Wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, Alhamisi, tarehe 27 Juni 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, Alhamisi, tarehe 27 Juni 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.  (Vatican Media)

Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini: Changamoto za Uinjilishaji wa Kina

Wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, Alhamisi, tarehe 27 Juni 2024 wamekutana na kuzungumza na Papa ambaye amegusia: Changamoto mamboleo katika mchakato wa uinjilishaji Amerika ya Kusini, mintarafu mageuzi yaliyoanzishwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Tume hii ni kielelezo cha huduma inayosimikwa katika busara na ufanisi mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Ushirika tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, “The Pontifical Commission for Latin America (CAL)” inaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili; dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari na ule wa shughuli za kichungaji kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wake. Hii ni sehemu ya Katiba mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katiba hii inadokeza umuhimu wa wongofu wa kimisionari sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, mambo msingi yanayoweza kulisaidia Kanisa kuonesha wazi Uso halisi wa Kristo Yesu kwa njia ya utendaji wa Sekretarieti kuu ya Vatican na mchakato wa uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa kwa wakati huu.

Wajumbe wa Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini.
Wajumbe wa Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini.

Wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, “The Pontifical Commission for Latin America (CAL)”, Alhamisi, tarehe 27 Juni 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika hotuba yake, amegusia kuhusu: changamoto mamboleo katika mchakato mzima wa uinjilishaji Amerika ya Kusini, mintarafu mageuzi makubwa yaliyoanzishwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini ni kielelezo cha huduma inayosimikwa katika busara na ufanisi mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Ushirika tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Tume hii ya Kipapa katika mkutano wake wa mwaka huu 2024, inajikita katika tafakari kuhusu uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; mateso ya Kristo Yesu yanayojionesha katika maisha ya watu wa Mungu Amerika ya Kusini; Uinjilishaji unaofumbatwa katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu na huduma makini ya Tume hii kwa Mabaraza ya Maaskofu pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caraibi, CELAM pamoja na Sekretarieti Kuu ya Vatican. Huu ndiyo mwelekeo wa mabadiliko ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili Kanisa zima liweze kukumbatia na kushuhudia mwono wa kweli wa Kristo Yesu, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa kujikita katika uaminifu katika wito na asili yake katika umoja kwa kutambua kwamba, hii ni Kanisa linalosafiri linaitwa na Kristo Yesu kuendeleza marekebisho ya Kanisa bila kukoma kwa sababu hii ni taasisi ya kibinadamu na kidunia. Rej. Unitatis Redintegratio, 6.

Changamoto za Uinjilishaki katika Nchi za Amerika ya Kusini.
Changamoto za Uinjilishaki katika Nchi za Amerika ya Kusini.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linaondokana na Taalimungu hasi, ili kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa uliotakaswa na kupyaishwa kama ambavyo Kanisa linaendelea kutekeleza kwa njia ya Katiba mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini inapaswa kuwa ni chombo cha huduma ya shughuli za kichungaji mintarafu Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini ni kielelezo cha huduma inayosimikwa katika busara na ufanisi mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili kujenga na kudumisha umoja, tayari kwa Kanisa la Kristo Yesu Amerika ya Kusini kuanza kutembea pamoja, huku likiongozwa na Roho wa Bwana, tayari kuonesha ile sura ya Kimisionari na Huduma ya Kanisa kwa ajili ya Amerika ya Kusini; kwa kufikiri, kuamua na kutenda Kisinodi. Tume hii ya Kipapa katika unyenyekevu wake, upendo na ukaribu wa Bikira Maria, visaidie kukuza na kudumisha upendo na ukweli na kwamba, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unakwenda sanjari na umoja wa Kanisa. Hata waamini walei wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kujikita katika mang’amuzi ya wongofu wa kisinodi, tayari kupokea dhamana na majukumu; kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho wa kidugu, ili kuibua mwelekeo mpya Amerika ya Kusini na kwamba, hii ni sehemu pia ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Tume iendelee kuhimiza, kuhamasisha na kuchochea uhuru ili kila ukweli wa Kikanisa na Kijamii utambue njia yake, pia kufuata mienendo ya Roho Mtakatifu katika ushirika na Kanisa la Kiulimwengu. Tume ijenge madaraja ya kuwaunganisha na kuwashirikisha kama sehemu ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu; tayari watu wa Mungu Amerika ya Kusini waweze kutembea pamoja.

Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya kusini: Changamoto za uinjilishaji
Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya kusini: Changamoto za uinjilishaji

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Kanisa linaitwa na kutumwa kutangaza Injili ya matumaini, kwa kujiaminisha kwa Bikira Maria, katika wasi wasi, shida na matarajio yao. Huu ni mwaliko kwa Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, kushiriki kikamilifu, kwa kutoa mwaliko kwa watu wa Mungu Amerika ya Kusini kufanya hija ili kutangaza na kushuhudia ujumbe wa matumaini ambao watu wanapaswa kuugundua na hatimaye, kuusikiliza. Bikira Maria wa Guadalupe, aendelee kuwatia shime, ili wajenge Kanisa linalosimikwa katika umoja mintarafu mwono wa Kristo Yesu, kama pia Jumuiya yao inavyotakiwa kuwa!

Tume Amerika ya Kusini
27 June 2024, 15:28