Papa kwa Wafocolari:ushuhuda ni chanzo cha furaha na faraja
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amekutana na washiriki wa Mkutano wa Baraza la Kidini wa Harakati ya Wafocolari , mjini Vatican tarehe 3 Juni 2024. Katika hotuba yake Baba Mtakatifu ameanza na salamu kwa Rais wa Harakati ya Wafocolari ambaye amempatia pole kwa matukio yanayoendelea katika Nchi yake, na kuwakaribisha kwa moyo mkunjufu washiriki wote katika Mkutano huu wa Dini Mbalimbali. Ametoa shukrani zake kwa uvumilivu ambao Kazi ya Maria inaendelea na safari iliyoanza na Chiara Lubich, kukuza umoja na watu wa dini zisizo za Kikristo wanaoshiriki hali ya kiroho ya umoja. Hili ni tukio linalohuishwa na Roho Mtakatifu, lenye mizizi, na tunaweza kusema, katika moyo wa Kristo, katika kiu yake ya upendo, ushirika na udugu.
Hakika, ni Roho ambaye hufungua njia za mazungumzo na kukutana, wakati mwingine njia za kushangaza. Hii ilitokea zaidi ya miaka hamsini iliyopita nchini Algeria, wakati jumuiya ya Waislamu wote wanaofuata Harakati ilipozaliwa ilifanyika pia na mikutano ya Chiara Lubich na viongozi wa dini mbalimbali: Wabudha, Waislamu, Wahindu, Wayahudi, Masingasinga, na wengineo. Mazungumzo haya yamestawi kwa muda, kama inavyothibitishwa na uwepo wao hapo. Msingi wa uzoefu huu ni upendo wa Mungu unaooneshwa kupitia kupendana, kusikilizana, kuaminiana, ukarimu na kufahamiana, wakati wote huo kuheshimu kikamilifu utambulisho wa kila mmoja wao. Baada ya muda, urafiki na ushirikiano umekua katika kutafuta kujibu kwa pamoja kilio cha maskini, katika kutunza uumbaji na kufanya kazi kwa amani. Kupitia safari hiyo Baba Mtaklatifu Francisko amedhibitisha kuwa, baadhi ya kaka na dada wasio Wakristo wameshiriki katika hali ya kiroho ya Kazi ya Maria, au katika baadhi ya sifa zake, na kuishi kulingana nazo miongoni mwa watu wao wenyewe.
Pamoja na wanaume na wanawake hawa, wanavuka mazungumzo, wanajisikia kama kaka na dada, wanashiriki ndoto ya ulimwengu uliounganishwa zaidi, katika maelewano ya utofauti. Baba Mtakatifu amesema ushuhuda wao ni chanzo cha furaha na faraja, hasa wakati huu wa migogoro, ambapo mara nyingi dini hutumiwa vibaya ili kuchochea migawanyiko. Hakika, mazungumzo baina ya dini “ni hali ya lazima kwa amani duniani, na hivyo ni wajibu kwa Wakristo na jumuiya nyingine za kidini” (Evangelii Gaudium, 250). Papa Francisko amewatia moyo na ili wasonge mbele, daima wakiwa wazi na utulivu kwa utendaji wa Roho Mtakatifu. Ametoa shukrani zake za dhati kwa ziara yao! Mungu wa amani awabariki na Mama Yetu awalinde. Na wasisahau kumwombea.