Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Pallia Takatifu Kwa Maaskofu Wakuu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 29 Juni 2024 anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwasherehekea Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, waliokuwa tayari kuyamimina maisha yao kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka sanjari na kutoa Pallia Takatifu. “Pallium” kwa lugha ya Kilatin ambayo kwa lugha sanifu ya Kiswahili ni “Pallia Takatifu” yaani vazi la kiliturujia linalovaliwa na Maaskofu wakuu wakati wa Ibada kwenye eneo la majimbo yao makuu mintarafu Sheria za Kanisa za Mwaka 1983. Pallia takatifu hutokana na sufu safi iliyokatwa kutoka kwa kondoo waliobarikiwa wakati wa Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, Bikira inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari. “Agnes” maana yake kwa lugha ya Kiswahili ni “Mwanakondoo.” Mtakatifu Agnes, Bikira na shahidi, aliuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu mchumba wake wa daima, kiasi cha kuyasadaka maisha yake, ili asiuchafue ubikira wake.
Na katika Agano Jipya Yohane Mbatizaji anamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu anayebeba na kuondoa dhambi za ulimwengu. Rej. Yn. 1:29, 36. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallia Takatifu, wanazovishwa Maaskofu wakuu katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Petro na Paulo Mitume. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Pallia takatifu anayovaa Askofu mkuu shingoni ni alama ya Mchungaji mwema anayewabeba kondoo wake mabegani.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 24 Aprili 2005 wakati alipokuwa anasimikwa rasmi kuliongoza Kanisa Katoliki alisema kwamba, Pallia takatifu wanayovaa Maaskofu wakuu mabegani mwao, ni alama pia ya wanakondoo waliopotea, wagonjwa na wadhaifu. Kumbe, ni dhamana na wajibu wa Askofu mkuu kuwabeba wote hawa na kuwapeleka kwenye chemchemi ya maji ya uzima. Kumbe, Pallia takatifu ni kielelezo cha nira ya Kristo Yesu anayewaalika waja wake akisema “Jitieni nira yangu… kwa maana nira yangu ni laini…” Mt. 11:20. Pallia takatifu ni alama ya ushiriki mkamilifu wa Maaskofu wakuu katika kuliongoza Kanisa la Kristo. Pallia baada ya kutengenezwa huwekwa chini kabisa ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, karibu na kaburi la Mtakatifu Petro: “Confessio Petri” na kubarikiwa kesho yake yaani tarehe 29 Juni ya kila mwaka, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa Kanisa.
Pallia inapambwa kwa alama ya misalaba mitano, kielelezo cha Madonda Matakatifu ya Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Pallia inapambwa pia kwa misumari mitatu iliyotumika kumtundika Kristo Yesu Msalabani, mara mikono na miguu yake ikafungwa kwa misumari. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa wakati huu ni Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu katika Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume atatoa Pallia Takatifu kwa Maaskofu 42 na kati yao 33 ndio waliofika Roma kwa ajili ya tukio hili. Kutoka Barani Afrika ni kama wafuatavyo:
Kardinali Protase RUGAMBWA, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania; Askofu mkuu Gustavo BOMBÍN ESPINO, O.SS.T. wa Jimbo kuu la Toliara, Madagascar; Askofu mkuu Prosper KONTIEBO, M.I. wa Jimbo kuu la Ouagadougou Burkina Faso; Askofu mkuu Abel LILUALA wa Jimbo kuu la Pointe-Noire, Jamhuri ya Watu wa Congo; Askofu mkuu Gabriel Blamo JUBWE wa Jimbo kuu la Monrovia, Liberia; Askofu mkuu Félicien NTAMBUE KASEMBE, C.I.C.M. wa Jimbo kuu Kananga, DRC; Askofu mkuu Raphael p’Mony WOKORACH, M.C.C.J. wa Jimbo kuu la Gulu, Uganda, Askofu mkuu Ignace Bessi Dogbo wa Jimbo kuu la Abidjan, nchini Pwani ya Pembe na hatimaye, ni Askofu mkuu Benjamin PHIRI wa Jimbo kuu la Ndola, Zambia.
Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 12 Januari 2015 alitamka kwamba, tangu wakati huo, Maaskofu wakuu watakuwa wanashiriki katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kubariki Pallia takatifu kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa imani, lakini Pallia takatifu watavikwa na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika kadiri ya nafasi zao. Lengo kuu la mabadiliko haya ni kuwawezesha watu wa Mungu kutoka katika Makanisa mahalia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya adhimu katika maisha, historia na utume wa Kanisa mahalia. Pili, ni kuendelea kuimarisha mchakato wa unafsishaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.”
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume kwa mwaka 2019 alikazia mambo makuu matatu: Mitume hawa walikuwa ni mashuhuda wa maisha, msamaha na mashahidi wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ni Mitume waliojisadaka kutangaza, kushuhudia na kuishi utume wao, hija ambayo imewafikisha hadi Roma, na hapa wakayamimina maisha, kielelezo makini cha ushuhuda kwa Kristo Yesu, maisha na msamaha! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda katika maisha ya kiroho kwani walikuwa ni wachamungu! Ni watu ambao walionesha udhaifu mkubwa wa kibinadamu, kiasi hata cha Mtakatifu Petro kumkana Kristo Yesu mara tatu wakati ambapo Mtume Paulo alilidhulumu Kanisa la Kristo. Lakini wote hawa wakaoneshwa na kuonjeshwa: huruma na upendo wa Kristo hasa pale Yesu alipomuuliza Mtume Petro mara tatu, ikiwa kama alikuwa anampenda, Petro akasononeka sana.
Mtume Paulo akaulizwa kwanini alikuwa analidhulumu Kanisa lake? Wote wawili waliitwa kwa majina yao, hali ambayo iliwaletea toba na wongofu wa ndani. Hawa ni wadhambi wawili waliotubu na kumwongokea Mungu; ni watu ambao walitambua kwamba ni wadhambi na Yesu akachukua fursa hii kuwafanyia miujiza, kielelezo cha upendo wake, kwa wale wote wanaothubutu kumfungulia hazina ya nyoyo zao, kwa kujiweka mbele ya Kristo, ili aweze kuwatumia kama vyombo na mashuhuda wake. Ni watu walioonesha moyo wa unyenyekevu hadi dakika ya mwisho wa maisha yao, kiasi hata cha Mtume Petro kusulubiwa miguu juu, kichwa chini! Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema, jina Paulo maana yake ni “mtu mdogo”, kielelezo cha unyenyekevu uliomfanya hata watu kusahau jina lake la asili ambalo ni Saulo, aliyekuwa Mfalme wa kwanza wa Israeli.
Hawa Mitume wakatambua kwamba, utakatifu wa maisha unafumbwa katika unyenyekevu, kwa kutambua na kukiri udhaifu na umaskini wao, kiasi cha kujiaminisha kwa Kristo Yesu, aliyewatendea miujiza kwa kuwanyanyua juu, kwa njia ya Msamaha unaoganga na kuponya! Mitume Petro na Paulo ni mashuhuda wa msamaha wa Kristo Yesu, uliowajalia toba na wongofu wa ndani, wakabahatika kuwa watu wapya, wenye furaha na amani ya ndani. Wakasahau ya kale na kuanza kuyaambata maisha mapya yaliokuwa yameboreshwa kwa huruma na upendo wa Kristo uliokuwa na nguvu kubwa kupita hata mapungufu na makosa yao ya kibinadamu. Huruma ya Mungu inawajalia waamini kuwa na maisha mapya, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho katika maisha yao!
Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka; mashuhuda wa msamaha unaoganga na kuponya na hatimaye, wakawa ni mashuhuda wa Masiha, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, nyakati zote ni zake; chemchemi ya upendo wa kweli. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni ushuhuda unaobubujika kutokana na Mtume Petro kukutana na Kristo Yesu katika maisha yake kama ilivyokuwa hata kwa Mtume Paulo anayelitaja jina la Kristo Yesu mara 400 katika nyaraka zake mbalimbali. Kwa Mtume Paulo, Kristo kwake ni nguzo ya maisha, kiasi kwamba, mambo yale yaliyokuwa faida kwake akayahesabu kuwa ni hasara kwa ajili ya Kristo!
Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, kuwaangalia Mashuhuda hawa wa imani, ili kupyaisha maisha yao, hatimaye, waweze kumfahamu Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao na wala wasikomee tu kwa yale yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii au kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili kweli Kristo Yesu aweze kuwa ni nguzo ya maisha yao, tayari kuwasamehe, ili kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha, kiasi hata cha kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda hai wa Kristo Yesu katika ulimwengu mamboleo. Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani yanahudhuriwa pia na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Costantinopol wa mwendelezo wa Mapokeo kwa Makanisa haya mawili.
Hii ni changamoto ya kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kuweza hatimaye, kufikia umoja kamili katika ngazi zote. Kwa sababu, wote wakiwa wamepatanishwa na Mwenyezi Mungu na kusamehewa dhambi zao; wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao yenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 26 Juni 2024 aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufuata mifano ya Wamisionari Mitume, Petro na Paulo, kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.
Baba Mtakatifu aliwaweka watu wote wanaoendelea kuathirika kutokana na vita, chini ya ulinzi na tunza ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa Imani, ili nchi ya Ukraine, Palestina, Israeli, Myanmar na maeneo mengine, yaweze kupata amani ya kudumu mapema iwezekanavyo!