamoto hizi zote haina budi kujikita katika majadiliano yanaosimikwa katika ukweli na uwazi pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Jumuiya ya Kimataifa itambue ni urithi gani ambao wangependa kuwaachia watoto wao kwa siku za usoni?
Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Katika Tamko hili, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Matumaini katika Neno la Mungu ili kuamini, kutumaini, kupenda na kuvumilia kwa kutambua kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini. Baba Mtakatifu anawataka Mabalozi hawa wapya kuwa ni alama ya matumaini, na wajenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu na kwamba, ujenzi wa urafiki wa kijamii unawezekana kwa kujikita katika ujenzi wa jumuiya inayosimikwa katika utu na udugu na kwamba, kwa njia hii amani inawezekana kabisa.
Mtakatifu Yohane XXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuondoa woga na hali ya kutojali, ili kujenga hali ya kuheshimiana, ili kukoleza maelewano, tayari kujifunga kibwebwe kupambana na ukosefu wa haki, ubaguzi, umaskini, ukosefu wa usawa unaowatendea vijana wa kizazi kipya, ili hatimaye, Mabalozi hawa wapya wawe ni vyombo na wajenzi wa amani Rej. Mt 5:9. Baba Mtakatifu amewahakikishia Mabalozi wapya utayari na ushirikiano kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao!
Balozi Hassan Idd Mwamweta-Tanzania.
Balozi Macenje Mazoka- Zambia.
Balozi Annonciata Sendazirasa- Burundi.
Balozi Mahlet Hailu Guadey - Ethiopia.
Balozi Mohamed Yahya Teiss - Mauritania.
Balozi Asma Naji Hussain Al-Amiri - Qatar.