Papa Francisko: Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2024 anasema, sura na macho ya wakimbizi, yanawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasiwageuzie kisogo Papa Francisko: Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2024 anasema, sura na macho ya wakimbizi, yanawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasiwageuzie kisogo  (2024 Getty Images)

Siku ya Wakimbizi Duniani 20 Juni 2024: Msiwageuzie Kisogo Wakimbizi

Papa katika Siku ya Wakimbizi Duniani anasema, sura na macho ya wakimbizi, yanawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasiwageuzie kisogo na kukataa ubinadamu unaowaunganisha, ili kweli hadhi na changamoto za maisha, zigeuzwe na kuwa ni zao pia! Anasema, sera za Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji."

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Siku ya Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2024 anasema, sura na macho ya wakimbizi, yanawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasiwageuzie kisogo na kukataa ubinadamu unaowaunganisha, ili kweli hadhi na changamoto za maisha, zigeuzwe na kuwa ni zao pia! Anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna sababu nyingi zinazowalazimisha watu kuzikimbia au kuzihama nchi zao: Vita, Majanga asilia, Umaskini nk. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali kuta za ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi!

Msiwageuzie wakimbizi kisogo
Msiwageuzie wakimbizi kisogo

Kumekuwepo na ongezeko kubwa la vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii; Uvunjwaji wa haki msingi za binadamu; Ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula unaopelekea ongezeko la baa la njaa, utapiamlo wa kutisha, umaskini, magonjwa na ujinga. Yote haya yanapelekea idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi na nchi zao, ili kutafuta: ulinzi na usalama; hifadhi, ustawi na maendeleo yao. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya milioni 120 wanaokimbia vita, dhuluma na nyanyaso kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa sehemu mbalimbali za dunia. Lengo ni kupambana pia na biashara ya binadamu na viungo vyake; sababu zinazopelekea watu kuthubutu kuhatarisha maisha yao kwa kufunga safari zisizo na uhakika pamoja na kutafuta suluhu ya vita na migogoro mbali mbali duniani. Ushirikiano na mshikamano wa Kimataifa ni jibu makini katika kukabiliana na changamoto za wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Kuna haja pia kushirikishana nyajibu na majukumu kama kielelezo makini cha ujenzi wa mshikamano na umoja wa udugu. Ni katika muktadha huu, Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 20 Juni, inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani, siku iliyoteuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuwaenzi wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia; watu wanaolazimika kuhatarisha maisha yao ili kutafuta hifadhi, usalama, ustawi na maendeleo yao.

Siku ya Wakimbizi Duniani 20 Juni 2024
Siku ya Wakimbizi Duniani 20 Juni 2024

Hii ni siku inayopania kulinda sanjari na kuboresha hali ya maisha ya wakimbizi na wahamiaji. Kwa mara ya kwanza, Siku ya Wakimbizi Duniani iliadhimishwa tarehe 20 Juni 2001, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 50 ya Mktaba wa Umoja wa Mataifa wa Mwaka 1951 “Convention Relating to the Status of Refugees” mintarafu hadhi ya wakimbizi duniani. Awali Siku hii ilijulikana kama Siku ya Wakimbizi Barani Afrika, kabla ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuiteuwa Siku hii maalum, mwezi Desemba 2000 na kuanza kuadhimishwa rasmi tarehe 20 Juni 2001. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR linasema, kumekuwepo na ongezeko kubwa la wakimbizi na wahamiaji, hadi kufikia watu milioni 120 katika Kipindi cha Mwezi Mei 2024 na idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji ni wale ambao wameathirika kwa vita. Sababu kubwa ya ongezeko maradufu la wakimbizi kadiri ya takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, ni mgogoro wa Sudan ambao umechangia raia milioni 10.8 kuwa wakimbizi mpaka mwishoni mwa mwaka 2023. Mataifa yanayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi ni: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Myanmar, mamilioni walikimbia makazi yao kwa mapigano ambapo inakadiriwa mpaka mwishoni mwa mwaka jana hadi watu milioni 1.7, sawa na asilimia 75% ya idadi ya watu wa Mataifa hayo waligeuka kuwa wakimbizi. Ukanda wa Gaza umeongeza wakimbizi wa Palestina na Siria hadi kufikia milioni 13.8. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kumekuwepo na ongezeko la watu 68.3 ya idadi ya wakimbizi sawa na ongezeko la asilimia 50%.

Siku ya Wakimbizi Duniani
20 June 2024, 14:29