Wanachama wa Chama cha Kitume cha  “Circolo San Pietro”, Jumatatu, tarehe 24 Juni 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Wanachama wa Chama cha Kitume cha “Circolo San Pietro”, Jumatatu, tarehe 24 Juni 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tangazeni Na Kushuhudia Injili ya Huduma ya Upendo Kwa Maskini

Wanachama wa Chama cha Kitume cha “Circolo San Pietro" wamekutana na kuzungumza na Papa Francisko. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya huduma ya maskini wa Roma kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu; wajitahidi kuwarithisha vijana wa kizazi kipya amana, utajiri na mang’amuzi haya. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo iwe ni fursa ya kumwilisha Injili ya upendo kwa mahujaji, wageni na maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Kitume cha “Circolo San Pietro” kilianzishwa na kikundi cha vijana wakatoliki kunako mwaka 1869, chini ya uongozi wa Kardinali Iacobini, kielelezo makini cha ushuhuda wa Injili ya upendo katika huduma na uaminifu wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Mwenyeheri Papa Pius IX akabariki juhudi hizi na kuwakabidhi vijana wa Roma utume wa kuwahudumia maskini wa Jimbo kuu la Roma, kiasi cha kubatizwa na kuitwa “Supu ya Papa.” Karama na utume wa Chama hiki unafumbatwa katika kauli mbiu yake “Sala, Matendo na Sadaka. Chama cha “Circolo San Pietro” ni sehemu ya historia ya mji wa Roma, kwani kimeshuhudia madhara ya Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia. Katika nyakati zote hizi, Chama hiki kimekuwa ni faraja kwa maskini; Injili ya upendo inayomwilishwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu.

Umuhimu wa kumwilisha Injili ya huduma ya upendo kwa maskini
Umuhimu wa kumwilisha Injili ya huduma ya upendo kwa maskini

Wanachama wa Chama cha Kitume cha  “Circolo San Pietro”, Jumatatu, tarehe 24 Juni 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya huduma ya maskini wa Roma kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu; wajitahidi kuwarithisha vijana wa kizazi kipya amana, utajiri na mang’amuzi haya. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo iwe ni fursa ya kumwilisha Injili ya upendo kwa mahujaji na wageni watakaofika mjini Roma. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa Chama cha Kitume cha “Circolo San Pietro” kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kwa maskini wa Roma, utume wanaoutekeleza kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Kanisa katika ujumla wake.

Injili ya upendo kwa mahujaji na wageni
Injili ya upendo kwa mahujaji na wageni

Kumbe, ni vyema ikiwa kama watazamisha mizizi ya amana na utajiri huu, kwa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya. Huu ni urithi wa imani na upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu. Vijana kupitia kwa wazee wajifunze kuwahudumia maskini kwa ari na moyo mkuu. Kama ilivyokuwa kwa Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati, hivi karibuni atatangazwa kuwa Mtakatifu, aliye bahatika kutoka katika familia inayojiweza, lakini akajichanganya na watu wengine kwa ajili ya huduma kwa maskini, vivyo hivyo inavyopaswa kuwa kwa vijana wa kizazi kipya. Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati alitangaza na kushuhudia upendo wa Mungu ambao ni kazi ya Roho Mtakatifu. Huu ni upendo kwa ajili ya Kristo Yesu pamoja na ndugu majirani. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.”

Rithisheni amana na utajiri huu kwa vijana wa kizazi kipya
Rithisheni amana na utajiri huu kwa vijana wa kizazi kipya

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa sasa ujenzi wa miundo mbinu unaendelea sehemu mbalimbali za Jiji la Roma, changamoto na mwaliko wa kumwilisha Injili ya upendo kwa mahujaji na watalii watakaofika mjini Roma. Injili ya huduma isimikwe katika: huduma makini; utu, heshima na haki msingi za binadamu; yote haya yafanyike sirini bila ya “kupiga baragumu.” Uwepo wao, katika huduma, umwilishwe katika huduma makini kwa maskini ambao ni amana na utajiri wa Kanisa. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewaaminisha wajumbe wa Chama cha Kitume cha “Circolo San Pietro” chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani.”

Mtakatifu Petro
24 June 2024, 15:50