Tafuta

Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani 2024

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani, Jumatano tarehe 26 Juni 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameelekeza katekesi yake juu ya siku hii muhimu, kama anavyosema Mtakatifu Yohane Paulo II kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya yanafukarisha jamii, yanapunguza nguvu za kibinadamu na kimaadili; yanaathiri uwezo wa mtu kuishi na kushiriki katika maboresho ya jamii husika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu mwaka 1989, Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni, inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani. Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupambana na dawa za kulevya na uhalifu, “United Nations Office on Drugs and Crime, UNODC” inasema, lengo ni kusaidia maboresho ya uelewa mpana zaidi wa mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani, sanjari na biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake. Kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho haya kwa mwaka 2024 ni “Kupambana na dawa za kulevya: kuwekeza katika kuzuia kwa maisha bora ya baadaye.” Ni wazi kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga linaloiathiri jamii kwa ujumla. Dawa haramu zinazosambaa sokoni huchochea matatizo ya afya na usalama, na kuhatarisha maisha ya watu binafsi na wale wanaowazunguka. Hii ndiyo sababu ni muhimu kuendelea kuongeza ufahamu, kuzuia matumizi haramu ya dawa za kulevya, na kutoa nyenzo kusaidia wale wanaoathirika. Katika siku hii ya uhamasishaji, ni muhimu kukumbuka kuwa mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya sio lazima yawe ya kuadhibu tu, bali pia yaambatane na hatua za kuelimisha na za kuzuia. Uwekezaji katika kuzuia ndio ufunguo wa kulinda jamii na kuhakikisha mustakabali mzuri wa kizazi kijacho. Jumuiya ya Kimataifa inakumbushwa kwamba, kinga ni bora zaidi kuliko tiba, na kwamba kila hatua ya mtu binafsi inazingatiwa katika mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kupambana na biashara hii ambayo ina madhara makubwa katika afya, utawala bora, ulinzi na usalama wa raia na mali zao! Ikumbukwe kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake ni kikwazo kwa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Siku ya Kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani
Siku ya Kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani

Baba Mtakatifu Francisko anasema, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kama vile kazi za suluba kwa watoto wadogo, biashara ya ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Mambo haya yanapaswa kutambuliwa kama yalivyo na viongozi wote wa kidini, wanasiasa, viongozi wa kijamii na watunga sera na sheria wa kitaifa na kimataifa! Waathirika wakuu wa janga la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni vijana wa kizazi kipya wanaopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa afya, maisha na jamii katika ujumla wake, changamoto kwa watu wote wenye mapenzi mema kujifunga kibwebwe ili kupambana dhidi ya uzalishaji, uchakataji, usambazi na matumizi haramu ya dawa hizi sehemu mbalimbali za dunia. Ni dhamana pevu kwa serikali kuhakikisha kwamba, zinapambana kufa na kupona na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwa kuwashughulikia kisheria wale wote wanaoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo miongoni mwa vijana! Matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa njia ya mitandao ni hatari inayoendelea kujionesha kila kukicha na kwamba, vijana ndio wanaotumbukizwa kwa urahisi katika janga hili, kiasi cha kupoteza maana ya maisha. Kutokana na changamoto hizi, Mama Kanisa anapenda kujipambanua katika masuala haya, ili kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili kwamba, binadamu na mahitaji yake msingi apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Utu wa binadamu ndiyo msingi wa Injili ya huruma ya Mungu. Ni kutokana na msingi huu, Wakristo wanapaswa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji ili kusaidia mchakato wa kuzuia, kuganga na kuponya magonjwa yanayotokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Biashara ya binadamu ni janga la kimataifa
Biashara ya binadamu ni janga la kimataifa

Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, Kanisa linataka kumweka binadamu kuwa ni kiini cha sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Mama Kanisa ataendelea kushirikiana na kushikamana na wadau sehemu mbalimbali za dunia katika kuelimisha, kuzuia, kurekebisha na kuwaponya waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu. Ushindi dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya unafumbatwa kwa namna ya pekee katika umoja na mshikamano kati ya taasisi, familia na sekta ya elimu katika ujumla wake. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani, Jumatano tarehe 26 Juni 2024, Baba Mtakatifu Francisko ameelekeza katekesi yake juu ya siku hii muhimu, kama anavyosema Mtakatifu Yohane Paulo II kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya yanafukarisha jamii, yanapunguza nguvu za kibinadamu na kimaadili; yanaathiri uwezo wa mtu kuishi na kushiriki katika maboresho ya jamii husika. Lakini, waathirika hawa wanabeba ndani mwao historia binafsi, kumbe, wanapaswa kusikilizwa, kueleweka, kupendwa, kugangwa na hatimaye kutakaswa, ili kulinda na kudumisha utu, na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI aliwahi kutoa maneno makali kwa wafanya biashara haramu ya dawa za kulevya, kutambua athari wanazosababisha kwa vijana na watu wazima katika jamii na kwamba, watawajibika mbele ya Mwenyezi Mungu kutokana na matendo yao yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa kuangalia athari za biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya kimaadili kuna haja ya kufikia ukomo wa uzalishaji, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Biashara hii imepelekea maelfu ya watu kupoteza maisha yao, watu kujipatia utajiri wa haraka haraka; vurugu, ghasia na uvunjifu wa haki msingi za binadamu.

Matumizi haramu ya dawa za kulevya yanakwamisha maendeleo
Matumizi haramu ya dawa za kulevya yanakwamisha maendeleo

Matumizi haramu ya dawa za kulevya yanapandikiza mateso, mahangaiko na hatimaye, utamaduni wa kifo; kumbe kuna haja ya kuwa na ujasiri wa kijamii ili kupambana na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani ambayo pia yamesababisha madhara makubwa katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama inavyojionesha kwenye bonde la msitu wa Amazoni. Baba Mtakatifu anakaza kusema, uwekezaji katika kuzuia ndio ufunguo wa kulinda jamii na kuhakikisha mustakabali mzuri wa kizazi kijacho; kwa kulinda na kudumisha haki, kwa kuwaelimisha na kuwarithisha vijana tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu zinazomjenga mtu binafsi na jamii katika ujumla wake; kwa kuwasindikiza na kuwapatia waathirika matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika hija zake za kitume, amebahatika kutembelea Jumuiya zinazowahudumia waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya na kwamba, hivi ni vituo vinavyotekeleza dhamana na wajibu wake mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Hizi ni Jumuiya za matumaini zinazoendeshwa na Mapadre, watawa na waamini walei wanaojifunza kuwa ni Wasamaria wema. Ni katika muktadha huu, baadhi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia wameanzisha mchakato wa kuwasaidia waathirika kwa kutunga na kutekeleza sera na mikakati ya kudhibiti matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Matumizi haramu ya dawa za kulevya ni hatari sana
Matumizi haramu ya dawa za kulevya ni hatari sana

Mtandao wa shughuli za kichungaji Amerika ya Kusini “La Pastoral Latinoamericana de Acompañamiento y Prevençión de Adicciones (PLAPA)” katika Katiba yake, unatambua unywaji wa kupindukia, matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo kuwa ni tatizo na changamoto inayowaathiri watu wengi ndani ya jamii bila kujali jiografia, hali ya kijamii, kitamaduni, kidini na umri wa mtu. Licha ya tofauti hizi msingi, mtandao huu unataka kujizatiti kama Jumuiya ili kushirikishana uzoefu na mang’amuzi, ari, matatizo na changamoto za matumizi haramu ya dawa za kulevya. Ni katika muktadha huu, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA mwezi Novemba 2023 liliadhimisha mkutano wake wa mwaka ulionogeshwa na kauli mbiu “Kuwawezesha vijana kama mawakala wa amani na matumaini.” Vijana walioshiriki katika mkutano huu, waliwashukuru Maaskofu kwa kuwajengea matumaini ya ujana wenye afya bora na unaoshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, vijana wanapaswa kusimama kidete kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya; vijana waoneshe mshikamano huu na vijana wenzao. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, leo hii kuna mamilioni ya watu ambao wameathirika kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya, licha ya kashfa ya utengenezaji, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya kuendelea kushamiri sehemu mbalimbali za dunia.

Muhimu: Usalama wa watoto na vijana dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya
Muhimu: Usalama wa watoto na vijana dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya

Kanisa haliwezi kuwageuzia kisogo waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, kama ilivyokuwa kwa wakati wa Kristo Yesu, aliyejipambanua kwa kuwa karibu na waathirika, Kanisa pia linaitwa na kutumwa kuonesha ukaribu wake kwa waathirika, ili kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio, upweke na hali ya kukata tamaa, wanayokabiliana nayo waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kuna haja ya kuwajengea matumaini ya maisha mapya waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, lakini zaidi kuombea toba na wongofu wa ndani wahalifu wanaoendelea kusababisha madhara makubwa kwa vijana wa kizazi kipya. Maadhimisho ya Siku hii yaendelee kupyaisha dhamana na wajibu wa Kanisa kuombea toba na wongofu wa ndani wale wote wanaoendelea kujikita katika biashara haramu ya dawa za kulevya. Baba Mtakatifu anasema, Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani, iwe ni fursa kwa familia kuhakikisha usalama wa watoto na vijana. Ikumbukwe kwamba, mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya yanapania kulinda na kudumisha utu, heshima sanjari na kuwakirimia matumaini na maisha bora kwa watu wote!

Dawa za Kulevya 2024

 

26 June 2024, 14:53

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >