Papa:katika Jubilei deni la nchi maskini linapaswa kufutwa au kupunguzwa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumatano asubuhi sana tarehe 5 Juni 2024 akikutana mjini Vatican na washiriki wa Mkutano wenye mada (Debt Crisis in the Global South) yaani Mgogoro wa Madeni Kusini mwa Ulimwengu ameanza na kuwatania kuhusu kuwaamsha mapema . Kwa hiyo ameanza kumsalimia Kardinali Turkson, Chansela wa Chuo cha Kipapa cha Sayansi, na wote wanaoshiriki katika mkutano wa “Mgogoro wa Madeni Kusini mwa Ulimwengu” unaolenga kuanzisha mazungumzo kuhusu utekelezaji wa sera zinazosaidia kutatua tatizo la madeni linalolikabili mataifa na huathiri nchi nyingi kusini mwa dunia, na kuathiri mamilioni ya familia na watu duniani kote.
Baada ya utandawazi kusimamiwa vibaya tunakabiliwa na shida ya deni
Watu hawahitaji ufadhili wowote tu, bali ni ule ambao unaashiria tu uwajibikaji wa pamoja kati ya wale wanaoipokea na wale wanaoitoa. Faida ambayo inaweza kuleta kwa kampuni inategemea hali yake, jinsi inavyotumiwa na maeneo ambayo migogoro ya madeni inaweza kutatuliwa. Baada ya utandawazi kusimamiwa vibaya, baada ya janga na vita, Baba Mtakatifu amesema: “tunajikuta tukikabiliwa na shida ya deni ambalo linaathiri sana nchi za ulimwengu wa kusini, likizalisha taabu na uchungu, na kuwanyima mamilioni ya watu uwezekano wa mustakabali wenye heshima. Kwa hiyo, hakuna serikali inayoweza kuwataka watu wake wapate kunyimwa mambo yasiyopatana na utu wa kibinadamu. Ili kujaribu kuvunja mzunguko wa ufadhili wa madeni, kuundwa kwa utaratibu wa kimataifa kungekuwa muhimu, kwa kuzingatia mshikamano na maelewano kati ya watu, ambayo inazingatia umuhimu wa kimataifa wa tatizo na athari zake za kiuchumi, kifedha na kijamii. Kutokuwepo kwa utaratibu huu kunapendelea “kila mtu kwa nafsi yake ambapo dhaifu daima hupoteza.
Misingi ya haki na mshikamano inapelekea kupata suluhisho
Sambamba na mafundisho ya watangulizi wa Baba Mtakatifu Papa amependa kusisitiza kwamba misingi ya haki na mshikamano ndiyo inayopelekea kupata suluhisho. Katika njia hii ni muhimu kufanya kazi kwa nia njema na ukweli, kwa kufuata kanuni za kimataifa za maadili, na kanuni za thamani ya maadili, ambayo inalinda mazungumzo. Kwa hivyo, hebu tufikirie usanifu mpya wa kimataifa wa kifedha ambao ni wa ujasiri na wa ubunifu.
Desturi ya kizamani ya kiyahudi ya kusamehe madeni
Katika Jubilei ya mwaka wa 2000, Mtakatifu Yohane Paulo II aliona kwamba suala la deni la nje “si hali ya kiuchumi tu, bali linaathiri kanuni za kimsingi za kimaadili na lazima lipate nafasi katika sheria za kimataifa “na kutambua kwamba “Jubile inaweza kuunda fursa inayofaa kwa ishara za nia njema [...], kusamehe madeni au angalau kuyapunguza [...] kwa manufaa ya wote” (Katekekesi 3 Novemba 1999). “Na hii ilikuwa desturi ya Wayahudi, katika mwaka wa Jubilei madeni yalisamehewa.” Papa amesema "Ningependa kurejea mwito huu wa kinabii, leo wa dharura zaidi kuliko wakati mwingine wowote, nikikumbuka kwamba deni la kiikolojia na deni la nje ni pande mbili za sarafu moja ambayo huweka rehani siku zijazo."
Jubilei 2025 inatualika kufungua akili na mioyo ili kufungua vifundo vya vitanzi vinavyo nyonga maisha
Kwa sababu hiyo Baba Mtakatifu amsema " Wapendwa, Mwaka Mtakatifu wa 2025 tunaouendea unatualika tufungue akili na mioyo yetu ili tuweze kufungua mafundo ya vitanzi hivyo vinavyonga maisha ya sasa, bila kusahau kwamba sisi ni walinzi na wasimamizi tu na sio mabwana. Papa ametoa mwaliko wa kuota ndoto na kutenda pamoja katika ujenzi wa uwajibikaji wa nyumba yetu ya kawaida ya pamoja; “hakuna mtu anayeweza kuishi huko akiwa na dhamiri safi wakati anajua kwamba karibu nao kuna umati wa kaka na dada wenye njaa ambao pia wamezama katika kutengwa na jamii na mazingira magumu.” Kuruhusu hili litokee ni dhambi, dhambi ya mwanadamu, hata kama mtu hana imani, ni dhambi ya kijamii.” Kwa hiyo wanachofanya ni muhimu, Papa amewaombea na Mungu awabariki. Na pia ameomba wasisahau kumuombea. Na kwa kila mtu ameomba Bwana awabariki. Amina.Amehitimisha.