Papa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu:Kuwa mkweli kwa imani yao!
Na Deborah Castellano Lubov na Angella Rwezaula – Vatican.
Daima mshikilie imani yenu hata mkijaribiwa na vuguvu, ni kuishi kwa imani kwa sababu wengine wanawatesa, shikilieni utambulisho wenu na muwe hodari kama wafiadini Wakristo walioteswa. Huo ni ujumbe uliotoka moyoni mwa Baba Mtakatifu Francisko katika maneno aliyozungumza na wanafunzi wa Vyuo Vikuu kutoka Asia. Walikuwa wakishiriki katika tukio lenye kuongozwa na mada: “Kujenga Madaraja katika Asia ya Pasifiki,” Alhamisi tarehe 20 Juni 2024, lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Loyola, Chicago na Tume ya Kipapa ya Amerika Kusini.
Baba Mtakatifu alishiriki kupitia mkondo wa moja kwa moja.
Chuo Kikuu cha Loyola cha Chicago kilizindua Mpango wa Kujenga Madaraja (BBI), mfululizo wa matukio unaozingatia wanafunzi na Vyuo vikuu, baada ya kuongozwa na wito wa Papa Francisko wa sinodi. Mkutano wa kwanza ulifanyika mnamo Februari 2022, wenye mada: “Kujenga Madaraja, Kaskazini-Kusini.” Wa pili, “Kujenga Madaraja katika Afrika,” uliolfanyika mwezi Novemba mwaka huo huo na ulihusisha wanafunzi kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa njia hiyo hata tukio hili limefuata mtindo huo lakini kwa kukaribisha ushiriki wa Papa.
Miongoni mwa wale walioshiriki katika mkutano huu wa sinodi ya hivi karibuni zaidi walikuwa wanafunzi wa vyuo vikuu, wanaofuatilia nyanja mbalimbali, kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Manila Ufilipino; Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Brisbane ,Australia; Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Fu Jen, Taipei, Taiwan; Chuo Kikuu cha Sogang Seoul, Korea Kusini; Chuo Kikuu cha Sophia-Tokyo, Japan; Chuo Kikuu cha Sanata Dharma(Yogyakarta, Indonesia). Wanafunzi pia walishiriki kutoka Singapore, Timor Leste, na Papua New Guinea, mataifa ambayo Baba Mtakatifu anatazamiwa hivi karibuni kutembelea wakati wa Ziara yake ya Kitume Barazani Asia na Oceania mwezi Septemba 2024.
Papa Francisko: Waombe wengine wawasaidie katika mazingira magumu yenu
Baba Mtakatifu alijiunga na mkutano huo, akiwasalimia kwa uchangamfu waliokuwepo kwa lugha ya Kihispania, na kuomba msamaha kwa kuchelewa kidogo kutokana na wingi wa ratiba katika ajenda yake. Vikundi vya wanafunzi vilitambulishwa kwa Papa na kutoa tafakari, ambayo Baba Mtakatifu, kwa kurudi, alitoa ushauri uu ya wasiwasi, na mapendekezo yake. Baba Mtakatifu alizungumza na kundi la kwanza kuhusu kujisikia kuwa wa jamii, na jinsi 'mali yetu' inavyoongeza usalama wetu ndani yetu na utu wetu wa kibinadamu. Mambo haya yote, alibainisha, yanatuokoa kutokana na mazingira magumu, kwa sababu leo hii vijana wako katika mazingira magumu sana. Ni lazima kila mara tutetee hisia hii ya kuhusishwa ili kuepusha mazingira magumu. Tazameni hatari mahali mlipo na muombe mtu awasaidie,” Papa aliwashauri vijana.
'Ukuu wa wanawake haupaswi kusahaulika'
Papa pia akiendelea alijadili afya ya akili, ubaguzi, unyanyapaa, na utambulisho na kutoa wito wa kutoa ushahidi na kuendelea. “Zingatieni kuwa na utambulisho wenu” alisema huku akiwahimiza wote waliohudhuria kila wakati kushirikiana na kudumisha umoja. Papa alikashifu unyanyapaa wote unaodhalilisha utu wa mtu. Alilaumu kwamba wakati fulani wanawake wanachukuliwa kuwa raia wa daraja la pili, jambo ambalo, alikumbusha kila mtu, kuwa si kweli. “Ukuu wa wanawake haupaswi kusahaulika. Wanawake ni bora kuliko wanaume kwa ufahamu wao na uwezo wao wa kujenga jamii,” alisema, huku akipongeza sifa na umahiri maalum kwa wanawake.
Papa kadhalika alitoa wito kwa wanafunzi kuonesha ukaribu na upendo kwa wengine, na kamwe bila kuwatenga. Akikumbuka maneno ya mwanafunzi aliyezungumzia jinsia akitaja pia kiwango cha juu cha VVU nchini Ufilipino, Papa alisema, “Lazima tuhakikishe kwamba huduma ya afya iko tayari kutibu na kusaidia watu wote, bila kutengwa. Papa alizungumzia elimu yenye ufanisi, ambayo, kwa maoni yake, inahitaji “kuelimisha na kuratibu mioyo, akili, na mikono yetu. Hivi ndivyo tunavyopaswa kuwaelimisha vijana,” alisema, akibainisha kwamba nguvu hii lazima isisahaulike kamwe.
Mioyo iliyounganishwa na maombi na wengine
Papa pia alikiri jinsi inavyoweza kuwa changamoto kwa vijana Wakristo kushiriki na kuwa katika jamii. Kwa kuzingatia ukweli huu, aliwahimiza kushikamana na imani yao, na kuweka mioyo yao kushikamana na sala. Kwa kufanya hivyo, kutasaidia katika suala hili na kukuwezesha daima, kwa ufanisi zaidi, kushirikiana na wengine,” Papa alisema. Baba Mtakatifu akiendelea na mazungumzo na vijana hao pia alizungumzia ukweli kwamba, katika nyakati fulani vijana hudhihakiwa au kupingwa kwa ajili ya imani yao. “Sikuzote muwe na hakika kabisa na imani yenyu” alishauri, huku akionya dhidi ya kujitenga, ambayo alionya kuwa inaweza kusababisha tabia mbaya na shida. Kutokana na hayo, Papa alisisitiza umuhimu wa kuelimishwa katika imani, na kuwa Wakristo wa kweli na halisi. “Jambo ni hili: Wakristo wameteswa tangu mwanzo,” alisema, huku akionesha ukweli kwamba jambo hili sio jipya. “Ingawa inaweza kushawishi kuwa na Ukristo uliopunguzwa na vuguvugu, hatuwezi kukubali. Badala yake, lazima tuwe imara, na lazima tuishi aina ya kifodini kwa maana hii.” Alitoa wito Papa Francisko.
Ugonjwa wa itikadi
Hatimaye, Papa alitoa wito wa kuhamasishwa zaidi juu ya majanga ya zamani, ili kujifunza kitu kwa siku zijazo na kufanya kazi kwa amani. “Itikadi ni ugonjwa,” alisema Baba Mtakatifu huku akiwataka watu wote kujenga maelewano na kuendeleza mazungumzo na tamaduni nyingine. “Hapana vita,” alisema, Papa akitoa wito wa amani. “Katika ulimwengu uliokata tamaa, usio na matumaini, lazima tuvutie maadili yetu,” alifafanua, huku akitoa wito kwa wanafunzi walioshiriki kulifanyia kazi hilo kabla ya kuwashukuru kwa juhudi zao. Baba Mtakatifu Francisko alimalizia kwa kuwashukuru wanafunzi hao kwa tafakari yao na kuwaambia kwamba wamemsaidia kuwaelewa, hasa wakati akijiandaa na safari yake ya kuelekea kwao mapema mwezi Septemba. Na hatimaye alitoa baraka zake.
Kujenga madaraja huanza na kila mmoja wetu
Ofisi mbalimbali za Vatican zilisaidia katika mpango huo, zikiwemo Sekretarieti Kuu ya Sinodi, Baraza Kipapa la Mawasiliano, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, Baraza la Kipapa la Elimu na Utamaduni na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji kwa ajili ya Uinjilishaji wa kwanza wa Makanisa maalum.
Kabla ya Baba Mtakatifu kujiunga na mazungumzo, hafla hiyo ilianza kwa utambulisho wa waandaaji, akiwemo Katibu wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini, Bi Emilce Cuda, na ujumbe wa video kutoka kwa Kardinali Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, yakifuatiwa na yale ya Askofu Luis Marín de San Martín, O.S.A., Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu. Kardinali Farrell alitoa wito kwa wanafunzi kuiga mfano wa Yesu wa kujenga madaraja na kuwakumbusha kwamba wakati wanaishi uhalisia uliobahatika, hasa wa kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu, kuna ulimwengu ambao una chuki, vita na mateso. Kutokana na hilo, aliwaalika hao kutenda wema, utunzaji, na uelewano katika ngazi ya kibinafsi, kwanza kabisa, kwa sababu vinginevyo, hatuwezi kutarajia wale wa ngazi za juu kufanya hivyo."
Askofu Marín naye alitoa maneno ya kutia moyo ambapo aliwaalika wote walioshiriki kwamba tumaini lipyaishwe, kuunda vifungo, kuvunja kuta na kujenga madaraja.” Wakati washiriki wakisubiri kuwasili kwa Papa, Dk. Cuda pia alisoma barua kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu, Kardinali José Tolentino de Mendonça, ambapo alikiri kwamba:“kujenga madaraja inaweza kuwa changamoto, na inaweza kukabiliana na mapambano na upinzani, lakini kwamba inastahili daima, kwa sababu inaishi kwa upendo ambao Yesu alitufundisha.”