Misaada bado inahitajika nchini Ukraine. Misaada bado inahitajika nchini Ukraine.  (Credit Caritas Polonia)

Papa Francisko atuma dawa za dharura nchini Ukraine

Mchango muhimu uliofika Vatican uliruhusu dawa nyingi za huduma ya kwanza kutumwa katika nchi iliyoharibiwa na vita.Hii ni ishara mpya ya umakini kwa wale wanaokumbwa na matokeo ya mzozo wa vita kama vile Ukraine.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika moyo wa Papa Francisko daima kumekuwa na kuteswa kwa nchi ya Ukraine, ambayo anaelekeza mawazo yake kila mara huku akitualika kusali kwa ajili ya amani. Tangu mwanzo wa vita kumekuwa na ishara nyingi za ukaribu na mshikamano: kama vile kuanzia na ununuzi wa jenereta hadi kupeleka chakula, nguo za joto na mablanketi. Kufuatia kile kilichofanyika siku za nyuma, mnamo Jumamosi iliyopita tarehe Mosi Juni 2024, Papa  Francisko alituma dawa za huduma ya kwanza nchini humo, hasa zilizokusudiwa kwa ajili ya majeruhi wa vita, zenye thamani ya euro laki moja, ambapo ni matokeo ya mchango muhimu uliopokelewa na  Shirika la Misaada ya Kitume kwa njia ya Ubalozi wa Vatican.

Hii ni njia ya kuwa karibu na watu katika shida kubwa, iliyojaribiwa na zaidi ya miaka miwili ya migogoro. Tahadhari kwa wale walio pembezoni ni utume ambao Papa amewakabidhi kwa Baraza la Kipapa  kwa ajili ya Huduma ya Upendo hivyo, katika Juma hili kuna pia  huduma ya upimaji wa afya iliyoanzishwa mjini Vatican kwa wale ambao wanahitaji msaada huo. Hawa ni karibu watu 50 ambao hawawezi kufikia Mfumo wa Kitaifa wa Afya  Italia na ambao, mara nyingi, hawajui kuwa wanaweza kuwa hatarini kwao wenyewe na kwa wengine.

Kuzuia saratani ya matiti

Msisitizo pia ni kuzuia, hasa wanawake wanaoishi pembezoni, bila huduma ya afya na kwa kawaida hufuatwa na kliniki ya “Madre di Misericordia yaani Mama wa Huruma ” na Zahanati ya Mtakatifu  Marta. Mnamo tarehe 18 Aprili iliyopita, gari kutoka Komen Italia, ya  Chama kinachojishughulisha na kinga na mapambano dhidi ya saratani ya matiti, ambacho kimekuwa katika harambee kila mara na Taasisi ya Mfuko wa Hospitali ya Agostino Gemelli (IRCCS) na Kisiwa cha Gemelli  Tiberina kimewapa takribani wanawake arobaini maskini fursa ya kunufaika na vipimo vya uchunguzi kwa ajili ya kujikinga na saratani ya matiti kwa kutumia vipimo vya ultrasound ya matiti. Uzoefu huo, ambao hudumu kila baada ya miezi miwili, pia unaarudiwa mwezi huu Juni. Kwa upande wa Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo amebainisha kuwa, “mipango inayotekelezwa ni ishara ya Injili inayokaribia, inayowaangalia wale wanaoteseka bila kuangalia upande mwingine.”

Msaada wa Papa kwa Ukraine
04 June 2024, 15:24