Tafuta

Katika mkesha wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, tarehe 28 Juni 2024, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli. Katika mkesha wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, tarehe 28 Juni 2024, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli.   (Vatican Media)

Majadiliano ya Kiekumene: Ushuhuda wa Imani, Matumaini na Mapendo Kwa Kristo Yesu

Tarehe 28 Juni 2024 Papa amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia kuhusu: Ushuhuda wa Makanisa haya pacha, Kumbukizi ya Miaka takribani 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kuzungumza na Patriaki Anathagoras, Tamko la Amani Kuhusu Yerulusalem, Waamini waungane ili kuombea amani; Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba ya imani, Jumamosi tarehe 29 Juni 2024 anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 asubuhi kwa Saa za Ulaya. Katika Ibada hii, atabariki Pallia Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 33 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2023-2024. Ni katika mkesha wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, tarehe 28 Juni 2024, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia kuhusu: Ushuhuda wa Makanisa haya pacha, Kumbukizi ya Miaka takribani 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kuzungumza na Patriaki Anathagoras, Tamko la Amani Kuhusu Yerulusalem, Waamini waungane ili kuombea amani; Jubilei ya Miaka 1700 tangu kuadhimishwa kwa Mtaguso wa Nicea. Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli kwa kutuma ujumbe katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, kielelezo cha mafungamano ya dhati kati ya Makanisa haya pacha, yaani Kanisa la Roma na lile la Costantinopoli, ambayo yamedhamiria kujikita katika hija ya kutafuta na hatimaye, kuambata umoja wa Wakristo, dhamana inayotekelezwa kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, atakayewawezesha Wakristo kufikia ushirika kamili katika tofauti zao msingi. Hii ni safari iliyoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Patriaki Anathegoras. Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014 alifanya hija ya kitume katika Nchi Takatifu kama kumbukumbu ya Jubilee ya miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu.

Jubilei ya Miaka 1,700 ya Mtaguso wa NICEA, 2025
Jubilei ya Miaka 1,700 ya Mtaguso wa NICEA, 2025

Tangu wakati huo majadiliano ya kiekumene yameendelea kushika kasi, ili kuvuka kipeo cha kashfa ya utengano kati ya Makanisa, ili hatimaye, katika umoja, upendo na mshikamano Wakristo waweze kutoa ushuhuda wa Injili unaobubujika kutoka katika umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kanisa Katoliki linaendelea kujipambanua kama chombo cha kuhamasisha umoja wa Wakristo. Kwa upande wake, Kanisa la Kiorthodox linaendelea kujiimarisha katika uekumene wa udugu miongoni mwa Wakristo. Mchakato wa majadiliano ya kiekumene anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza unafumbatwa katika: upendo, ukweli na unabii, hatua ambayo kwa sasa ndiyo inayovaliwa njuga na viongozi wa Makanisa haya mawili. Tukio la viongozi hawa wawili kukutana mjini Yerusalemu, mahali ambapo Kristo Yesu alizaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu; ni mahali ambapo Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume kwa mara ya kwanza katika maisha na historia ya Kanisa; kwa pamoja wakaamua kujizatiti katika hija ya kutafuta umoja wa Wakristo, ili wote wawe wamoja: “Ut unum sint” Rej. Yn 17:21. Baba Mtakatifu Francisko bado anakumbukumbu hai juu ya tukio hili na kwamba, anamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, kwa neema ya urafiki wa kidugu ambao umekuwa na kuchanua katika miaka ya hivi karibuni, kwa kukutana mara kwa mara na kushirikiana katika medani mbalimbali za maisha kama vile utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na amani. Ilikuwa ni tarehe 8 Juni 2014 viongozi wa Makanisa na Serikali ya Israeli na Palestina walipokutana na kusali kwa ajili ya kuombea amani, miaka kumi iliyopita. Leo hii kuna watu ambao wamegubikwa hofu na mashaka ya maisha yajayo! Sala ya kuombea amani ni kwa ajili ya Mataifa yote duniani, lakini kwa namna ya pekee Ukraine inayoendelea kuteseka sana. Katika kipindi hiki cha hofu na mashaka, Makanisa hayana budi kutangaza na kushuhudia Injili ya Matumaini na kwamba, Kristo Yesu ndiye tumaini lao. Rej. 1Tim 1: 1.

Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo
Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa Kanisa la Kiorthodox kushirikiana na Kanisa Katoliki ili kusindikiza tukio hili muhimu la Maadhimisho ya Mwaka wa neema ili kamwe waamini wasitindikiwe neema na matunda ya maisha ya kiroho katika maadhimisho haya na kwamba, uwepo wao katika maadhimisho ni muhimu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1,700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka huo Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Tukio hili la kihistoria liamshe ndani ya Wakristo ari na moyo wa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, huku wakiendelea kujenga umoja na ushirika wa Kanisa. Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Makanisa linaendelea kujipanga vyema, ili kuliadhimisha kikamilifu tukio hili. Baba Mtakatifu anasema, amepokea mwaliko kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza na kwamba, ametia nia ya kwenda kutembelea maeneo yaliyofanyikia Mkutano wa Nicea. Hii ni changamoto ya kuendelea kujikita katika hija ya upendo, upatanisho na huruma. Umoja wa Wakristo ni changamoto kubwa, lakini jambo la msingi ni kuendelea kutembea, kusali na kufanya kazi kwa pamoja!

Ujumbe wa Patriaki
28 June 2024, 14:47