Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume: Lango la Uinjilishaji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 29 Juni 2024 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwasherehekea Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, waliokuwa tayari kuyamimina maisha yao kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka sanjari na kutoa Pallia Takatifu kwa Maaskofu wakuu 42 walioteuliwa katika kipindi cha mwaka 2023-2024 na kati yao 32 wamehudhuria na kushiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu. “Pallium” kwa lugha ya Kilatin ambayo kwa lugha sanifu ya Kiswahili ni “Pallia Takatifu” yaani vazi la kiliturujia linalovaliwa na Maaskofu wakuu wakati wa Ibada kwenye eneo la majimbo yao makuu mintarafu Sheria za Kanisa za Mwaka 1983. Pallia takatifu hutokana na sufu safi iliyokatwa kutoka kwa kondoo waliobarikiwa wakati wa Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, Bikira inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallia Takatifu, wanazovishwa Maaskofu wakuu katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Petro na Paulo Mitume. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Pallia takatifu anayovaa Askofu mkuu shingoni ni alama ya Mchungaji mwema anayewabeba kondoo wake mabegani.
Mtakatifu Petro, Mtume alikuwa ni mvuvi kutoka Galilaya aliyechaguliwa kuwa ni mvuvi wa watu na Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa alilidhulumu Kanisa la Kristo, lakini kwa mwanga wa Neno la Mungu wameweza kushiriki kikamilifu mang’amuzi ya Fumbo la Pasaka, hawa wamekombolewa na Kristo Yesu na mlango ukawafungukia wenyewe katika mwelekeo wa maisha mapya. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia kielelezo cha mlango mintarafu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo; Ukombozi wa Mtakatifu Petro kutoka Gerezani na Mtakatifu Paulo akakutana uso kwa uso na Kristo Yesu Mfufuka, wakati akiwa njiani kuelekea Dameski, akienda kuwadhulumu Wakristo. Wote hawa wakapewa fursa ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, changamoto kwa Wakristo kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao; watakatifu Petro na Paulo Mitume ni walinzi na waombezi wa mji wa Roma; Maaskofu wakuu waliopewa Pallia Takatifu wanaitwa na kutumwa kuwa ni wachungaji wenye ari na moyo mkuu, wanaofungua lango la Injili, tayari kushiriki katika ujenzi wa Kanisa na jamii yenye malango yaliyo wazi.
Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Maadhimisho ya Jubilei ni muda wa neema na kwamba, kwa kufungua Lango kuu la Jubilei watu waaminifu wa Mungu wanaweza kuvuka na hatimaye kuingia katika Lango la Madhabahu hai ya Kristo Yesu, ili ndani mwake, waamini waweze kuonja upendo wa Mungu unaopyaisha matumaini na furaha, kama ilivyokuwa kwa maisha ya Mtakatifu Petro na Paulo. Somo la kwanza ni muhtasari wa historia ya ukombozi na mang’amuzi ya Fumbo la Pasaka, siku ya mikate isiyotiwa chachu, Herode Mfalme akanyosha mkono wake kuwatenda mabaya watu wa Kanisa; Ukombozi huu kutoka gerezani unafanyika usiku wa manane kama ilivyokuwa kwa Waisraeli! Kimsingi hili ni simulizi jipya, linalomwonesha Mwenyezi Mungu akilikomboa Kanisa lake na watakatifu wateule wake kutoka katika minyororo ya wadhalamu, kielelezo cha Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anayewaenzi waja wake katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu ndiye anayefungua lango, kuwakomboa waja wake na kuwaonesha njia ya kupita na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kiongozi wao mkuu. Haya pia ndiyo mang’amuzi ya Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, aliyetubu na kumwongokea Mungu baada ya kukutana uso kwa uso na Kristo Mfufuka wakati akiwa njiani kuelekea Dameski, akienda kuwadhulumu Wakristo. Akapata fursa ya kumtafakari Kristo Yesu Mteseka, akagundua neema katika udhaifu wake wa kibinadamu na kutiwa shime na Kristo Mfufuka, ili akiwa amesulubiwa pamoja na Kristo Yesu, wala si yeye tena anayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yake. Rej. Gal 2:20. Tukio la Mtume Paulo kukutana na Kristo Mfufuka linamkirimia ari na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Rej. 2Tim 4:17.
Hiki ni kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake fursa za kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, na Mwenyezi Mungu akawafungulia hata wapagani Lango la imani, mwaliko kwa waamini hata wao kusali ili Mwenyezi Mungu awafungulie Lango la Neno ili wapate kutangaza na kushuhudia Fumbo la Kristo. Rej. Kol 4:3. Baba Mtakatifu anasema, Mtume Petro na Paulo walifanya mang’amuzi ya imani, wakashuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, kiasi hata cha kuwafungulia wapagani Lango la Imani na kuwapatia fursa ya kuinjilisha, kama kielelezo cha kushiriki ile furaha ya kukutana na ndugu zao pamoja na Jumuiya za waamini zilizokuwa zinaibuka kwa wakati ule. Huu ni mwaliko kwa waamini kung’amua Lango la Imani, ambalo wakati mwingine linafungwa kutokana na uchoyo na ubinafsi; hali ya kutoguswa wala kuwajali wengine; hali ya kujikatia na kukata tamaa. Waamini wakiwa wameshikamana na kuambatana na Kristo Yesu, wawe tayari kutambua Lango la Imani, ili waweze kuonja furaha ya Uinjilishaji, huku wakipiga moyo konde, tayari kuambata ushindi dhidi ya ndago zinazofifisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Waamini wanayo shauku ya Kanisa linalowafungulia Malango ya matumaini, tayari kuwapokea watu wote, ili waweze kujisikia kwamba, wanakumbatiwa na upendo wa Mwenyezi Mungu.
Mji wa Roma unapaswa kuwa ni Lango wazi, ambalo halina haja ya kujifungia ili kujilinda kama ilivyokuwa hapo awali, bali Roma uwe ni mji unaojikita katika matumaini, kwa kuyaendea yajayo, kwa amani na utulivu na hivyo kujikita katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Mji wa Roma upate nafuu ya usafiri, watu wote wapate fursa ya kujisikia kwamba, wako nyumbani. Roma uwe ni mji unaochochea utamaduni wa watu kukutana, usaidie kukoleza ujenzi wa urafiki wa kijamii, mshikamano na uwe ni mji unaofumbata tamaduni, sanaa na uzuri, tayari kutoa nafuu katika maisha. Baba Mtakatifu Francisko amebariki Pallia Takatifu kwa ajili ya Maaskofu wakuu wapya 42 watakazovikwa na Mabalozi wa Vatican kwenye Majimbo yao makuu. Pallia Takatifu ni kielelezo cha ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa mfano wa Kristo Yesu, Lango la kondoo wake. Rej. Yn 10:7. Maaskofu wakuu waliopewa Pallia Takatifu wanaitwa na kutumwa kuwa ni wachungaji wenye ari na moyo mkuu, wanaofungua lango la Injili, tayari kushiriki katika ujenzi wa Kanisa na jamii yenye malango yaliyo wazi. Pallia takatifu ni alama ya ushiriki mkamilifu wa Maaskofu wakuu katika kuliongoza Kanisa la Kristo. Pallia baada ya kutengenezwa huwekwa chini kabisa ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, karibu na kaburi la Mtakatifu Petro: “Confessio Petri” na kubarikiwa kesho yake yaani tarehe 29 Juni ya kila mwaka, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa Kanisa. Pallia inapambwa kwa alama ya misalaba mitano, kielelezo cha Madonda Matakatifu ya Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Pallia inapambwa pia kwa misumari mitatu iliyotumika kumtundika Kristo Yesu Msalabani, mara mikono na miguu yake ikafungwa kwa misumari. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallia takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa wakati huu ni Baba Mtakatifu Francisko.
Baba Mtakatifu katika Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume ametoa Pallia Takatifu kwa Maaskofu 42 na kati yao 33 ndio waliofika Roma kwa ajili ya tukio hili. Kutoka Barani Afrika ni kama wafuatavyo: Kardinali Protase RUGAMBWA, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania; Askofu mkuu Gustavo BOMBÍN ESPINO, O.SS.T. wa Jimbo kuu la Toliara, Madagascar; Askofu mkuu Prosper KONTIEBO, M.I. wa Jimbo kuu la Ouagadougou Burkina Faso; Askofu mkuu Abel LILUALA wa Jimbo kuu la Pointe-Noire, Jamhuri ya Watu wa Congo; Askofu mkuu Gabriel Blamo JUBWE wa Jimbo kuu la Monrovia, Liberia; Askofu mkuu Félicien NTAMBUE KASEMBE, C.I.C.M. wa Jimbo kuu Kananga, DRC; Askofu mkuu Raphael p’Mony WOKORACH, M.C.C.J. wa Jimbo kuu la Gulu, Uganda, Askofu mkuu Ignace Bessi Dogbo wa Jimbo kuu la Abidjan, nchini Pwani ya Pembe na hatimaye, ni Askofu mkuu Benjamin PHIRI wa Jimbo kuu la Ndola, Zambia. Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 12 Januari 2015 alitamka kwamba, tangu wakati huo, Maaskofu wakuu watakuwa wanashiriki katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kubariki Pallia takatifu kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa imani, lakini Pallia takatifu watavikwa na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika kadiri ya nafasi zao. Lengo kuu la mabadiliko haya ni kuwawezesha watu wa Mungu kutoka katika Makanisa mahalia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya adhimu katika maisha, historia na utume wa Kanisa mahalia. Pili, ni kuendelea kuimarisha mchakato wa unafsishaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.”
Baba Mtakatifu Francisko ameushukuru ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, kwa kuhudhuria na kuonesha utashi wa ujenzi wa umoja wa Kanisa kati ya Makanisa haya mawili. Amewaomba wamfikishie salam na matashi mema Patriaki Bartolomeo wa kwanza.