Papa:Tunahitaji Kanisa na jamii isiyomtenga mtu na bila kumwona najisi!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Dominika ya 13 ya Mwaka B, tarehe 30 Juni 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana kwa Mahujaji na waamini waliofika kwa wingi katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Akianza tafakari yake kabla ya sala hiyo Papa amesema “Injili ya liturujia ya leo inatuambia juu ya miujiza miwili ambayo inaonekana kushikamana na kila mmoja. Yesu akiwa njiani kuelekea nyumbani kwa Yairo, mmoja wa viongozi wa sinagogi ambaye binti yake ni mgonjwa sana, mwanamke anayesumbuliwa na damu aligusa vazi lake njiani. Aliacha amemponya. Wakati huohuo, tunaambiwa kwamba binti Yairo alikuwa tayari amekufa, lakini Yesu hakusimama. Alifika nyumbani, na kuingia katika chumba cha binti huyo na anamshika mkono, na kumwinua, na kumfufua (Mk 5:21-43).
Katika miujiza miwili, Papa ameffanua kuwa "mmoja ni uponyaji na mwingine ufufuo." Papa aidha amesema: “uponyaji huu wa aina mbili hupo katika sehemu moja. Zote mbili zilitokea kwa kuwasiliana kimwili. Kiukweli, mwanamke huyo aligusa vazi la Yesu, na Yesu alimshika Binti kwa mkono. Kwa nini mawasiliano haya ya kimwili ni muhimu? Papa ameuliza na kujibu kuwa “Ni kwa sababu wanawake hao wawili walionekana kuwa wachafu na wasiweza kwa hiyo, kuguswa kimwili, kwani mmoja ni kwa sababu anapoteza damu na mwingine kwa sababu amekufa. Hata hivyo, Yesu alijiruhusu mwenyewe kugusa na hakugopa kugusa. Hata kabla ya kufanya uponyaji wa kimwili, Yeye alipinga imani ya kidini ya uwongo kwamba Mungu huwatenganisha walio safi, akiwaweka upande mmoja, kutoka kwa wale wasio safi hadi mwingine. Badala yake, Mungu hafanyi aina hiyo ya utenganisho, kwa sababu sisi sote ni watoto Wake. Uchafu hautokani na chakula, magonjwa, au hata kifo; uchafu hutoka katika moyo mchafu.
Baba Mtakatifu ameomba tujifunze hili somo kwamba: “mbele ya mateso ya kimwili na ya kiroho, ya majeraha ambayo roho zetu hubeba, juu ya hali zinazotuponda, na hata katika uso wa dhambi, Mungu hatuweki mbali. Mungu hatuonei haya; Mungu hatuhukumu. Kinyume chake, Yeye hukaribia ili kujiruhusu mwenyewe kuguswa na kutugusa, na Yeye hutufufua daima kutoka katika wafu. Daima anatushika mkono na kusema: binti, mwana, inuka! (rej. Mk 5:41). Tembea mbele; jitahidi mbele! Papa ameongeza kwamba unaweza kusema kuwa: “Bwana mimi ni mwenye dhambi”, lakini Yeye atakujibu: “Jitahidi kwenda mbele; nimekuwa mdhambi kwa ajili yako, ili nikuokoe” na wewe utasema: “Lakini wewe, Bwana, si mwenye dhambi.” Yeye atakujibu: “Hapana, lakini nimevumilia matokeo yote ya dhambi ili kukuokoa.” Kwa hiyo Papa amesema na hii ni nzuri!
Baba Mtakatifu kwa njia hiyo amesema: “Hebu basi tuweke sura ambayo Yesu anatupatia mioyoni mwetu. Mungu ndiye anayekushika mkono na kukuinua tena. Ni yeye anayejiruhusu kuguswa na maumivu yako na kukugusa ili kukuponya na kukupa uzima tena. Habagui yeyote kwa sababu anampenda kila mtu. Hivyo, tunaweza kujiuliza: je, tunaamini kwamba Mungu yuko hivi? Je, tunajiruhusu kuguswa na Bwana, na Neno Lake, na upendo Wake? Je, tunahusiana na kaka na dada zetu kwa kushika mkono ili kuwainua, au je, tunaweka mbali na kuwataja watu kulingana na mapendekezo na mapenzi yetu? Tunawabandika watu lebo.”
Papa Francisko kwa kukazia zaidi ameuliza swali tena :Je, Mungu, Bwana Yesu, anawataja watu? Kila mtu ajibu swali hili. Je, Mungu huwataja watu? Na je, ninaishi kwa kuweka watu lebo kila mara? Kwa hiyo tuutazame moyo wa Mungu, ili Kanisa na jamii isimtenge wala kumchukulia mtu yeyote kuwa ni “mchafu, najisi” ili kila mtu, pamoja na maisha yake ya zamani, apokelewe na kupendwa bila alama, chuki au vivumishi. Kwa kuhitimisha tafakari amesema “Tuombe kwa njia ya Bikira Mtakatifu. Yeye ambaye ni Mama wa huruma atuombee sisi na dunia nzima.”