Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya Kuombea: Toba, Wongofu wa ndani na Utakatifu wa maisha na utume wa Kipadre. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya Kuombea: Toba, Wongofu wa ndani na Utakatifu wa maisha na utume wa Kipadre.  (Vatican Media)

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Toba, Wongofu na Utakatifu wa Maisha

Ijumaa tarehe 7 Juni 2024, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hii pia ni Siku ya Kuwaombea Mapadre: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Mwenyezi Mungu amependa kukutana na binadamu wote kwa njia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini wote kuendelea kujiaminisha kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kusema “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 7 Juni 2024 anaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ambaye kwa huruma, upendo, upole na unyenyekevu wa Moyo wake Mtakatifu, aliinuliwa pale juu Msalabani, akawa ni chemchemi ya huruma, upendo na uzima kwa watu wote wa Mungu. Kristo Yesu anatufahamu na anatupenda sisi sote, na kila mmoja wakati wa maisha yake. Hofu yake ya kifo katika bustani ya Mizeituni, na mateso yake yametolewa kwa ajili ya kila mmoja wetu: “Mwana wa Mungu… ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Ametupenda wote kwa moyo wa kibinadamu. Kwa sababu hiyo, Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa kwa sababu ya dhambi zetu, na kwa ajili ya wokovu wetu, unachukuliwa kama alama na ishara kuu ya mapendo yake yasiyo na mipaka ambayo kwayo Mkombozi, ambaye ni Mungu, anampenda Baba wa milele na watu wote bila kikomo.” KKK 478. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake Jumatano tarehe 5 Juni 2024 kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na Moyo Safi wa Bikira Maria, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujibu kwa ari na moyo mkuu, upendo wa wokovu kutoka kwa Kristo Yesu pamoja na kujiaminisha katika sala na maombi kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu. Yote haya ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko mjini Paray-le-Monial, nchini Ufaransa na kumkabidhi dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Maadhimisho haya yalianza kutimua vumbi tarehe 27 Desemba 2023 na yatahitimishwa tarehe 27 Juni 2025 katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Kurejesha upendo kwa upendo” tema inayomwilishwa katika hija mbalimbali, maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa pamoja na mikutano ambayo imekuwa ikiendeshwa kama sehemu ya kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque.

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Siku pia ya kuombea Utakatifu wa Mapadre
Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Siku pia ya kuombea Utakatifu wa Mapadre

Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kuandika Waraka wa Kitume kuhusu Moyo Mtakatifu wa Yesu, unaotarajiwa kutolewa Mwezi Septemba 2024. Huu ni waraka unaochota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu; Tafakari za Mababa wa Kanisa kuhusu Upendo wa Kristo Yesu, ili kulipyaisha Kanisa na ujumbe mahususi kwa walimwengu, kwani ulimwengu mamboleo unaonekana kukosa moyo! Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Mei 2024 alikutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la kumbukizi ya miaka 350 tangu Kristo Yesu alipotokea huko mjini Paray-le-monial, nchini Ufaransa. Katika hotuba yake kwa washiriki wa Kongamano la Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko Paray-le-Monial, na kumkabidhi dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, amekazia umuhimu wa kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazoendelea kusiginwa katika ulimwengu mamboleo. Ni vyema waamini wakajitambua kwamba, wao ni wadhambi, tayari kukiri udhaifu wao na kuomba msamaha. Sadaka ya Kristo Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba kwa binadamu mdhambi, chachu ya upatanisho kati ya Mwanadamu na Mwenyezi Mungu na kati ya binadamu wenyewe. Mwenyezi Mungu anaendelea kutoa machozi kutokana na kusiginwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbalimbali za dunia na hata kati ya watu wateule na watakatifu wa Mungu. Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu.

Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale Msalabani
Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale Msalabani

Kauli mbiu ya mkutano huu, inaonesha kwamba, makovu yanaweza kugangwa na kuponywa, ikiwa kama kuna utashi wa kutenda hivyo kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho, ili kurejesha amani na utulivu wa moyo! Toba na wongofu wa ndani pamoja na mambo mengine, inafumbatwa katika maisha ya mwamini kwa kutambua kwamba, ni mdhambi na anapaswa kuomba msamaha wa dhambi alizotenda na kwamba, Mwenyezi Mungu yuko tayari kumpokea mwamini aliyevunjika na kupondeka moyo, ili aweze kupata msamaha na maondoleo ya dhambi. Toba na msamaha ni kutambua dhambi zilizotendwa kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu aliyetambua ndani mwake kwamba, amekosa juu ya mbingu na mbele ya Baba yake Mwenye huruma. Rej. Lk 15:21. Kuomba msamaha kunafungua majadiliano yanayopania pamoja na mambo mengine, kurejesha mahusiano na mafungamano katika upendo wa kidugu, tayari kuonja faraja, pamoja na kupokea msamaha unaotolewa na huo ni mwanzo wa kuchipua tena fadhila ya upendo ili kuganga madonda ya moyo! Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko Paray-le-Monial, alimwomba, watu wafanye toba na malipizi kwa maondoleo ya dhambi zinazoendelea kuutesa Moyo wake Mtakatifu. Hii ndiyo dhamana na wajibu wa wajumbe hawa kuhakikisha kwamba, waamini wanaendeleza ibada ya toba na maondoleo ya dhambi, kama sehemu ya hija ya toba na wongofu wa ndani inayotekelezwa na kila Mbatizwa ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 aliitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu
Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu

Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu. Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wasikubali kumezwa na malimwengu, bali: utii, useja na ufukara, viwe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao. Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mapadre kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Papa Pio XII, “Haurietis acqua” wa Mwaka 1956 kuhusu “Moyo Mtakatifu wa Yesu kiini cha huruma ya Mungu.” Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya: imani, upendo, huruma, msamaha, uvumilivu, uaminifu na unyenyekevu wa Mungu, aliyejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta maisha na uzima wa milele! 

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Siku pia ya kuombea Utakatifu wa Mapadre
Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Siku pia ya kuombea Utakatifu wa Mapadre

Utakatifu wa Mapadre ni hitaji muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ukweli huu wa imani katika maisha na utume wa Mama Kanisa, unagusa hata maisha ya waamini walei ambao usiku na mchana wanatafuta utakatifu wao, kwa kutambua au kwa kutokujua kutoka kwa mtu wa Mungu. Waamini wanamwona Padre kuwa ni mshauri wa maisha ya kiroho, mpatanishi wa amani; mtu mwenye hekima na busara. Ni kiongozi salama ambaye watu wa Mungu wanaweza kujiaminisha kwake nyakati ngumu na wakati wa majaribu ya maisha, ili kuonja na hatimaye, kupata faraja na usalama wao! Ijumaa tarehe 7 Juni 2024, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hii pia ni Siku ya Kuwaombea Mapadre: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Mwenyezi Mungu amependa kukutana na binadamu wote kwa njia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini wote kuendelea kujiaminisha kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kusema “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako.” Waamini wainogeshe sala hii hasa zaidi wakati wa Mwezi Juni, uliotengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Waamini wamwombe Kristo Yesu ili aweze kuwafundisha kumpenda Mungu na jirani. Kwa wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya, watambue kwamba, Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kisima cha huruma na upendo wa Mungu unaopaswa kuwashwa duniani. Hapa ni mahali ambapo, waamini wanaweza kujichotea imani, matumaini na mapendo thabiti. Baba Mtakatifu Francisko anawashauri waamini wasione woga kumtolea Kristo Yesu shida na mahangaiko, wasiwasi, hofu na udhaifu wa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni Sherehe inayopendwa sana na watu wa Mungu. Ni wakati wa kuvumbua amana na utajiri unaohifadhiwa kwenye “sakafu” ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili hatimaye, kujifunza kumpenda Mungu na jirani na hivyo, kujenga utamaduni wa upendo. Waamini wamwombe Kristo Yesu neema na baraka ili waweze kuzitakatifuza nyoyo zao na hivyo kuondoa makando kando yanayokwamisha ustawi na maendeleo yao ya kiroho. Wamwombe Kristo Yesu kuondokana na kiburi na hali ya kukosa utaratibu katika maisha. Na badala yake, ajaze nyoyo zao upendo na hofu ya Mungu, ili hatimaye, nyoyo za waamini ziweze kupata amani, faraja na utulivu wa ndani.

Jubilei ya Miaka 350 Kwa Ibada ya Moyo Mtakatifu wa yesu
Jubilei ya Miaka 350 Kwa Ibada ya Moyo Mtakatifu wa yesu

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 26 Juni 2019 aliwakumbusha waamini kwamba, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni ukumbusho kwamba, Kristo Yesu anaishi “Christus vivit.” Kristo Yesu anawapenda waja wake, anaendelea kujisadaka kama chemchemi ya huruma, upendo, msamaha na wokovu wa walimwengu. Baba Mtakatifu anasema, huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia ili kuweza kupata: hifadhi, amani na utulivu wa ndani kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Waamini wajitahidi kwenda kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa Sakramenti ya Upatanisho. Kamwe waamini wasisite kujiaminisha chini ya Moyo Mtakatifu wa Yesu katika hija ya maisha yao hapa duniani! Waamini wavutwe na hisia za upendo wa kweli unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Watumie siku hii kwa ajili ya kuombea toba, wongofu na utakatifu wa Mapadre na wanapofanya hivi, wamkumbuke hata yeye katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili maisha na utume wao wote, upate chapa ya upendo wa Mungu kwa wanadamu wote! Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre kuendelea kukesha kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Upatanisho mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha wongofu wa shughuli za kichungaji. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu ni dalili kwamba, wito na utume huu mtakatifu, umehifadhiwa katika chombo cha udongo. Mapadre wanaopitia vipindi vigumu vya maisha na utume wao, wanapaswa kusindikizwa kwa huruma na upole; wasikilizwe kwa makini; wasaidiwe kufikia mang’amuzi na ukomavu katika maisha. Huu ni wajibu wa kwanza kwa Maaskofu mahalia, lakini hata kwa Jumuiya nzima ya waamini pamoja na familia zao, ambazo mara nyingi zinabeba Msalaba mzito! Wakleri ni watu ambao wanapaswa pia kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha na utume wao!

Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu
Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu

Kamwe Mapadre wasidhaniwe kuwa ni mashine za kutolea huduma ya mambo matakatifu! Mapadre wapendwe katika ukweli na uwazi; wasaidiwe kupata mahitaji yao msingi. Waamini walei, wakishirikiana, wakisaidiana na kushauriana na Mapadre wao, maisha na utume wa Kanisa vitasonga mbele kwa ari kubwa zaidi! Pale ambapo Mapadre wanaonekana kuchoka na kuanza kukata tamaa, waamini wawe mstari wa mbele kuwaenzi kwa sala na sadaka zao; kwa kutambua na kuthamini huduma zao pamoja na ushauri wa udugu wa kibinadamu. Siku ya Kuombea Utakatifu wa Mapadre, iwe ni fursa ya kuwasindikiza Mapadre katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Katika majitoleo kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mama Kanisa anawaalika watoto wake katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: kushiriki Misa Takatifu, kupokea Ekaristi Takatifu na kutenda matendo ya huruma, kusali sala iliyoelekezwa na Mama Kanisa kama njia ya kulipia madhulumu dhidi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu yafanywayo na watu mbalimbali na hasa kwa kukosa heshima kwa Sakramenti Kuu, yaani Ekaristi Takatifu. Matunda ya majitoleo hayo ni neema zibubujikazo kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu! Ahadi zinazobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu: Nitawajalia neema zote watakazozihitaji katika hali yao ya maisha. Nitawajalia amani katika familia zao. Nitawafariji katika magumu yao yote. Nitakuwa kimbilio lao salama wakati wa maisha yao, na zaidi sana katika saa yao ya kufa. Nitawapa baraka tele katika shughuli zao zote. Wakosefu watapata katika Moyo wangu chanzo na bahari ya huruma isiyo na mwisho. Waamini walio vuguvugu watakuwa na bidii. Waamini wenye bidii watakwea kwa upesi katika ngazi za juu za ukamilifu. “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako Mtakatifu.”

Sherehe Moyo Mtakatifu wa Yesu
06 June 2024, 15:15