Teknolojia ya Akili Mnemba: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu Zizingatiwe!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 5 Juni 1993. Hii ni kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo la mfuko huu ni kufanya upembuzi yakinifu, kufafanua na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia: wafanyabiashara na wataalam katika medani mbalimbali za maisha; kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Vatican katika kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mfuko huu umeendelea kuwa nyenzo muhimu sana ya ushuhuda wa uwepo fungamani wa Kanisa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mfuko huu unawajumuisha viongozi wa Kanisa Katoliki, wasomi na wataalamu kutoka katika nyanja mbalimbali. “Akili mnemba ya kuzalisha na Dhana ya Kitekonolojia: Jinsi ya Kukuza Ustawi wa Binadamu, Utunzaji Bora wa Mazingira na Ulimwengu wa Amani.” Akili mnemba ni mada tete sana katika maisha ya mwanadamu kwani ina athari zake katika uchumi, maisha ya kijamii na inaweza kuleta madhara makubwa kwa ubora wa maisha, mahusiano na mafungamano ya kibinafasi na ule wa Kimataifa; amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wa Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, Jumamosi tarehe 22 Juni 2024.
Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 ilinogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Mnemba na Amani”: “Artificial Intelligence and Peace”: Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia kuhusu: Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kuelekea ujenzi wa amani; Wakati ujao wa akili mnemba: kati ya ahadi na hatari; Teknolojia ya siku zijazo: mashine ambazo "hujifunza" peke yake; Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia; Masuala motomoto kwa maadili; Je, tugeuze panga ziwe majembe? Changamoto za kielimu na hatimaye, ni changamoto za maendeleo ya sheria za Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, akili ni kati ya zawadi ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu kwa kumuumba kwa sura na mfano wake, akampatia akili ya kuweza kujibu upendo wa Mungu kwa uhuru zaidi na kwamba, kwa njia ya kazi na maarifa yake, binadamu daima amefanya bidii ili kuyaendeleza maisha yake. Huu ni mwaliko wa kushirikiana na mpango wa Mungu ili kujenga na kudumisha amani miongoni mwa watu wa Mataifa; kukuza uhuru, ushirika wa udugu wa kibinadamu, ili kuboresha maisha ya binadamu na hatimaye ulimwengu. Mama Kanisa anatambua maendeleo makubwa ya sayansi ambayo yameboresha maisha ya watu wengi, mwaliko ni kuwajibika barabara na matumizi haya makubwa ya sayansi na teknolojia, ili kuepuka hatari sanjari na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Maendeleo haya makubwa yanajionesa katika ulimwengu wa kidigitali na wasi wasi wake kwa siku za mbeleni.
Teknolojia ya siku zijazo: Kumekuwepo na maboresho makubwa katika maisha ya watu kutokana na kuboreka kwa njia za mawasiliano, huduma kwa umma, elimu pamoja na ongezeko la ulaji; mwingiliano na mafungamano ya kijamii, mambo yanayojionesha katika uhalisia wa kila siku ya maisha ya watu. Kuna haja ya kufahamu kwa kina maana ya sayansi na teknolojia pamoja na athari zake kwa binadamu. Kumbe, teknolojia ya akili mnemba lazima izingatie mambo yafuatayo: Iwe ni shirikishi, inayotekelezeka kwa misingi ya ukweli na uwazi; usalama, usawa, pamoja na kulinda siri za watu na kwamba, teknolojia ya akili mnemba iwe inategemewa. Kuwepo na chombo kitakachodhibiti masuala ya maadili, haki msingi za watumiaji na waathirika. Teknolojia ya akili mnemba itumie pia tafiti za kiteknolojia na kisayansi, ili kulinda na kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili haki iweze kuchangia katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani duniani. Teknolojia ya akili mnemba ni teknolojia ya siku zijazo na kwamba, itakuwa na athari kubwa katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu, kwa kuweka msingi wa ufahamu hadi kufikia ukweli na kamwe teknolojia hii isitumike kwa ajili ya kusambaza habari za kughushi na hivyo kusababisha njia za mawasiliano ya jamii kutoaminika, kwa kujikita katika masuala ya ubaguzi; kuingilia katika michakato ya uchaguzi, kwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kukomaza ubinafsi; mambo ambayo yanaweza kuwa ni kikwazo kikubwa cha kutafuta na kudumisha amani.
Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia kwani kuna hatari ya kushindwa kuchakata takwimu nyingi na hivyo kusababisha ukosefu wa haki na maamuzi mbele katika mazingira zilimotoka takwimu hizi, kumbe, binadamu anapaswa kufanya tathmini na hatimaye kutoa uamuzi wa mwisho. Hapa, kuna haja ya kufikiria ukomo katika teknolojia kamwe teknolojia isitumike kuzalisha utajiri kwa watu wachache ndani ya jamii na hivyo kuhatarisha demokrasia na amani katika ujumla wake. Mwenyezi Mungu aliwakirimia wanadamu Roho wake ili wapate ustadi, ufahamu na ujuzi katika kila kazi. Kwa hiyo sayansi na teknolojia ni bidhaa nzuri za uwezo wa ubunifu wa wanadamu na kwamba, teknolojia ya akili mnemba hutokana hasa na matumizi ya uwezo huu wa kazi ya uumbaji uliotolewa na Mwenyezi Mungu. Teknolojia ya akili mnemba ni chombo chenye nguvu sana kinachotumika katika medani mbalimbali za shughuli za mwanadamu. Kutoka katika dawa hadi katika ulimwengu wa kazi; utamaduni, mawasiliano, elimu na siasa na kwamba, matumizi ya teknolojia ya akili mnemba yanaathari zake katika maisha ya mwanadamu, mahusiano na mafungamano yake kijamii na hata jinsi ya kufikiria utambulisho wao kama wanadamu. Suala la teknolojia ya akili mnemba huchukuliwa kama utata, kwani kwa upande mmoja hutoa msisimko unaowezekana na wakati mwingine husababisha hofu kwa matokeo ambayo hutangulia. Kumbe hapa kuna hisia ya maendeleo makubwa yanayotokana na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba na wakati huo huo, woga unashamiri kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba.
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 14 Juni 2024 wakati akishiriki mkutano wa Viongozi Wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7 alisema kuna wito wa kutafuta, kujenga na kudumisha amani sanjari na ubinadamu katika enzi ya akili mnemba. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mapinduzi ya teknolojia ya akili mnemba; teknolojia inayotumia hali ya binadamu, lakini bado ni tete sana; Utaratibu wa msingi wa teknolojia ya akili mnemba; umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na kanuni maadili; Siasa inayohitajika katika kujenga udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii, ili kukuza na kudumisha amani ulimwenguni sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, mapinduzi ya teknolojia ya akili mnemba yamesaidia kuunda mfumo mpya wa kijamii, kiasi kwamba, teknolojia hii inaweza kusaidia mchakato wa demokrasia, tafiti za kisayansi pamoja na kupunguza kazi zinazofanywa na mashine. Lakini maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba yanaweza kusababisha kukosekana kwa uwiano wa maendeleo kati ya nchi changa duniani na nchi zilizoendelea; ni teknolojia inayoweza kuibua matabaka kiasi cha kujenga utamaduni wa kutupa badala ya utamaduni wa kuwakutanisha watu. Maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba ni tishio linalohitaji tafakuri ya kina, ili kuweza kubaini changamoto zinazoletwa na teknolojia ya akili mnemba.
Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake kwa wajumbe wa Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kushirikiana na Taasisi ya Kipapa ya Mtakatifu Augustiani kwa ajili ya Mababa wa Kanisa “Augustinian Patristic Pontifical Institute” amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kwani kwa hakika, teknolojia ya akili mnemba inaweka mbele ya Jumuiya ya Kimataifa changamoto pevu hasa katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Nafasi ya binadamu katika maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba lazima yapewe kipaumbele cha kwanza, ili maendeleo haya yaweze kuleta usawa, ustawi na maendeleo ya kijamii. Hatari kubwa ya maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba yameanza kujionesha katika: Soko, uchunguzi wa magonjwa ya binadamu, utabiri kuhusu ulaji na hivyo kuifanya teknolojia ya akili mnemba kutoa maamuzi, hali inayoathiri mchango na uwajibikaji wa binadamu katika maendeleo ya teknolojia. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika sekta ya afya, hususan: tafiti na utengenezaji wa dawa; kwenye sekta ya kilimo kwa kuzalisha zaidi ili kupambana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Kuna hatari kubwa ikiwa kama teknolojia ya akili mnemba itatumiwa katika masuala ya kijeshi, bila ya kuwa na udhibiti na uwajibikaji wa binadamu. Teknolojia ya akili mnemba inaweza kusaidia katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kumbe, teknolojia ya akili mnemba, isitazamwe tu kama kiashiria cha hatari kwa ustawi na maendeleo ya binadamu bali, teknolojia hii itumike kwa kuzingatia na kuheshimu: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu, na hivyo kuepuka matumizi ya teknolojia ya akili mnemba kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wachache ndani ya jamii.