Tafuta

Makanisa ya Mashariki yanapaswa kupendwa kwa sababu yanahifadhi Mapokeo ya maisha ya kiroho na hekima ya kimbingu. Makanisa ya Mashariki yanapaswa kupendwa kwa sababu yanahifadhi Mapokeo ya maisha ya kiroho na hekima ya kimbingu.  (Vatican Media)

ROACO Ni Chombo cha Huduma ya Matumani Kwa Makanisa ya Mashariki

Makanisa ya Mashariki yanapaswa kupendwa kwa sababu yanahifadhi Mapokeo ya maisha ya kiroho na hekima ya kimbingu na kwamba, yanayo maelezo ya kina kuhusu maisha ya Kikristo, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Liturujia, Mababa wa Kanisa, Mitaguso Mikuu, Umonaki; amana na utajiri mkubwa kwa Mama Kanisa. Katika Makanisa ya Mashariki kuna yale ambayo tayari yana umoja na Kanisa Katoliki na hivyo kushirikisha uzuri na historia ya maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO ni chombo cha huduma ya matumaini kwa Wakristo wa Makanisa ya Mashariki na hasa Mashariki ya Kati eneo ambalo kwa sasa limegeuka kuwa ni uwanja wa vita. Makanisa ya Mashariki yanapaswa kupendwa kwa sababu yanahifadhi Mapokeo ya maisha ya kiroho na hekima ya kimbingu na kwamba, yanayo maelezo ya kina kuhusu maisha ya Kikristo, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Liturujia, Mababa wa Kanisa, Mitaguso Mikuu, Umonaki; amana na utajiri mkubwa kwa Mama Kanisa. Katika Makanisa ya Mashariki kuna yale ambayo tayari yana umoja na Kanisa Katoliki na hivyo kushirikisha uzuri na historia ya maisha na utume wake. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, uzuri na historia ya Makanisa haya unaendelea kutoweka kwa kuanguka kwa Msalaba, kiasi kwamba, Makanisa haya yamegeuka kuwa ni Makanisa ya Mashuhuda wa Imani, yanayo beba ndanimwe Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Makanisa haya ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo uliotobolewa kwa Misumari na mkuki ubavuni.

Mkutano mkuu wa 97 wa ROACO, 2024
Mkutano mkuu wa 97 wa ROACO, 2024

Ni katika muktadha huu, Makanisa haya yanaendelea kububujika damu kutokana na vita inayoendelea kurindima huko Nchi Takatifu, Ukraine, Siria, Lebanon, Mashariki ya Kati, Caucaso pamoja na Tigray; maeneo ambayo kimsingi yana idadi kubwa ya Wakristo wa Makanisa ya Mashariki. Vita inaendelea kuyaathiri maeneo haya. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 27 Juni 2024 kwa wajumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewambia kwamba, Kanisa haliwezi kufumbia macho mahitaji msingi ya Wakristo wa Makanisa ya Mashariki, waamini wanapaswa kukita mizizi yao katika msingi wa Injili, ROACO inashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; Vita kati ya Israeli na Plestina, Vita kati ya Ukraine na Urusi; wimbi kubwa la wakimbizi na Wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati.

ROACO inataka kuwekeza katika Injii ya matumaini kwa vijana
ROACO inataka kuwekeza katika Injii ya matumaini kwa vijana

Baba Mtakatifu anasema, Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anawaalika Wakristo kuwakumbuka na kuwasaidia Wakristo katika mahitaji yao msingi na wala wasiwageuzie kisogo. Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo, ili kufanya upembuzi yakinifu wa kijiografia, ili kuonesha ujirani mwema, tayari kupunguza mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa ROACO kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwaunga mkono Wakristo Wakatoliki wa Kanisa la Mashariki, ili kupambana na udhaifu na umaskini; ili Wakleri na Watawa wawe tayari kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati, ili waweze kuimarisha imani yao, kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili; tayari kusimama kidete kulinda na kudumisha ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo na kwamba, wao ni Wakristo na Watoto wa Mungu.

Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu
Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu

Baba Mtakatifu anaishukuru ROACO kwa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji, kwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa; wao ni mawakala wa Injili ya upendo na ukarimu; vyombo na mashuhuda wa matumaini mintarafu Injili ya Kristo, utume wanaopaswa kuutekeleza kwa upendo na unyenyekevu, bila kutafuta makubwa, kwani hii ni kazi inayopendeza machoni pa Mwenyezi Mungu. Ni wakala wanaosimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu; wako tayari kusikiliza na kujibu kilio cha watoto wadogo kwa njia ya huduma! Ni watu wanaofanya kazi katika mazingira ya chuki na vita, lakini waendelee kujizatiti katika kupandikiza mbegu ya amani pasi kutumia mtutu wa bunduki. ROACO inaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, mwaliko kwa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kuhisi uwepo wao wa karibu, ili kushinda kishawishi cha Wakristo kutoka Mashariki ya Kati kukimbia nchi zao kutokana na madhara ya vita.

ROACO ni chombo cha Uinjilishaji wa kina
ROACO ni chombo cha Uinjilishaji wa kina

Vita kamwe haitakuwa ni chanzo cha amani na badala yake, wajikite katika mchakato wa majadiliano, ili kuhakikisha kwamba, watu wanaridhiana na kuishi kwa amani. Kwa njia ya vita, hakuna mshindi na kwamba, kuna waathirika wengi wa vita wanaohitaji suluhu ya vita. Bado kuna waathirika wa vita nchini Ukraine, na mwaliko ni kuendelea kusali bila kuchoka, ili amani ya kweli iweze kupatikana ili hatimaye, waamini waweze kukuza na kudumisha imani. Baba Mtakatifu amewakumbuka pia wakimbizi walioko Karabakh na kwamba, amempongeza na kumshukuru kiongozi mkuu wa Kanisa la Armenia na kumwomba amfikishie salam zake kwa viongozi wengine wastaafu. Inasikitisha kuona kwamba, kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati, wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kuna vijana wengi wanaoishi diaspora wanaohitaji huduma ya kitume, ili kuendeleza utambulisho wao, kwa kulinda na kudumisha amana na utajiri wa maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anayashukuru Makanisa ya Madhehebu ya Kilatini, yanayowapokea na kuwahudumia waamini hawa huku wakiheshimu tamaduni na Mapokeo yao. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kulihamasisha Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, kuifanyia kazi changamoto hii, kwa kuwapatia huduma za maisha ya kiroho, ili waendelee kubaki imara na thabiti katika Mapokeo yao, kwa kuwatengenezea Sheria na Kanuni za waamini wanaoishi diaspora.

ROACO 2024

 

27 June 2024, 14:57