Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Juni, anaadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Juni, anaadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji.   (katolici.mk)

Sherehe ya Kuzaliwa Kwa Yohane Mbatizaji: Shuhuda wa Nuru ya Uzima!

Papa Francisko anawaalika waamini kuiga ushuhuda na wa unyenyekevu uliotolewa na Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Ndiye aliyebahatika kumtangulia Kristo Yesu, ili kumwandalia njia, akamtambulisha kwa watu wa Mataifa, ili awasaidie kuwa mashuhuda jasiri wa Injili. Waamini wajitahidi kuvunjilia mbali tofauti zao ili kujenga na kudumisha maridhiano, udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii. Hizi ni nguzo msingi zinazoaminika katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Juni, anaadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Kwa kawaida Mama Kanisa huwaenzi watakatifu katika Liturujia siku ya kumbukizi ya vifo vyao. Lakini kwa Yohane Mbatizaji, Bikira Maria na Kristo Yesu tu huenziwa pia siku za kuzaliwa kwao, na hii ni kwa sababu ya nafasi walizonazo katika historia ya ukombozi wa mwanadamu. Leo tunaadhimisha kuzaliwa kwa mtangulizi wa mkombozi ambaye kuzaliwa kwake kuliashiria kuwa sasa ukombozi umefika. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuiga ushuhuda angavu na wa unyenyekevu uliotolewa na Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Ndiye aliyebahatika kumtangulia Kristo Yesu, ili kumwandalia njia, akamtambulisha kwa watu wa Mataifa, ili awasaidie kuwa mashuhuda jasiri wa Injili. Waamini wajitahidi kuvunjilia mbali tofauti zao ili kujenga na kudumisha maridhiano, udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii. Hizi ni nguzo msingi zinazoaminika katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Yohane Mbatizaji, alitumwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni shuhuda wa nuru, ili watu wasitembee tena gizani!

Tarehe 24 Juni ni Sherehe ya Yohane Mbatizaji
Tarehe 24 Juni ni Sherehe ya Yohane Mbatizaji

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wataendelea kujizatiti katika maisha yao kwa kuwa waaminifu katika miito mbalimbali waliyoitiwa na Mwenyezi Mungu, kama ushuhuda wa maisha na wito wa Kikristo. Waamini wanapaswa kujitahidi kumfuasa na hatimaye kufika kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hiki ni kiini cha Habari Njema inayopaswa kutangazwa kwa njia ya unyenyekevu; udugu; imani na utii kwa msaada na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu anayeendelea kulitegemeza Kanisa kwa nyakati mbalimbali za maisha na utume wake. Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni kielelezo makini cha uhusiano wa kina kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu, kwa njia ya Roho Mtakatifu. Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyefunga Agano la Kale, akawa daraja ya Agano Jipya, aliyemwandalia njia na hatimaye, wakati ulipowadia akamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Masiha, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Watu wengi walimfananisha Yohane Mbatizaji na Nabii Elia aliyewatakasa Waisraeli kutoka katika ibada ya kuabudu miungu, na kuwarejesha tena katika imani ya kweli iliyokita mizizi yake kwa Mwenyezi Mungu aliye hai, yaani Mungu wa Abramu, Isaka na Yakobo. Mtakatifu Yohane Mbatizaji alihubiri juu ya uwepo wa Masiha ambaye atajifunua kwao. Yohane Mbatizaji akawataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.

Watoto wana haki ya kupata ulinzi na usalama wa maisha yao
Watoto wana haki ya kupata ulinzi na usalama wa maisha yao

Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa. Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu akamshukia Kristo Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Kristo Yesu ni Masiha wa Bwana. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, tukio hili lilimshangaza sana Yohane Mbatizaji, kumwona Yesu akiwa kati kati ya kundi kubwa la wadhambi kama wao, lakini kwa ajili yao, ili aweze kubatizwa na kutekeleza haki yote sanjari na mpango wa wokovu wa Mungu. Kristo Yesu akajionesha kuwa ndiye Mwana kondoo wa Mungu anayeichukua na kuondoa dhambi ya ulimwengu. Yohane Mbatizaji ndiye aliyemtambulisha kuwa Kristo Yesu ndiye Mwana kondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Yesu! Hawa ndio akina Simone aitwaye Petro, na Andrea nduguye, Yakobo na ndugu yake Yohane, wote hawa walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya kama ilivyokuwa kwa Yesu. Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyetangaza na kusimamia ukweli, aliyekatwa kichwa na wafuasi wake waliposikia wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika kwa heshima! Hivi ndivyo nyota angavu ya Yohane Mbatizaji, ilivyozimika baada ya kumshuhudia Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Yohane Mbatizaji, kati ya watu maarufu wa Agano Jipya, anaishia kukatwa kichwa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kifodini ni huduma, utume na zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifodini ni kielelezo cha ukatili wa binadamu dhidi ya watu waaminifu wa Mungu.

Mtakatifu Yohane Mbatizaji
23 June 2024, 15:08