Siku ya Columba Kwa Mwaka 2024 & Jubilei ya Miaka 25 ya Utume
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya “Siku ya Columba kwa Mwaka 2024 sanjari na Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mikutano ya Kimataifa ya Wacolumbani, yamefanyika katika Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Piacenza-Bobbio, nchini Italia, Dominika tarehe 23 Juni 2024. Hii ni changamoto ya kuendelea kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa Kanisa mintarafu mwanga wa Injili ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliowaandikia washiriki wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Siku ya Columba kupitia kwa Askofu Adriano Cevolotto wa Jimbo Katoliki la Piacenza-Bobbio pamoja na mambo mengine anakazia ujenzi wa mtandao wa maisha ya kiroho na utamaduni wa urafiki wa udugu wa kibinadamu; waamini warutubishe maisha yao ya kiroho kwa tunu msingi za kijamii na kamwe wasimezwe na malimwengu. Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka washiriki wote wa Jubilei ya Miaka 25 ya Siku ya Wacolumba na kwamba, wajumbe wanayo kila sababu ya kushiriki furaha hii ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuazishwa kwake, kama kumbukumbu endelevu ya utume na maisha aliyoishi Mtakatifu Columba aliyezaliwa tarehe 7 Desemba 521 na kufariki dunia tarehe 9 Juni 597 na kujipambanua kama Abate na mmisionari aliyesimma kidete kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.
Maadhimisho haya ni chemchemi ya utajiri wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Ujumbe wa Mtakatifu Columba ni muhimu katika ujenzi wa maisha ya kiroho, dhidi ya upagani mamboleo pamoja na kupenda sana malimwengu. Mtakatifu Columba, mmonaki na mmisionari alichakarika kutemba usiku na mchana, akitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na hivyo kuokoa tena mbegu ya Ukristo iliyokuwa imedhoofu na hivyo kuingia katika hatari za kutoweka katika uso wa dunia. Wamonaki hawa walichangia pia katika mchakato wa maboresho ya maisha ya kiroho, elimu na kanuni maadili. Ni katika muktadha huu, Wabenediktini kwa njia ya wamonaki wa Mtakatifu Columba wamechangia kwa kiasi kikubwa utunzaji na upyaishaji wa utamaduni wa Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa waamini walioko katika karne ya ishirini na moja, wanapaswa kuchota amana na utajiri unaobubujika kutoka katika tunu msingi za maisha ya kiinjili, bila kuzama katika utanadawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; huruma ishike mkondo wake badala ya kuzama katika uchu wa madaraka.
Kumbe, huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia imani na utamaduni unaofumbatwa katika ubunifu na uaminifu mintarafu utajiri wa mapokeo yao. Ni kwa njia hii, waamini wataweza kuchangia katika mchakato wa ujenzi wa Ulaya unaoliwezesha Bara la Ulaya na watu wake kuishi kwa amani, huku wakitembea bega kwa bega; kuthamini tofauti zao msingi, lakini daima wakiwa wazi kukutana na kuendelea kupyaisha majadilinao pamoja na tamaduni nyinginezo, kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha ujumbe wake kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Siku ya Columba, kwa kuwashukuru washiriki wote, lakini zaidi wale wanaotekeleza dhamana na shughuli zao zinazopata chimbuko lake kutoka katika tunu msingi za Kiinjili na kuziendeleza kwa njia ya ushirikiano na Serikali mbalimbali. Wote hawa Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume.